Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi amesema mataifa mengi ya Afrika yamekuwa yakipoteza kesi nyingi katika mahakama za kimtaifa na mabaraza ya usuluhishi kutokana Mawakili wao kutokuwa na umahiri wa kutosha unaoendana na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na kimaendeleo.
Na kwa sababu hiyo amesisitiza haja na umuhimu kwa mawakili hao wa Serikali pamoja na wataalamu wengine wakiwamo wachumi na manunuzi kujengewa uwezo na umahili na ubobevu wa kuweza kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa.
Ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Bi. Aida Sylla na Bi. Manuela Dieng ambazo ni wataalamu kutoka Taasisi ya Kimataifa ya The African Legal Support Facitility ( ALSF) Mazungumzo hayo yamefanyika Katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu iliyopo katika Jengo la Bunge Dodoma.
ALSF ipo chini ya Banki ya Maendeleo ya Afrika ( AfDB) yenye Makao yake Makuu Abidjani, Cote d’Ivoire. Na inato pamoja na mambo mengine ushauri wa kisheria katika nchi za Afrika pamoja na mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu katika nchi hizo.
Wataalamu hao wapo Mkoani Dodoma kwaajili ya mafunzo mafupi ya kuwajengea uwezo, umahili na ujuzi adimu wataalamu wakiwamo mawakili wa serikali katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji mkubwa ikiwamo eneo la madini, mafuta na gesi.
“Wataalamu wetu hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla wakiwamo wanasheria, wachumi na watu wa manunuzi wanakabiliwa na changamoto nyingi,tunahitaji kuwajengea uwezo na umahili wa mara kwa mara, Afrika tunapoteza kesi nyingi kwasababu tunapungukiwa ujuzi na utaalamu wa kiwango cha kimataifa, nipende kutoka shukrani zangu za dhati kabisa kwa ALSF kukubali ombi la Ofisi yangu la kuja kutoa mafunzo huu ni mwanzo mzuri wa ushirikiano endelevu” akabainisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha amesema, amefurahishwa pia kwamba miongoni mwa wataalamu watakao shiriki mafunzo hayo wapo kutoka Tanzania Visiwani kwa kile alichosema yapo masuala mtambuka yanayohusu pande mbili za Muungano ambayo wataalamu wake wanapaswa kuwa na uelewa wa pamoja.
Naye Bi Manuela Dieng akizungumza kwa niaba ya mwenzake, amesema ALSF imefurahi kuja kutoa mafunzo hayo na kwamba huo ni mwanzo na akamwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali Eliezer Feleshi kuainisha maeneo zaidi ambayo anadhani yanahitaji kujengewa uwezo.
Vile vile wameelezea kuridhishwa kwao na ushirikiano ambao wanaupata kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kwamba wanaendelea pia na majadiliano ya maeneo zaidi ya kuwajengea uwezo.
Baadhi ya Taasisi na Wizara zinazoshiriki mafunzo hayo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bunge, EWURA, PURA, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, Kamisheni ya Madini Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mazungumzo na wataalam Bi. Aida Sylla na Bi Manuela Dieng kutoka Taasisi ya Kimataifa ya African Legal Support Facility ( ALSF) wataalam hao wamekuwa na Mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana namna ALSF itakavyosaidia kuwajengea uwezo na umahili wataalamu wakiwamo Mawakili wa Serikali katika maeneo mbalimbali yenye uwekezaji mkubwa yakiwamo ya madini, gesi na mafuta. Jumla ya wataalamu 40 watapewa mafunzo katika maeneo hayo ambayo yanafadhiliwa na ALSF.
Bi Manuela Dieng kutoka ALSF ambayo ni Taasisi ya Benki ya Maendeleo ya Afrika yenye Makao yake Makuu Abidjani Cote D'Ivoire akiwa na mtaalamu mwenzake Aida Sylla ambao wapo nchini kwaajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu kutoka sekta mbalimbali. ALSF kupitia wataalamu hao wamemwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuainisha maeneo mengine ambayo wataalam wa ndani wanahitaji kujengwea uwezo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe Jaji Eliezer Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka ALSF pamoja na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ofisi ya Mwasheria Mkuu wa Serikali katika Jengo la Bunge
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇