Waziri wa Madini, Dk. Dotto Biteko (wa pili kushoto) akizungumza na Meneja wa Idara ya Uchejuaji Dhahabu katika mgodi wa GGML, Elibariki Andrew (wa nne kulia) na Makamu Rais wa AngloGoldAshanti anayeshughulikia maendeleo kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo (kushoto) wakati alipotembelea mgodi huo juzi mkoani Geita. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong.
Makamu Rais wa AngloGoldAshanti anayeshughulikia maendeleo kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo (katikati) akifafanua jambo kwa Waziri wa Madini, Dk. Dotto Biteko alitembelea mgodi huo jana mkoani Geita. Kulia ni Katibu Mkuu wa wizara ya madini, Adolf Ndunguru akiwa pamoja na wafanyakazi wa GGML.
Waziri wa Madini, Dk. Dotto Biteko (wa pili kulia) akimsikiliza Meneja wa Idara ya Uchenjuaji Dhahabu katika mgodi wa GGML, Elibariki Andrew (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji GGML, Terry Strong (kulia). Kushoto ni Mbunge wa Geita Mjini, Costatine Kanyasu (CCM).
*************************
NA MWANDISHI WETU, GEITA
WAZIRI wa Madini, Dk. Dotto Biteko amesema Kampuni ya Uchimbaji madini ya dhahabu Geita (GGML) ndiyo kampuni uchimbaji inayoongoza Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa kutekeleza kikamilifu mpango wa Uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).
Pia amesema wizara hiyo inajipanga kutengeneza kanuni na muongozo maalumu ambao utafanya watu wote watekeleze miradi ya CSR bila kutegea.
Dk. Biteko ametoa pongezi hizo juzi alipotembelea mgodi wa GGML ili kushuhudia miradi mipya ya uchimbaji dhahabu inayofanyika katika mgodi huo mkoani Geita.
Alisema kwa muda mrefu GGML wamekuwa wakitekeleza kwa kiwango cha kuridhisha mpango huo wa CSR na mtu yeyote atakayesema mgodi huo haufanyi vizuri kwenye CSR atakuwa anawaonea.
“Mimi ningependa tuwe wa kweli, nchi hii kampuni inayofanya vizuri kwenye CSR kwenye madini ya kwanza ni GGM. Wamefanya kazi nzuri,” alisisitiza Dk. Biteko.
Aliongeza kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na wananchi katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii zinazozunguka migodi hususani, katika ujenzi wa hospitali, shule, vifaa vya tiba ili jamii ipate huduma bora.
Alisema ziara yake ililenga kuona hali ya mgodi baada ya kuhama kutoka kwenye uchimbaji wa shimo la wazi kwenda kwenye uchimbaji wa chini kwa chini ambao pia unazalisha.
“Hofu yetu ilikuwa ni kwamba kwa kuwa mgodi huu utakuwa kwenye hatua ya uendelezaji, tulidhani utashuka lakini sasa tunafurahi kwamba mgodi wamejitahidi kuweka uzalisha kuwa kwenye kiwango kinachotakiwa,” alisema.
Aidha, Makamu Rais wa AngloGoldAshanti anayeshughulikia maendeleo kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo alisema kampuni hiyo inaendelea kushirikiana na wananchi ili kujenga mahusiano mazuri katika mazingira yote yanayozunguka mgodi.
Pia, alimshukuru Dk. Biteko kwa kuipongeza GGML kwa namna kampuni hiyo inavyojitaidi kwenye kununua bidhaa na kutumia huduma za kitanzania.
“Mtafahamu kwamba mgodi huu umekuwa wa uchimbaji wa wazi tangu kwa miaka 15, kuanzia mwaka 2002 hadi 2015… kuanzia mwaka 2015 tumeanza kuhamia chini kwa chini, kufikia leo tuna miradi mitatu mikubwa, mradi wa Star and commet, Nyankanga na Geita hill ambayo yote inazalisha. Pia miradi hii inasaidiana na miradi ya wazi ya Nyamlilima,” alisema.
Aidha, aliongeza asilimia kubwa ya bidhaa za mgodi huo sasa karibu asilimia 70 ya fedha inayotumiwa na GGML inanunua bidhaa kutoka Tanzania.
Shayo alisema kuwa, lengo la kampuni ya GGML ni kuhakikisha kuwa inaendelea kuwa kinara kwa kufanya vizuri ili watu wavutiwe kuwa mwajiriwa wa GGML na wote wanaozunguka mgodi huo kuwa na ujirani wa manufaa.
Kwa upande wake Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu (CCM) aliipongeza GGML kwa kushirikisha kikamilisha wazawa wa Geita na watanzania kwa ujumla katika utoaji wa huduma mbalimbali ndani ya mgodi.
Alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa zinazotangazwa na GGML ili kupata zabuni za kutoa huduma ndani ya mgodi huo.
“Sisi Halmashauri ya Mji wa Geita ni wafaidika namba moja kwa sababu katika taarifa kwenye CSR inayotengwa tunapata asilimia 54 ya Sh bilioni tisa ambazo tumezielekeza kwenye maeneo manne makubwa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇