LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 5, 2022

NSSF YAZIDI KUCHANGIA VILIVYO KUIPAISHA SERIKALI YA AWAMU YA SITA CHINI YA RAIS SAMIA KWA KUWEKA REKODI KUBWA YA MAFANIKIO

Na Khalfan Said, Saba Saba
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeonyesha kuzidi kuchangia kuipasha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan, kufuatia kuweka rekodi kubwa ya mafanikio katika utendaji wake.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Masha Mshomba, amesema thamani ya Mfuko huo sasa inakaribia Sh. Trilioni 6 kulingana na mahesabu ambayo bado hayajakaguliwa kuishia Juni 30, mwaka huu wa 2022.

Mshomba ameyasema mafanikio hayo Juzi, Julai 3, 2022, kwenye Banda la NSSF katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, kwenye Viwanja vya Maonyesho hayo vya Julius Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.

“Kwa sasa tuko Sh. trilioni 5.8, hiyo ndiyo thamani ya Mfuko na thamani hiyo imekuwa ikikua sana kufuatia mwitikio mzuri wa uchangiaji  ambao waajiri wamekuwa wakionyesha kwa takriban miaka miwili iliyopita, na tunavyozungumza sasa hivi makusanyo ya mwezi yanazidi Sh. Bilioni 110.” Alibainisha.

Mshomba alisema mwaka ulioishia tarehe 30/6 NSSF ilikusanya zaidi ya Sh.trilioni 1.3 (Sh. Trilioni 1 na Bilioni 300).

“Hili ni ongezeko kubwa ukilinganisha na makusanyo ya mwaka uliopita ulioishia tarehe 30/6/ ambapo tulikusanya shilingi  trilioni 1.1 (Trilioni 1 na bilioni 100), ongezeko la zaidi ya asilimia 18% hii inatokana na kwanza kuwajengea mazingira mazuri ya kazi watumishi yanayopelekea kuongezeka kwa ari ya kufanya kazi, matumizi ya TEHAMA yanayoziba mianya ya utendaji kazi usio wa kuridhisha, mwitikio wa waajiri na wafanyakazi,” Alifafanua.

Alisema Mfuko umekuwa ukiwapa waajiri elimu ya Hifadhi ya Jamii hali ambayo anaamini imesaidia kuongeza tija.

“Mtu akielewa umuhimu wa Hifadhi ya Jamii swala la mchango linakuwa sio la kumlazimisha kwasababu ndio njia pekee ambayo itampatia mtu kipato pale ambapo uwezo wa kufanya kazi unapokoma, Hifadhi ya Jamii unaweza kuona kama ni jambo dogo lakini umuhimu wake utauona unapofikisha umri wa miaka 60 ambao unastaafu au kwa bahati mbaya umepata ulemavu na usiweze kufanya kazi.

Lakini kama umewekeza kwenye Mfuko wetu mapato yako yako pale, watoto wako watapata, mwenza atapata na ndio maana sisi NSSF tunasema tunajali maisha yako ya sasa na ya baadaye",
Alisema.

 
Kwa upande wa ulipaji Mafao, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema mwaka jana NSSF ililipa Mafao sh. Bilioni 594 na wanajiandaa kulipa shilingi bilioni 658 mwaka unaofuata ambapo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 10%.

“Mwitikio ni mkubwa lakini tunaweza kulipa sana kwa sababu wanaoomba kulipwa Mafao ni wengi lakini pia matumizi ya TEHAMA  yanasaidia sana.” Alisema na kuongeza; "Ndio maana tunasema siku za usoni sisi dhamira yetu ni kuhakikisha kwamba tunatumia TEHAMA kwa matumizi yetu yote".

ULIPAJI KODI YA SERIKALI
Mshomba alisema, kwa upande wa Serikali NSSF imekuwa ikisaidia sana kupitia ulipaji kodi za serikali, katika miaka mitano iliyopita NSSF imelipa kodi  zaidi ya Sh. Bilioni 400,

“Kiwango hiki sio kidogo, kodi hiyo inasiadia katika kuchangia maendeleo ya taifa ya ujenzi wa miundombinu ya hospitali, shule.

Lakini pia NSSF imekuwa ikisaidia jamii kupitia (Corporate Social Responsibility) ambapo alisema kuna sera mahsusi inayowaelekeza kujikita katika mambao ya msingi kama vile Afya, Elimu, Barabara na wamekuwa wakifanya kazi kubwa kupitia mpango huo", alisema Mshomba.

Kuhusu ushiriki wa Mfuko kwenye Maonesho hayo, alisema ni fursa nzuri ya kukutana na wadau ili kutoa elimu ya masuala mbalimbali yahusuyo Hifadhi ya Jamii lakini pia kuwahudumia wanachama na wananchi kwa ujumla.

"Katika Maonesho haya tumekuwa tukitoa elimu kuhusu Kikokotoo kipya.
 

Tunatoa elimu ya kutosha kuhusu mabadiliko ambayo yametokea katika sekta ya Hifadhi ya Jamii kama mnavyofahamu kumekuwa na mabadiliko ya kikokotoo namna ambavyo tunawalipa wastaafu wetu kuanzia tarehe 1/7/2022, tumebadilisha kidogo fomula ya ulipaji.

Jambo hili lilikuwa la muda mrefu tangu serikali ya awamu iliyopita mwaka 2018 yalitoka maagizo ya kulifanyia kazi suala hilo kwa kushirikisha wadau wa vyama vya wafanyakazi, waajiri na serikali.

Uamuzi huo wa serikali ni kufuatia malalamiko yaliyotokea baada ya ile fomula iliyowekwa kufuatia mabadiliko ya sheria ya mwaka 2018." Alisema na kuongeza;

"Tunashukuru kwa jitihada kubwa zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Jambo hilo limewezekana na kuanzia tarehe hiyo tuna fomula mpya ya ulipaji Mafao.

Kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, jambo hili litabaki katika historia kama moja ya Legacy yake, na nampongeza pia Mheshimiwa Spika Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika na Wabunge kwa ujumla kwa kufanya kazi kubwa ya kulijadili swala hili kwa kina na ninahakika Waheshimiwa Wabunge watakaporudi kwa wananchi huko majimboni watakuwa wawakilishi wazuri sana kuwaelezea wananchi kuwa jambo hili lina umuhimu mkubwa kwa taifa.
 

Kufuatia mabadiliko hayo NSSF sasa italipa malipo ya mkupuo asilimia 33% badala ya asilimia 25% ya fomula ya zamani kwa hiyo ni jambo zuri na wananchama wamelipokea vizuri na maisha ya wananchama yataendelea kuboreka.” Alisema.

MATUMIZI YA MIFUMO YA TEHAMA 

Kuhusu TEHAMA Mkurugenzi huyo Mkuu alisema; "Pia tunasisitiza sana matumizi ya Mifumo ndani ya NSSF, takriban miaka miwili sasa tumekuwa tukitoa kipaumbele shughuli zetu zote za msingi tunazifanya kwa kutumia mifumo, jambo hilo ni muhimu kwa sababu kwanza linaboresha huduma lakini pia  linatupunguzia gharama za uendeshaji na wateja wamekuwa wakifurahia kwa sababu linawapa urahisi wa kufanya mambo yao na wengi hawahitaji kuja katika ofisi za NSSF, huko waliko wnaaweza kutumia simu zao au komputa wakaingia kwenye website ya NSSF na kupata huduma zetu bila ya kuhitajika kufika ofisini kwetu.

Nijambo tulilolipa kipaumbele na tunatumia maonesho haya kuzidi kuwaelkimisha wanachama wetu na wananchi kwa ujumla kuhusu matumizi ya TEHAMA na tunawaahidi kwamba hata kwa zile shughuli chache ambazo hazijawekwa katika mfumo, ndani ya mwaka mmoja huu unaokuja tunatarajia kwamba tutakuwa tumeziweka katika mfumo na tunatumaini tukifikia hatua hiyo huduma zetu zitaboreka sana na ndivyo dunia inavyokwenda na sisi NSSF tunataka kwenda kidijitali na tunataka iwe ya kidijitali kwelikweli".

TUNATOA HUDUMA ZA KAWAIDA
Kuhusu shughuli za NSSF ndani ya Sabasaba Mkurugenzi huyo Mkuu alisema; "Tuko hapo kwa ajili ya kutoa huduma pia mtu akija kuulizia michango yake, akitaka kujua hatua ya mafao yake yamefikia hatua gani aweze kulipwa. 

Pia akitaka kujisajili kama amekidhi vigezo tuko hapa kumsajili na vile vile tunatumia nafasi hii kutatua kero wengine wakija si kwamba wanataka kuhudumiwa tu lakini wanakuwa na kero zao kwa namna moja au nyingine tunatumia nafasi hii kutatua kero kwa kadiri ambavyo mazingira yaliyopo hapa, kama yatashindikana tutamuelekeza kushughulikia kero hiyo kwenye ofisi zetu".

UWEKEZAJI
Kuhusu Uwekezaji, alisema; "Tunatangaza shughuli zetu za kiuwekezaji, kama mnavyojua NSSF ni moja ya taasisi kubwa hapa nchini zinazowekeza kwa kiasi kikubwa sana, tunatumia nafasi hii kutangaza uwekezaji wetu nyumba zetu za kupangisha na kununua mfano tuna nyumba huko Wilayani Kigamboni hususan Mtoni Kijichi, Tuangoma, Dungu, maeneo ya Muongozo.

Tuna nyumba nzuri sana na mwitikio wa kununua nyumba hizo umekua ni mzuri sana, pia tunajenga jengo la Mzizima hapa Dar es Salaam na nia hasa ni  kulipangisha kwa watu watakaoendesha mradi wa hoteli pia Mwanza na lengo ni hilo hilo kulipangisha kwa mtu atakayeendesha shughuli za hoteli, tunatumia Maonesho haya kutangaza hizo nafasi ndani ya nchi lakini pia nje ya nchi ili tuweze kupata wadau hao ili kuhakikisha tunapata wapangaji au kununua nyumba hizo".

Mkurugenzi Mkuu NSSF Masha Mshomba (kushoto), Meneja wa Mpango wa Sekta Isiyo Rasmi wa Mfuko huo, Rehema Chuma (watatu kushoto) na Meneja wa Mfuko huo Mkoa wa Temeke Feruzi Mtika, wakimsikilzia Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma NSSF, Lulu Mengele wakati kiongozi huyo alipotembelea banda la NSSF kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Julai 3, 2022.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Masha Mshomba, akimsikiliza Mfanyakazi wa Mfuko huo anayesimamia masuala ya uwekezaji.

Mshomba akimsikilzia Afisa Matekelezo Mkuu, NSSF, Asha Salum.

Mshomba akibadilishana mawazo na Mameneja wa Mfuko huo, Rehema Chuma (katikati) na Feruzi Mtika.

Mkurugenzi Mkuu Masha Mshomba (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mfuko huo kwenye banda la Ushirikiano la Mifuko ya NSSF na PSSSF Julai 4, 2022

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages