LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 7, 2022

WCF: WAKULIMA, WAFUGAJI NA WAVUVI WALIO KATIKA AJIRA NI WATEJA WETU

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MBEYA

MKURUGENZI wa Huduma za Tathmini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dkt. Abdulsalaam Omar, amesema Maonesho ya Nanenane mwaka huu 2022 yanayofanyika jijini Mbeya, yana maana kubwa kwa Mfuko huo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo alisema kaulimbiu ya Maonesho hayo inayosema “Agenda 10/30 Kilimo ni Biashara; Shiriki Kuhesabiwa ili kutekeleza vizuri Mipango ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi,”  inaakisi moja kwa moja shughuli na mipango ya WCF kwa maana hivi sasa kilimo hiki sio kile cha mazoeza kwani kinatarajiwa kuongeza ubora na kuthaminiwa kama ilivyo biashara zingine hili ni jambo kubwa la kukuza uchumi wa nchi nasisi WCF tunaipongeza sana Serikali ya Awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kama ulivyosikia siku ile ya ufunguzi wa Maonesho haya, Serikali imedhamiria kukifanya kilimo chetu kuwa cha Biashara, na ndio maana kauli mbiu inataja Kilimo ni Biashara, kwa hivyo hapa unazungumzia ajira za wafanyakazi.” Alisema

Unapozungumzia masuala ya ajira maana yake moja kwa moja WCF inaingia hapo kwa hiyo wote walioajiriwa rasmi  ni wadau wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na pindi wanapopatwa na changamoto za ajali au magonjwa yanayotokana na kazi wanapokuwa wanatekeleza shughuli zao za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kwa namna moja ama nyingine watastahili kulipwa fidia, alisisitiza Dkt. Omar.

“WCF tuko hapa kukutana na Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ili na wao waweze kujua haki zao mbalimbali ikiwemo ni Mafao gani wanaweza wakapata na tunawakaribisha wananchi katika Banda la WCF.”  alisema.

Alisema kama ambavyo wamekuwa wakitekeleza jukumu la kulipa fidia kwa wafanyakazi wanapoumia au kuugua kutokana na kazi kwa mujibu wa mikataba yao ya kazi, pia wakulima,wafugaji na wavuvi nao watastahili kupata haki za kufaidika na Mafao hayo kwa vigezo vile vile vinavyotumika.

Aliyataja Mafao hayo kuwa ni pamoja na Fao la Matibabu, Fidia ya Ulemavu wa Muda, Mafao ya Ulemavu wa Kudumu na yanaweza kuwa ya mkupuo au kulingana na kiwango inaweza kuwa pensheni ya kila mwezi, naendapo itatokea amefariki basi wale wategemezi wake watalipwa fidia na Mfuko.

Kuhusu viwango vya uchangiaji katika Mfuko, Dkt. Omar alisema hivi sasa  Serikali imepunguza viwango vya michango kutoka asilimia 0.6% kwenda asilimia 0.5 kwa waajiri walio katika sekta binafsi sawa na wale wa sekta ya Umma.

Wakizungumza baada ya kutembelea banda la WCF, wafanyakazi mbalimbali wameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuuwezesha Mfuko huo kuwahudumia wafanyakazi wanapopatwa na changamoto mbalimbali wawapo kazini.

“Ni jambo jema sana Mfanyakazi anapokuwa anatekeleza majukumu yake na ikatokea amepata changamoto za kuumia, kuugua ama kufariki akiwa kazini aweze kupata haki yake ya kufidiwa, ni kitu kizuri na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuuwezesha Mfuko huu kutekeleza majukumu yake.” Alisema Bw. John Chazi ambaye ni Mfanyakazi kwenye Chuo Cha Kilimo Inyala, Mbeya.

Mfanyakazi mwingine wa jijini Mbeya Bw. Aloyce Gonzaga alisema yeye amepata Elimu zaidi kwani alikuwa anausikia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na aliamua kutembelea banda la WCF  ili kupata uelewa zaidi wa namna gani mfanyakazi anaweza kufidiwa endapo atapata madhila yoyote akiwa kazini.

Aidha Afisa Mfawidhi wa WCF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi. Rose Satta ametoa wito kwa wafanyakazi kutoka sekta zote walio katika ajira rasmi kwenye Kanda hiyo kutembelea Ofisi za WCF Kanda zilizoko jijini Mbeya.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Mfuko  wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bi. Laura Kunenge, akifafanua jambo wakati akitoa elimu kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi na shughuli za Mfuko huo kwa Mfanyakazi huyu aliyetembelea banda la WCF kwenye Maonesho ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya Agosti 7, 2022.
Afisa Matekelezo WCF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Ayoub Bendera, (kushoto) akitoa elimu ya fidia kwa wafanyakazi hawa kutoka Wizara ya Kilimo jijini Mbeya.
Afisa Mfawidhi wa WCF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi. Rose Satta (kushoto), akitoa elimu ya fidia na shughuli zinazotekelezwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi WCF kwenye banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya Agosti 7, 2022.

Utoaji elimu ukiendelea.
Afisa Mfawidhi wa WCF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bi. Rose Satta akimpatia zawadi Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Profesa Mkumbukwa Angelo Mtambo, (kushoto)  alipotembelea Banda la WCF. Kulia ni Afisa wa WCF, Bi. Aruna Mwakanyamale.
Afisa Mfawidhi wa WCF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bi Rose Satta akimpatia zawadi Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa (kushoto) alipotembelea Banda la WCF. Kulia ni afisa wa WCF, Bi. Aruna Mwakanyamale.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele, mkoani Rules, Mhe. Filberto Hassan Sanga (mwenye T-shirt nyekundu), Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo M. Buswelu (mwenye T-shirt ya Blue) wakimsikiliza Afisa Matekelezo wa WCF, Bw. Ayoub Bendera, walipotembelea Banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages