LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 18, 2022

WAMILIKI WA ARDHI MABWEPANDE WALIA NA GENGE LA WAVAMIZI WA ARDHI - WAIOMBA SERIKALI KUINGILIA KATI KWA KUWAONDOA

 

*Wadai kuna vigogo wanaoratibu zoezi zima la uvamizi wa ardhi, wahatarisha maisha ya wenye hati miliki za ardhi, wafyeka mazao na mifugo.

Na MWANDISHI WETU

Wamiliki ardhi kata ya Mabwepande Wilaya ya Kindondoni waililia serikali kuwaondoa wavamizi wa ardhi wanaohatarisha usalama katika maeneo hayo. Suala la uvamizi wa ardhi limezua hali ya sintofahamu kwa wamiliki kwani wavamizi hao wanaonekana ni kama genge linaloratibiwa na vigogo, hayo yameelezwa na wamiliki leo Mabwepande, Kinondoni Dar es salaam.

Wakizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki baadhi ya wananchi ambao ardhi zao zimevamiwa walisema chanzo cha uvamizi wa ardhi ni watu waliokuwa wanachimba kokoto miaka 2000 ambao walianza kuvamia eneo la Nyakasanga na kujikatia viwanja kwenye maeneo ya watu.

Mzee Pascha Lutege alisema eneo lake alinunua mwaka 1995 na alianza kufunga ng’ombe na mbuzi ambapo mwaka 2008 alianza kulipima eneo lake na ilipofika mwaka 2012 upimaji ulikuwa umekamilika na alipata hati ya kumiliki ardhi.

“Nilikuwa nimejenga nyumba, banda la ng’ombe, banda la mbuzi, nilikuwa na tofali zaidi 3,500 na nilikuwa nimechimba bwawa kubwa kwa ajili ya kufuga samaki, lakini wavamizi wa ardhi walikuja wakavamia eneo langu lote na kufanya uharibifu mkubwa kwa kupora ng’ombe, mbuzi, walibomoa nyumba na kumkata mapanga kijana aliyekuwa anaishi eneo hilo pamoja na kuvuruga bwawa la samaki,” alisema.

Mzee Lutege alisema mwaka 2011 alifanikiwa kuwakamata waliovamia katika eneo lake na kuwafikisha katika vyombo vya sheria lakini wavamizi hao walirudi tena katika maeneo hayo na kufanya vitu vya jinai ikiwemo kubaka baadhi ya watu na kuhatarisha usalama kwa kukata watu mapanga.

Aliiomba Serikali kuwachukulia hatua kali wavamizi wote wa ardhi katika Kata ya Mabwepande ili wenye haki waweze kupewa mashamba yao kwa ajili ya kuyaendeleza.

Naye, Muzamil Karamagi alisema inawezekana wavamizi hao wa ardhi wanalindwa na wakubwa hivyo aliiomba Serikali kuweka mkakati maalum wa kuwaondoa na kurudisha ardhi yote kwa wenye hati miliki.

“Kuna siku tulikuwa na kikao cha wenye mashamba na alikuja Waziri (hakumtaja jina) lakini kuna kiongozi mmoja aliteremka kwenye meza ya viongozi akaenda kukakaa na wavamizi na akawapachika jina akawaita wakazi, kitendo kile kilitushangaza na kutusikitisha mno," alisema.

Alisema vitendo kama hivyo vinawavunja moyo wenye haki na wanadhani migogoro ya ardhi Kata ya Mabwepande inachochewa na baadhi ya vigogo wa Serikali ambao wamevamia ardhi za watu na wanaziuza kwa watu wengine kinyume cha sheria.

 

“Ni jambo la kushangaza umenimilikisha ardhi, mtu mwingine ananivamia ananipeleka Mahakamani nikamshinda tena sio mara moja inakuwaje sasa wavamizi hawa waonekane na haki kuliko sisi ambao tunayamiliki maeneo haya kisheria,” alisema.

Alisema wavamizi wa ardhi wanaumiza watu kwa maana tangu mwaka 2018 shambani kwake hajakanyaga na kipindi hicho alipoenda walikuwa na Mkuu wa Wilaya pamoja na askari lakini anashanga kuona wavamizi wanaogopwa kuliko wenye haki.

“Serikali wakati imenipa hati na nalipa kodi ya ardhi kwa mujibu wa sheria mpaka mwaka huu sina deni, sasa inanisaidiaje kuwaondoa wavamizi katika eneo langu ambalo Serikali yenyewe ilinipa hati miliki, hawa walioovamia eneo langu wanalindwa na sheria gani,” alihojia Karamagi.

Naye, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mji Mpya Kata ya Mabwepande, Mohamed Tajukhan Basta alikiri kuwepo kwa wavamizi ya ardhi katika mitaa yote mitano ya Kata ya Mabwepande ukiwemo mtaa wa Mbopo, Mabwepande, Mji Mpya, Bunju B na Kionzile.

Alisema wavamizi wa ardhi katika Kata ya Mabwepande ulianza tokea mwaka 2002/2003 ambapo katika Mtaa wake wa Mji Mpya kuna eneo la Serikali linalomilikiwa na NSSF limevamiwa na wavamizi wa ardhi ambapo ameomba kuwepo maridhiano ili wenye ardhi na wananchi wakubaliane maeneo yaliyovamiwa yapimwe ili waweze kulipa kidogokidogo.

“Nilikuwa na pendekezo kuwa hata hapa katika eneo la Serikali ambalo ni la NSSF kutumike utaratibu nzuri waliovamia pale ambao tayari wanajua kuwa ni eneo la Serikali waambiwe kuna mradi aliyekuwa tayari kulipa kwenye utaratibu wa kiserikali basi apimiwe aendelee na utaratibu na wale ambao wameshindwa basi watakuwa wameshindwa wenyewe,” alisema.

Kwa upande wake, Zulfa Sultan ambaye aliuziwa eneo la NSSF alikiri kuuziwa eneo hilo na wavamizi lakini baada ya kubaini kuwa eneo hilo ni mali ya Serikali yupo tayari inapopima ardhi katika eneo hilo aweze kufikiriwa kwani yuko tayari kununua viwanja ili aweze kumilikishwa kihalali.

Kwa upande wa Valentin Urasa, alisema ni mmiliki halali wa eneo la ekari mbili ziliziopo Mtaa wa Mbopo Mabwepande ambalo alinunua miaka 12 iliyopita alikuwa akilima mahindi, mihogo na kulikuwa miembe lakini baada ya miaka mitatu eneo lake lilivamiwa na alipoulizia kwa majirani aliambiwa kuwa maeneo hayo ni hatari.

“Baada ya eneo langu kuvamiwa nilikuja nilikutana na Mzee akaniambia alipigwa mpaka akavuliwa nguo hivyo nikaona bora nikae mbali nisije kuhatarisha uhai wangu,” alisema.

Urasa alisema eneo hilo lina hofu kubwa na wamiliki wa mashamba wanapokwenda wanaambiwa wawe na tahadhari na hata magari yao wanayaweka mbali kwa kuhofia usalama hivyo aliiomba Serikali kuwachukulia hatua wavamizi wote wa ardhi.

Baadhi ya wamiliki wa mashamba na viwanja Kata ya Mabwepande wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakizungumza na maafisa wa polisi huko Mambwepande Julai 16, 2022.
Bw. Pascal Mbikilwa (kulia) na Bw. Muzamil Mustafa Karamagi wakionyesha nyaraka za umiliki wa ardhi Kata ya Mambwepande, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam Julai 16, 2022. Wote hao wanadai kuporwa ardhi yao na wavamizi.
Mohammed Basta, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mji Mpya, Kata ya Mambwepande akizungumzia uvamizi huo.
Baadhi ya wananchi ambao ardhi yao imevamiwa wakiwa na Bi. Faiza Amour ambaye yeye aliuziwa kiwanja na watu hao waitwao wavamizi na kisha kujenga nyumba.
Bw. Muzamil Mustafa Karamagi, akitoa malalamiko yake.
Bw. Valentino Oswald Urassa, akionyesha nyaraka zake za umiliki wa ardhi yake ambayo imevamiwa.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Mabwepande, H.G. Kaduri (kulia), akizungumza na Bw. Karamagi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages