LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 4, 2022

MKUU WA SHULE YA SEKONDARI KAWE UKWAMANI SAFINA EGHA AONYA BODABODA WANAORUBUNI WANAFUNZI WAKE

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Waendesha Bodaboda na Bajaji wenye maegesho yao jirani na Shule ya Sekondari Kawe Ukwamani katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, wamepewa onyo wakitakiwa kuacha haraka vitendo vya kuwarubuni wanafunzi hasa wa kike wa shule hiyo.

Onyo hilo kali limetolewa na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Safina Egha alipokuwa akizungumimza na Wazazi wa Wanafunzi, kuhusu mustakabali wa masuala mbalimbali yakiwemo hatma ya wanafunzi na shule yenyewe, katika mkutano na Wazazi hao uliofanyika, juzi shuleni.

"Najua katika kikao hiki wamo Wazazi ambao mnawajua bodaboda hao wenye maegesho jirani na shule hii, wapelekeeni salam, kwamba kuanzia sasa wakome na waache kabisa tabia zao za kuniharibia watoto (wanafunzi) wangu, na karipio hili ni la mwisho, wakiendelea nitachukua hatua kali ikiwemo za kisheria na kuwafukuza waondoke kwenye maegesho yao yale", akafoka Mwalimu Egha na kuongeza;

"Baada ya kufuatilia kwa muda sasa, tumegundua kuwa hawa bodaboda ni mingoni mwa chanzo kikubwa cha kuharibika watoto wetu hasa wa kike na kuingia katika kuwa na tabia mbaya. Kama mnavyojua kutokana na baadhi ya watoto mazingira ya nyumbani kwao kutokuwa rafiki kwa kujisomea wengi hubaki hapa shuleni hadi saa 2 usiku wakijisomea.

Wanapotoka wote kupitia njia ile ambako kuna maegesho ya bodaboda hawa, sasa boda boda hao hutumia changamoto ya usafiri kuwarubuni watoto wakijifanya wanawapa msaada wa usafiri kisha wanatumia nafasi hiyo kuwatongoza watoto wangu, na mnajua watoto uelewa wao ni mdogo kuhusu madhara ya ngono na kuingiliwa kinyume cha maumbile kwa watoto wa kiume, basi wanajikuta wamenasa mtegoni hadi wanazoea mambo hayo ya kishenzi".

Mwalimu Egha alisema, licha ya jitihada za walimu katika kujenga vema tabia za watoto, lakini changamoto ya mienendo mibaya kwa baadhi ya wanafunzi imeendelea kuwepo, jambo ambalo aliwataka wazazi kutoa ushirikiano mkubwa na Walimu ili kwa pamoja wakabiliane katika kuwajengea watoto (wanafunzi) misingi mizuri ya sasa na baadaye.

"Ndugu wazazi, tazameni hapa tuna kazi kubwa sana ya kusaidiana na ninyi kulea watoto hawa, mzazi lazima ushughulike kujua, mtoto akitoka nyumbani amevaa vipi, amechukua nini katika begi lake, usalama wa njia anayoipita shule na anakula nini akiwa shuleni, siyo kumuacha tu mtoto afanye atakavyo. msiowaone hivi, watoto hawa wana mambo mengi sana tusiyoyajua kama hatuwafuatilii", akasema Mwalimu Egha.

Alisema, katika hali isiyo ya kwaida, asilimia 75 ya watoto (wanafunzi) wa kidato cha kwanza cha sasa shuleni hapo wana mahusiano ya kimapenzi na tena siyo mapenzi tu hadi ya kufanya ngono, tofauti na vidato vingine ambavyo alisema japo ni watundu lakini utundu wao siyo wa hatari mno kwa kuwa ni ule wa kuibiana vifaa vya kusomea na kupigana.

Katika mkutano huo, Shule iliteua wajumbe wa Kamati ya kutekeleza agizo la Serikali la shule kuwa na kaulimbiu ya 'Shule salama' ambapo zimeteuliwa baadhi ya shule ikiwemo Kawe Ukwamani kuunda Kamati hiyo ambayo wajumbe wake ni Wazazi. Pia Walichaguliwa wajumbe watatu wa Bodi ya Shule kufuatia ile iliyokuwepo kumaliza muda wake wa miaka mitatu.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kawe Ukwamani, iliyopo Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam Safina Egha akizungumza katika Kikao chake na Wazazi wa Shule hiyo, kilichofanyika shuleni hapo, juzi. Kulia ni Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Utawala Shuwena Mohammed.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages