Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inakwenda kutekeleza ujenzi wa bwawa la maji la Kidunda mkoani Morogoro litakalotumika kutega maji wakati wa mvua.
Rais Samia amesema hayo jana, wakati akizindua miradi ya maji Kigamboni, kukabidhi mitambo ya kuchimba visima na ujenzi wa mabwawa na kukabidhi eneo la ardhi kwa mkandarasi wa mradi wa bwawa hilo la maji Kidunda.
Amesema bwawa hilo lenye thamani ya sh. bilioni 329 litakalojengwa kwa kutumia fedha za ndani litawezesha kuwepo uhakika wa maji kwa kipindi cha mwaka mzima jijini Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani ambayo kwa sasa yanategemea maji ya Mto Ruvu.
Ujenzi wa bwawa hilo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu 2022 hadi 2025 ambao utakapokamilika licha ya matumizi ya kawaida utachochea kasi ya maendeleo ya viwanda katika mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, mradi wa maji wa Kigamboni utaimarisha huduma ya maji katika maeneo ya Temeke, Ilala na Kinondoni hivyo kupunguza ukali wa mgao wa maji.
Rais Samia ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha inasambaza maji kwa wananchi katika wilaya ya Kigamboni kwa asilimia 100 huku akiitaka Wizara ya Maji kutoa elimu kwa wananchi kuacha kuchoma misitu ovyo, kuchepusha maji na kuingiza mifugo hasa wananchi wanaoishi kando ya vyanzo vya maji kwani vitendo hivyo husababisha upungufu wa maji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuwasha pampu ya kusukuma maji kwenye tanki kubwa la maji kwa ajili ya usambazaji kwa wakazi wa maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam, lilopo Kigamboni, jana, Novemba 11, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiwakabidhi mfano wa ufunguo, Waziri wa Maji Jumaa Aweso na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga, baada ya kuzindua na kugawa magari ya kuchimbia visima virefu na mabwawa sehemu mbalimbali nchini kwenye hafla iliyofanyika Kigamboni Jijini Dar es Salaam, jana, Novemba 11, 2022.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na Wananchi kwenye hafla ya uzinduzi wa Mradi wa maji Kigamboni ambao unatoa lita milioni 70 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam, jana, Novemba 11, 2022. (Picha na Ikulu)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇