Na Issa Michuzi, Birmingham
Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola inafungwa rasmi leo katika Uwanja wa Alexander jijini Birmingham, Uingereza, huku jiji la Victoria, Australia, likiwa ndilo linalokabidhiwa mikoba kuandaa michuano ya 23 miaka minne ijayo.
Tanzania inamaliza ikiwa imeshika nafasi ya 32 kati ya nchi 35 ambazo zimeweza kuambulia medali, ambapo kuna takriban wanamichezo 5,054 wanashiriki katika Michezo hiyo kutoka nchi 72 na jumla ya Michezo 20 imechezwa.
Wachezaji watatu waliofanikiwa kuipatia Tanzania Medali kwenye Michezo hiyo ni Alphonce Felix Simbu ambaye ni Mshindi wa medali ya Fedha katika mbio za Marathon na washindi wa medali za Shaba katika ndondi, Yusuf Lucasi Changalawe na Kassim Selemani Mbundwike.
Kenya ni ya 13 kimsimamo kwa kuwa na jumla ya medali 21, 6 zikiwa ni za dhahabu, 5 za Fedha na 10 za Shaba huku Uganda ikiwa ni ya 16 kwa kuwa na Medali 3 za Dhahabu na 2 za Shaba.
Australia yenye jumla ya medali 176, ambazo ni dhahahu 66, Fedha 57 na Shaba 53 ndio wanaoongoza, wakifuatiwa na wenyeji Uingereza ambao wana jumla ya medali 168 kiwa ni dhahabu 55, Fedha 60 na Shaba 53.
Katika ufungaji rasmi wa Michezo hiyo ya 22 ya Madola, Shamrashamra za kila aina zimeandaliwa kutumbuiza Mataifa 72 yaliyoshiriki mashindano hayo, zikiwemo burudani za Muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali wakubwa wa Uingereza, wakiwemo UB40 na waigizaji Dexys Midnight Runners watakaoonesha sehemu ya mchezo wao maarufu katika Peaky Binders: The Redemption of Thomas Shelby.
Alphonce Alex Simbu (kati) Mshindi wa medali ya Fedha katika mbio za Marathon kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola akiwa na washindi wa medali za Shaba katika ndondi, Yusuf Lucasi Changalawe (kushoto) na Kassim Selemani Mbundwike, wakiwa kambini kwenye kijiji cha wanamichezo kilichopo Chuo Kikuu Cha Birmingham leo asubuhi. (Picha na Issa Michuzi).

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇