LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 10, 2022

MAJALIWA: KUFANYA MAASWI SIKU YA EID NI SAWA NA KUMUASI MUNGU SIKU YA KIYAMA

Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaasa Waislam kote Nchini kusherehekea Sikukuu ya Eid kwa kutofanya maaswi akiwakumbusha warejee maneno ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwamba “Mwenye kufanya maaswi siku ya Eid ni sawa na kumuasi Mwenyezi Mungu, Allah Sub-hanahu Wata’ala siku ya kiyama”.
 
“Tunaposherehekea Eid El Adha ni vema pia tukakumbuka maneno ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam kwamba “Mwenye kufanya maaswi siku ya Eid ni sawa na kumuasi Allah Sub-hanahu Wata’ala siku ya kiyama”.

Amewaasa kuendelee kudumisha amani, upendo, umoja, mshikamano, kuhurumiana, utulivu samjari na kujiepusha na vitendo vinavyoashiria vurugu, uonevu na uvunjifu wa amani waposherehekea Sikukuu hiyo ya Eid El Adha.

Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 10, 2022) kwenye Baraza la Eid El Adha, lililofanyika katika Msikiti wa Mfalme Muhammad wa Sita wa Morocco uliopo Kinondoni, Dar es Salaam.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan anawasihi waislamu na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuonesha upendo, umoja na mshikamano hata baada ya kumalizika kwa masiku kumi bora katika mwaka yanayopatikana kwenye mwezi wa Dhul-Hijja.

Majaliwa amesema moja ya jambo adhimu katika Eid El Adha ni kuchinja na jambo hilo limethibitika katika Qur’an Tukufu pale Allah Ta’ala aliposema katika surah ya 108 ayah ya pili kwamba basi swali kwa ajili ya Mola wako na chinja kwa ajili yake.

“Hivyo basi, nami nahimiza kwamba tutumie fursa hiyo ya kuchinja kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fadhila mbalimbali alizotujalia pamoja na kuwahurumia na kuwaonesha upendo wale wenzetu miongoni mwa maskini na mafakiri. Lengo ni kuhakikisha walionacho na wasionacho tunakuwa kitu kimoja na kufurahi pamoja.”

Wakati huo huo, Majaliwa amewasisitiza wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika tarehe 23 Agosti 2022. “Tujitokeze kwa wingi kuhesabiwa na kuunga mkono zoezi hilo. Tutoe ushirikiano kwa Makarani wa Sensa na Watendaji wetu wa Mitaa katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022.”

Amewapongeza viongozi wote wa dini nchini, vyombo vya habari kwa kuendelea kuelimisha na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 linalotarajia kufanyika nchini Agosti 23. “Maendeleo yetu yanatokana na kujua idadi ya watu tulionao tuendelee kuelimisha wananchi kushiriki katika zoezi hilo.”

Majaliwa amemempongeza Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally pamoja na Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA), kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuiunga mkono Serikali katika utoaji na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo na elimu na afya.

Kwa upande wake, Sheikh Mkuu Abubakar Zubeir bin Ally amesema sense ni msingi mkubwa wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, hivyo amewaagiza Masheikh wa mikoa na wilaya waendelee kuwahimisha waislamu kote nchini wajitokeze kuhesabiwa siku hiyo itakapofika.

“Suala la sensa ni jambo muhimu na linakubalika katika sheria za uislamu. 

Kama hakuna sensa hakuna maendeleo kwa sababu hata nyumbani kwako lazima uwe na sensa kama una watoto 13 utatafuta unga na nyama ya kutosha watoto 13. Jitokezeni kuhesabiwa Serikali inataka kujua idadi ya wananchi wake ili iweze kupanga mipango ya maendeleo na utoaji wa huduma za jamii kwa wananchi wake kama afya, maji, umeme na elimu.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk. Abubakar Zubeir bin Ally  (kushoto) baada ya kushiriki katika Swala na Baraza la  EiD-ADH’HAA kitaifa  kwenye Msikiti wa  Mfalme wa Morocco Muhammad  VI uliopo Kinondoni jijini Dar es salaam, Julai 10, 2022.  Katikati ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam, Dk. Alhad  Mussa Salum. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages