Na Dismas Lyassa, Morogoro
KWA mwezi mmoja sasa nimekuwa katika safari za kikazi katika mikoa tofauti ukiwamo Mkoa wa Morogoro na wilaya zake. Siku moja usiku nikiwa maeneo ya stendi kuu ya Mkoa wa Morogoro nilikutana na baba mmoja ambaye kwa haraka niliona kama hakuwa na sababu za kuwa katika mazingira yale; yaani alikuwa amelala nje katika mazingira ambayo hayakuwa mazuri. Alionekana ni mtu mzima mwenye uso wa hekima ingawa alionekana kujawa na msongo wa mawazo.
Mwandishi wa habari Dismas Lyassa (kushoto) akiwa na Philipo Kamwilu.
Nikiwa nataka kumfuata ili kumfahamu zaidi simu yangu iliita, nikapokea na kuanza kuzungumza kwa muda mrefu, nilipogeuka ili kumfuatilia yule mtu sikumuona.
Niliuliza watu waliokuwepo pale karibu wote hawakuwa na majibu. Nikalazimika kumtafuta maeneo tofauti, sikuweza kumuona. Nikaondoka kuelekea kwenye hoteli niliyofikia.
Siku iliyofuata nikiwa Morogoro nilikutana na mtu huyo ambaye alinisimamisha na kuniomba fedha; nikalazimika kumuomba nikae nae kwa mazungumzo ili kumfahamu zaidi na kujua sababu kwanini anafanya shughuli za ombaomba wakati anaonekana kama ni mtu mwenye kuweza kujitegemea kwa kufanya shughuli ndogondogo.
“Unachosema ni kweli kabisa, sipendi kuombaomba mitaani,” alisema baba huyo aliyejitambulisha kwa jina la Philipo Kamwilu, Mtanzania kabila Msukuma anayeendesha familia kwa shughuli za kuombaomba mitaani.
Anaendelea kusema “Mimi natokeo Mtaa wa Mwembeni, Kata ya Pamba, Wilayala ya Nyamagana na hata familia yangu iko huko. Shughuli zangu zilikuwa kunyoa nywele na kilimo, shughuli ambazo zilikuwa zinaniwezesha kulea mke na watoto wangu watatu. Kwa bahati mbaya nilipata ajali ya mguu na kulazwa kwa muda mrefu, kiasi kwamba kwa sasa sijui pa kuanzia.
Kamwilu anasema mkono wake wa kulia ulikatwa akiwa mdogo baada ya viganja vyake kuungua na uji wa moto, amekuwa akifanya shughuli mbalimbali ikiwamo kunyoa kwa kutumia mkono wa kushoto, lakini kilichomuangusha ni kupata ajali kubwa na kuvunjika mguu. Alilazwa muda mrefu, aliwekewa chuma mguuni kwa muda mrefu kisha alifanyiwa upasuaji mwingine ili kulitoa baada ya mifupa kiliyovunjika kuonekana kujiunga. Hata alipotoka hospitali aliambiwa na madaktari asiwe anasimama kwa muda mrefu, kitendo kilichoyumbisha kabisa maisha yake kiuchumi na kulazimika kuuza kidogo vitu vyake vikiwamo vifaa vya kunyolea ili aweze kuendesha maisha.
Philipo Kamwilu akiwa amevuta suruali juu kuonyesha eneo la mguu ambalo lilivunjika na kumlazimu kulazwa kwa muda mrefu kitendo kilichovuruga kabisa uchumi wake.
Alipoulizwa anaweza kupata kiasi gani kwa siku anasema mara nyingi haizidi Tsh10,000, hivyo kiasi hutuma kwa mkewe ili ajili ya kulea watoto wanaoishi huko Mwanza, huku yeye akiendelea kuombaomba na wakati mwingine kulala bila kula. Yeyote anayewiwa kuwasiliana na Kamwili anapatikana kwa simu 0786 68 40 51.
"Kuombaomba sio kuzuri, natamani kuwa na biashara lakini shida mtaji," anasema Kamwilu.
Mwisho
Mwandishi Dismas Lyassa anapatikana kwa simu 0754498972
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇