Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na kijana mnufaika wa fani ya ufundi Cherehani, Honolina Mayondi wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya wananufaika na programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo, katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Nyamidaho VTC Kasulu, mkoani Kigoma.
Mwanagenzi kutoka chuo cha Nyamidaho VTC Kasulu, Henrico Daniel (katikati) akieleza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alipofanya ziara katika chuo hicho ikiwa ni sehemu ya kukagua maendeleo ya wananufaika na programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (wa tatu kutoka kushoto) akiangalia nguo iliyoshonwa na vijana wa fani ya ufundi cherehani wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya wananufaika na programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo
Na: Mwandishi Wetu – Kasulu, KIGOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia Programu ya Taifa Taifa ya Kukuza Ujuzi ili kuweza kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki zitakazo wawezesha kumudu ushindani katika soko la ajira.
Mheshimiwa Ndalichako ameyasema hayo Agosti 4, 2022 wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Nyamidaho VTC Kasulu, mkoani Kigoma kwa lengo la kukagua maendeleo ya wananufaika na programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo.
Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambapo kupitia programu hiyo fursa za mafunzo ya stadi za kazi imekuwa ikitolewa kwa vijana hivyo, kuwataka vijana nchini kuchangamkia fursa hiyo ili kupatiwa ujuzi utakao wawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi na hatimaye kujiajiri, kuajiriwa ama kuajiri wenzao.
“Asilimia 55 ya nguvu kazi ya taifa ni vijana hivyo, haipendezi kuona fursa zinatangazwa na wanaojitokeza ni vijana wachache, wakati wengi wamekuwa wakilia hawana shughuli za kufanya, tunategemea fursa hizo zinapotangazwa vijana watajitokeza kwa wingi,”
“Niwasihi vijana kuchangamkia fursa ambazo serikali inazitoa kwa sababu dhamira ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kuona vijana wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa maendeleo ya taifa,” alisema Waziri Ndalichako
Waziri Ndalichako alifafanua kuwa, katika maeneo ya miji zinapotangazwa fursa hizo kwa vijana hujitokeza kwa wengi tofauti na maeneo ya vijijini, hivyo amehimiza watendaji wa Halmashauri na Kata kuendelea kutoa hamasa kwa vijana katika maeneo yao ili waweze kushiriki katika mafunzo yanayotolewa na Ofisi hiyo kupitia Programu ya Taifa Taifa ya Kukuza Ujuzi.
Aliongeza kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imepanga kuendelea kupanua wigo wa wanufaika kwa kuongeza fani kulingana na mahitaji ya soko la ajira, sambamba na kujenga vituo atamizi vya kulea ujuzi wa vijana “Common facilities for Youth Skills Development” kwenye kanda tano nchini ambapo kupitia vituo hivyo, vijana watapata fursa ya kuendelea na mafunzo yao kwa vitendo, kuanzisha shughuli za uzalishaji mali na wataweza kujiingizia kipato kutokana na shughuli watakazokuwa wanafanya kwenye vituo hivyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isack Mwakisu, aliwataka vijana hao kuthamini jitihada zinazofanywa na serikali kwa kuwapatia ujuzi na stadi za kazi zitakazowasaidia kuondokana na changamoto ya ajira.
Akizungumza awali, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Nyamidaho VTC, Bw. Hamenya Ntabaye, alieleza kuwa mafunzo hayo ya Uanagenzi yamekuwa ni chachu ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa fani mbalimbali zitakazowasaidia kujiajiri na kuajiriwa.
Wakiongea kwa nyakati tofauti vijana wanaonufaika na mafunzo hayo ya Uanagenzi katika chuo hicho wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuthamini mchango wa vijana na kufadhili mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kujiajiri na pia waweze kuchangia katika maendeleo ya taifa lao.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇