LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 18, 2022

IJA YAENDESHA MAFUNZO ELEKEZI KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA, MSAJILI MKUU CHUMA AWAFUNDA

Na Mwandishi Maalum (IJA), Lushoto
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbard Chuma amewafunda vya kutosha Watumishi wapya 58 wa Mahakama Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwaasa kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na viapo vyao.

Mh. Chuma amewafunda wakati akifungua rasmi leo Jumatatu, Julai 18, 2022, mafunzo elekezi kwa wafanyakazi hao wapya, katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kilichopo mkoani Tanga.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na kufanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).


Hili ni kundi la kwanza kati ya waajiriwa 27 waliofanyiwa usaili na kuajiriwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama hivi karibuni ambapo kuna kada mbalimbali kama Mahakimu, Maafisa Utumishi, Maafisa TEHAMA, Makatibu Mahususi, Watunza Kumbukumbu Wasaidizi na Madereva.

Akitoa hotuba ya ufunguzi, Mhe. Chuma alianza kwa kuwapongeza waajiriwa hao wapya kwa kuwaeleza kuwa ajira waliyopata hawakupata kamahisani ila imepatikana kutokana na ubora waliouonesha wakati wa usaili hivyo wanapaswa kuwa waaminifu, na wachapakazi kwa kuzingatia mikataba ya ajira, viapo na sheria za nchi katika utumishi wao.

Mhe. huma aliendelea kwa kuwasisitiza Watumishi hao wapya wa Mahakama kwakumnukuu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe Mei 31, 2021 katika hotuba yake aliyoitoa wakati akifungua Mafunzo elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Mahakama Kuu Zanzibar hapa Chuoni kwa kusema watumishi wa Mahakama wanatakiwa kuwa na uadilifu na maadili ili wafanyekazi kwa kuzingatia Katiba na masharti ya viapo.

“Watu husahau kuwa mara nyingi sheria siyo mbaya bali ni nafsi, maadili na tabia za wanaotekeleza sheria hizo. Hivyo nawakumbusha kila jalada utakalokuwa ukilitolea uamuzi ukumbuke kuwa linagusa watu halisi, linagusa uhuru wao, biashara zao, mali zao na familia zao.

Kumbukeni uwa wananchi kupitia katiba wametupa sisi Majaji mamlaka ya utoaji haki lakini wananchi wamebaki na haki zao zote za msingi”, alinukuu.

Mhe. Chuma aliendelea kwa kuwakumbusha watumishi hao kuwa maadili ni kiini cha haki, na hivyo wakati wa kutekeleza jukumu la utoaji haki wanatakiwa kuzingatia maadili ya kazi na kutoa maamuzi kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

Mhe. Chuma aliwaeleza watumishi hao wapya kuwa malengo ya mhimili wa Mahakama yatafikiwa iwapo watakuwa na nia moja na ushirikiano baina yao na watumishi wengine watakaowakuta kwenye vituo vya kazi watakavyopangiwa.

Alieleza kwamba ushirikiano huo utasaidia kufanikisha jitihada zinazoendelea za maboresho ya Mahakama ya Tanzania.

Mhe. Chuma aliwasisitiza kuwa na ushirikiano na wadau wengine kwa kuchukua mawazo mazuri na bora kutoka kwenye taasisi au idara zingine kwa kuyafanyiakazi au uyafikisha mahali panapostahili ili yalete mabadiliko kwa kuwa kazi ya kulijenga taifa ni ya wote.


Mhe. Chuma aliendelea kwa kuwasisitiza kuwa dhana ya uhuru wa mahakama haina maana ya kuvunja sheria kwa kuwa kanuni hiyo ya kikatiba inaenda sanjari na kanuni ile ya Utawala wa Sheria. Hivyo, amewataka Mahakimu kuwa ni wajibu wao kufanyakazi zao chini ya kivuli cha uhuru wa Mahakama, kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi na sio kwa kuzivunja.

Aliendelea wa kuwaasa watumishi wengine ambao sio mahakimu wakawasaidie maafisa wa Mahakama wa ngazi mbalimbali katika kufikia azma ya kutendanakutoa haki kwa mujibu wa sheria ili wasiwe chanzo cha malalamiko au kusababisha uvunjifu wa amani kutoka na nautendajikazi ambao unakiuka misingi ya utu nakatiba.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa makundi matatu ambapo kundi la kwanza la Mahakimu Wakazi na Maafisa Kumbukumbu Wasaidizi yamenza leo tarehe 18 Julai, 2022, Makundi mengine ya kada nyingine yatafuata kutegemea kumalizika12 Agosti, 2022.

IJA inajukumu la kuwajengea uwezo watumishi wote wa mahakama kwa lengo la kuboresha utendajikazi wao pia kwa mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma za utoaji haki nchini.

Pamoja na mafunzo hayo Chuo kimebobea katika kutoa mafunzo ya Stashahada na Astashahada ya sheria na vilevile Chuo kinafanya shughuli za kutoa ushauri wa kitalaamu, machapisho na tafiti mbalimbali.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbard Chuma akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Mahakamaya Tanzania yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi waMahakamaLushoto mkoani Tanga. Chini ni picha mbalimbali za watumishi wakiwa kwenye mafunzo hayo, leo👇

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages