LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 16, 2022

AG DK. FELESHI AFUNGUA MKUTANO WA 'MWANASHERIA SACCOS', ASISITIZA SACCOS KUSAIDIA KUPUNGUZA CHANGAMOTO ZA WATUMISHI IKIWEMO ADA ZA WATOTO

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dk. Eliezer Feleshi amesema kuanzishwa  kwa Vyama vya Ushirika (SACCOS) sehemu za kazi kulilenga kuwasaidia Watumishi kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo ulipaji ada za watoto, hivyo ni muhimu vyama hivyo viendelee kutekeleza kwa ufanisi lengo hilo.

AG Feleshi ambaye ni Mlezi wa  Chama cha Ushirika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  cha Sheria SACCOS ameyasema hayo alipokuwa akifungua Mkutano wa Wanachama  wa Sheria Saccos  ambao umefanyika leo  Agosti 16, 2022, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ipagala Jijini Dodoma.

Katika Mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na Maafisa Ushirika kutoka Jiji la Dodoma, pamoja na  mambo mengine wanachama watafanya tathmini na kujaidili changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili Saccos hiyo pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuifufua tena na kuifanya iwe imara kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Kwanza, niwapongeze sana kwa kufanya mkutano huu, hii ilikuwa hamu yangu ya muda mrefu mkutane ili  pamoja na mambo mengine mjadiliane na kuweka mikakati madhubuti kuhusu Saccos yetu. Nimefarijika sana” akasema Mwanasheria Mkuu  wa Serikali.

Mlezi huyo wa Sheria Saccos aakabainisha kuwa vyama vya ushirika vilitiliwa mkazo sana na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na baadaye Hayati Rais Benjamin Mkapa ambaye naye alihimiza sana kuwa, pamoja na  kipato kinachotokana na mshahara, mtumishi awe na shughuli ya kujiingizia kipato kwa kujipatia mitaji kutoka Saccos hizo.

“Hakuna mtu anayependa kuishi maisha ya shida, kila mtu anapenda kuishi kwa furaha, Vyama hivi vya ushirika  vitusaidie kuishi kwa furaha kwa kutusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwamo za kulipa karo za wanafunzi na mambo mengine. Kwa hiyo, kama mlezi ningependa kuona Saccos iliyo imara na inayosaidia kupata suluhu la changamoto za watumishi”. Akasema AG Feleshi.

Mlezi huyo wa Sheria Saccos akabainisha pia kwamba katika kuifanyia mageuzi makubwa Sheria Saccos ni vema wanachama hao kupitia mkutano huo wakajadiliana pia namna ya kuvutia wanachama wapya ikiwani ni pamoja na kuwarejesha waliowahi kuwa wanachama.

Hata hivyo amesisitiza kwamba, ili kuwa na Saccos imara na yenye kuwanufaisha wanachama ni muhimu kuwa na viongozi na wanachama waadilifu.

“Nisisitize pia suala ya maadili kwa viongozi na wanachama,  ni  bora mkabaki wachache waadilifu kuliko kuwa  na wanachama wengi wavurugaji. Baadhi ya wanachama wanapokuja kuomba mkopo mikono inakuwa mbele wakishapata  mikopo  inakuwa shinda”.

AG Dk. Feleshi pia amesema licha ya changamoto ambayo Sheria Saccos imepitia, bado inabaki kuwa Saccos yenye heshima kutokana na viongozi wengi wakiwamo Wanasheria Wakuu wa Serikali waliopita, Wakurugenzi wa Mashtaka waliopita, wanasheria wengi na ambao wengine sasa ni majaji kuwa wanachama wa Saccos hiyo.

Akasema pia kuwa, akiwa  mlezi wa Sheria Saccos itakuwa ni aibusana kusikia kwenye Sheria Saccos kuna ubadhirifu wa fedha na kwa sababu hiyo atasimima sana suala la uadilifu.

Aidha  amewataka Maafisa Ushirika kuwa karibu na vyama vya Ushirika ili pamoja na mambo mengine kubaini mapema  changamoto na kuzitafutia ufumbuzi mapema.

Awali Afisa Ushirika Yusuf Timotoli akizungumza  wakati wa mkutano huo, amesema Sheria Saccos inakabiliwa na changamoto kama ilivyo kwa Saccos nyingine nyingi zilizohamia Dodoma kutoka Dar es Salaam.

Hata hivyo amesema Ofisi yao imejitahidi kusaidia katika kuzifufua baadhi ya Saccos ikiwamo ya Utumishi na sasa watahakikisha wanaisimamia kwa  karibu Sheria Saccos ili ifikie ubora wake.

Naye Mwenyekiti wa Sheria Saccos Richard Mbaruku amesema Saccos hiyo ilikuwa na  Wanachama 91 lakini waliopo sasa na ambao wapo hai ni 49. Wanachama wa Sheria Saccos ni wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali  na  Tume ya Kurekebisha Sheria.

Manasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dk. Eliezer Feleshi ambaye ni Mlezi wa  Chama cha Ushirika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  cha Sheria SACCOS akiungumza alipokuwa akifungua Mkutano wa Wanachama  wa Sheria Saccos  ambao umefanyika leo  Agosti 16, 2022, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ipagala Jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages