Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Jamii kwa Mashirika ya Umma (PSSSF), CPA Hosea Kishimba amesema kuwa mfuko huo umelipa mafao yote yaliyorithiwa kiasi cha Shilingi 1.02 trilioni ndani ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO jijini Dodoma Novemba 9, 2022, kuhusu utekelezaji wa majukumu yao, CPA Kishimba amesema utekelezaji wa jambo hili haukuwa rahisi lakini kwa umahiri mkubwa jukumu hilo lilikamilishwa kwa ufanisi.
NDUGU MSOMAJI NAKUOMBA UENDELEE KUSOMA MAMBO MENGINE ALIYOJIRI KWENYE MKUTANO HUO
Ulianzishwa Mwaka 2018 kupitia Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma Namba 2 ya Mwaka 2018. Mfuko huu ni matokeo ya kuunganishwa kwa iliyokuwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya GEPF (1942), LAPF (1944), PPF (1978) na PSPF (1999).
#Madhumuni makuu ya kuunganishwa kwa Mifuko hii ni kuleta uendelevu wa Mifuko, kuondoa ushindani usio na tija, kupunguza gharama za uendeshaji na kuwianisha mafao yanayotolewa na Mifuko ya pensheni
#Thamani ya Mfuko wa PSSSF kwa mwaka 2018 ilikuwa ni Shilingi trilioni 5.86 na hadi kufikia Septemba 30, 2022 thamani ya Mfuko imefikia Shilingi trilioni 7.72.
#
#Gharama za uendeshaji wa Mfuko zimepungua kwa mwaka kutoka Shilingi bilioni 128.93 mwaka 2018 hadi Shilingi bilioni 68.83 sawa na kushuka kwa asilimia 46.61.
#Kuanzia tarehe 1 Julai, 2022, wanachama wote wa mifuko ya pensheni wanalipwa mafao ya uzeeni kwa kutumia kanuni zinazofanana ambazo zinalipa mafao bora na kuwezesha mifuko kuwa endelevu.
#Hadi kufikia Juni, 2022 Mfuko umefanikiwa kuandikisha wanachama wapya 61,007
#Hadi kufikia mwezi Juni 2022, Mfuko wa PSSSF ulikuwa na uwekezaji wenye thamani ya Shilingi trilioni 7.5 ambapo maeneo yaliyowekezwa ni Hatifungani za Serikali, Majengo ya Biashara, Uwekezaji wa viwanda, Hisa za Makampuni, Amana za mabenki, Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.
#Kutokana na uwekezaji huu, Mfuko hupata faida ya uwekezaji wastani wa asilimia 8 kwa mwaka, ambayo ni juu ya Mfumuko wa bei na hivyo kufanya uwekezaji huu kuwa na tija. Kwa mwaka wa fedha ulioshia Juni 2022, Mfuko ulipata faida ya uwekezaji kiasi cha Shilingi bilioni 581.72.
#Mfuko umewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 500 katika soko la hisa la DSM kupitia makampuni mbalimbali yaliyoorodheshwa. Uwekezaji huu mkubwa wa Mfuko unasaidia kukuza soko la mitaji nchini na kuchochea uchumi na maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja.
#Mfuko wa PSSSF ni mmoja ya waendelezaji milki wakubwa nchini. Mfuko unamiliki majengo ya kupangisha katika miji mbalimbali ambayo hutumika kwa shughuli za kibiashara 72%, ofisi na makazi 98%.
#Hadi kufikia mwezi Juni 2022, Mfuko ulikuwa umeshawekeza kiasi cha Shilingi bilioni 130 katika miradi ya viwanda ambapo miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
#Mfuko umelipa mafao ya jumla ya Shilingi trilioni 6.32 ikiwa ni mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko kwa mujibu wa Sheria.
#Wakati wa kuunganishwa Mifuko, kiasi kilichokuwa kinalipwa kama pensheni kwa mwezi kwa wastaafu kilikuwa Shilingi bilioni 34, lakini mpaka kufikia sasa wastani wa kiasi cha Shilingi bilioni 60 kinalipwa bila kukosa kwa wastaafu zaidi za 150,000 kila ifikapo tarehe 25 kila mwezi.
#Wakati wa kuunganisha Mifuko PSSSF ilirithi madeni ya Serikali yaliyohakikiwa yenye thamani ya Shilingi bilioni 731.40, mpaka sasa kiasi cha Shilingi bilioni 500 kimelipwa na Serikali.
*MATARAJIO YA BAADAE*
#Kuongeza vituo vya uhakiki katika halmashauri mbalimbali na kuanzisha utaratibu wa kujihakiki kwa simu janja.
#Kuhakikisha mifumo ya PSSSF inasomana na mifumo mingine kutoka taasisi nyingine za Umma ya watoa huduma
#Kurahisisha uandikishaji wanachama na uletaji wa madai kupitia mtandao (online claim submission). Utaratibu huu utasaidia kutoa huduma kwa haraka na kupunguza matumizi ya karatasi
#Kubuni mifumo mipya na salama ya TEHAMA kulingana na mahitaji ya Mfuko
#Kutumia Mifumo ya TEHAMA, asilimia 85 ikiwa malengo ni kutumia kwa asilimia 100 ifikapo 2023, katika shughuli za Mfuko hivyo kuboresha utoaji wa huduma kwa Wanachama na wananchi kwa ujumla.
#PSSSF imejipanga vizuri kuendelea kutoa elimu kwa wanachama na watanzania wote ili kuhakikisha sekta hii inafamika vyema ili kuendelea kutoa mchango katika uchumi wa nchi yetu. Mkutano huu na moja ya njia mahsusi ya kufukisha elimu kwa umma.
*ALIYOYASEMA MKURUGENZI WA IDARA YA HABARI NA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, GERSON MSIGWA*
#Leo tunapopata taarifa za mfuko kukua kwa asilimia nane ni taarifa ambazo zinatupa faraja kubwa kwani wengi walihofu juu ya kuunganishwa kwa mifuko hiyo.
#Niwapongeze PSSSF kwa kazi kubwa mnayofanya kadhalika kwa kuweka Mifumo ya usimamizi wa kazi, dunia ya leo inakwenda kidigiti hivyo mnavyokwenda namna hii Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tunafurahi kwamba mnafanya kazi kisasa.
#Kwa wafanyakazi ni muhimu kufuatilia kama michango yako inawasilishwa ili kuepuka changamoto mbalimbali wakati wa kustaafu.
#Wafanyakazi walioondolewa kazini wanatakiwa kwenda kwa Waajiri wao wa mwisho ili kupata utaratibu kabla ya kwenda kwenye mfuko husika.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇