LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 15, 2022

BARAZA LA MAWAZIRI LAELEKEZA WATAALAM KUFANYA UCHUNGUZI AJALI YA NDEGE ILIYOUA 19 NA KUJERUHI 26, BUKOBA, NOVEMBA 6, 2022

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Baraza la Mawaziri limewaelekeza wataalamu wa ndani na nje ya nchi kufanya uchunguzi wa ajali ya Ndege ATR 42-500 namba PW 494 ya Precision Air ambayo Novemba 6, 2022 iliangukia Ziwa Victoria wakati wa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera na kusababisha vifo kwa watu 19 na 26 kujeruhiwa.

Ndege hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kupitia Bukoba ilikuwa na watu 43, ambao 39 walikuwa abiria na Wengine wanne wakiwa ni Rubani na msaidizi wake na Maafisa waili wa Usalama ndani ya ndege (Air Hostess).

Taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, imesema Baraza hilo la Mawaziri limetoa maelekezo hayo baada ya kupokea taarifa ya awali juu ya ajali hiyo na hatua zilizochukuliwa mara baada ya ajali, katika Kikao chake cha dharura kilichofanyika jana jijini Dodoma, kikiongozwa na Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan.

Msigwa amesema, lengo la Baraza hilo kutoa maelekezo hayo kwa wataalam kufanya uchunguzi, ni ili kujua chanzo cha ajali na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana na ajali na majanga ya aina hiyo na kwamba hiyo ni kwa mujibu wa taratibu na sheria za Kimataifa zinazoshughulikia ajali za ndege ambapo Tanzania imesaini makubaliano ya kutekeleza taratibu na sheria hizo.

Aidha, Baraza la Mawaziri limeagiza vitengo vyote vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe.

Msigwa amsema, kwa mujibu wa taratibu za kukabiliana na ajali za ndege zipo hatua tatu ambazo alizitaja kuwa ni;  Timu ya uchunguzi wa ajali na matukio ya ndege kupaswa kutoa taarifa ya awali (Accident Bulletin) ndani ya siku 14 na kisha kutoa ripoti ya awali (Preliminary Report) itakayotolewa ndani ya siku 30 na hatimaye ripoti kamili (Final Report) itakayotolewa ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea.

"Baraza la Mawaziri linawashukuru wote waliohusika katika uokoaji baada ya ajali hii kutokea vikiwemo vyombo vya uokozi, Wananchi wa Bukoba wakiwemo Wavuvi, Wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba, Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera na wengineo.
 
Wananchi wote mnaombwa kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi ukifanyika na utakapokamilika mtajulishwa matokeo ya uchunguzi huo", amesema Msigwa katika taarifa hiyo aliyoitoa jana, jijini Dodoma.

 

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages