LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 26, 2022

RC DODOMA AZITAKA TAASISI ZA KIDINI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUONDOA UDUMAVU KATIKA JAMII


Na Mwandishi wetu – Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Senyamule amezitaka taasisi za kidini kushirikiana na Serikali katika kuwezesha wananchi teknolojia rahisi ambazo zitaweza kuwawezesha kufanya shughuli za kilimo licha ya hali ya ukame uliopo ili kusababisha wananchi kuwa na chakula cha uhakika na kupambana na tatizo la lishe duni na udumavu.

Akizungumza wakati aliposhiriki ibada ya Jumuiya ya kikristo Tanzania CCT bi. Rosemary Senyamule amesema kumekuwa na fikra potofu kuwa Mkoa wa Dodoma ni  mkame hivyo baadhi wa watu wanashindwa kujishughulisha na kilimo wakiamini kuwa Mkoa ni mkame.

“Mkoa wa Dodoma hali ya udumavu ni asilimia 34 hii namba ni kubwa sana lazima tushirikiane kuhakikisha tunawawezesha wananchi teknolojia rahisi nakumbuka nane nane mlionyesha drop irrigation ya madumu elimu ile mkiipepeka vizuri kwa wananchi wataweza kilima mboga mboga hatimaye kuondokana na udumavu” amesema Bi. Senyamule.

Amesema endapo wananchi watapata elimu juu ya kilimo hicho itasaidia sana kupunguza tatizo la lishe katika jamii na jamii itakuwa na chakula cha kutosha pia itawasaidia kupata kipato cha kaya.

Amewataka CCT kushirikiana na serikali kwani kuna mambo mengi ya kushirikiana katika kupeleka maendeleo kwa wananchi ili kuondoa umaskini miongoni mwa jamii.

“Mimi ninapoiangalia CCT siiangalii kama taasisi ya dini bali ni taasisi ambayo inamchango mkubwa kwa jamii katika kupeleka maendeleo kwa jamii ya watanzania na ninawafahamu mmefanya mambo makubwa katika kuisaidia serikali kutoa huduma kwa jamii” amesema.

Amesema serikali inampango wa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa mkoa wa Dodoma ambapo kwa Wilaya ya Chamwino kuna heka 8000 na Bahi ni 2700 yote haya ni katika kuanzisha kilimo cha pamoja(block farming)  ambayo itakwenda sambamba na ujenzi wa Mabwawa makubwa na maghala ya kuhifadhia chakula.

“Dodoma tunabahati kubwa sana kiwanda kikubwa cha mbolea kinajengwa Dodoma na serikali imetoa ruzuku kwahiyo upatikanaji wa mbolea itakuwa rahisi sana kwa wananchi wa Dodoma” amesema .

Pia amezitaka taasisi za kidini na nyingine kushirikiana na serikali katika utunzaji wa mazingira hasa katika zoezi la kupanda miti ili kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameanza kuikumba nchi yetu.

   “Hivi karibuni tutaanzisha kampeni maalumu ya utunzaji wa mazingira na upandaji miti tunaona serikali inafanya kazi kubwa katika ujenzi wa makao makuu ya nchi sisi jamii kazi yetu ni kutunza mazingira na upandaji miti” amesema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania CCT Mchungaji Moses Matonya amesema wameona ni vyema wakaandaa ibada maalumu ya kumukaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kumuelezea kazi kubwa wanayoifanya katika jamii.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages