LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 15, 2022

LUBINGA ASISITIZA UMAKINI UCHAGUZI CCM KUEPUKA MAMLUKI

Na Jacqueline Liana, Hai

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, amewataka wanachama wa CCM kujihadhari na wanaowania uongozi kwa masilahi binafsi.


Akizungumza na viongozi wa mashina, matawi na kata, wilayani Hai, Kilimanjaro, jana Julai 14, 2022, alisema kuna wanaoutaka uongozi ndani chama kwa sababu wanazozijua wao wenyewe.


"Tuchague viongozi bora na wazuri, wanaoendana na mazingira ya wakati huu ambapo maendeleo duniani yamekuwa ya kasi'', alisema.


Alisema CCM mkoa wa Kilimanjaro ni tulivu, hivyo ni muhimu kuwapima wagombea wa nafasi za uongozi kwa umakini na busara kuepuka kuwapa nafasi mamluki na vivuruge.


"Kuweni makini na baadhi ya wagombea, wengine ni vivuruge, kazi yao ni kuvuruga tu, wachagueni wagombea bora na wazuri," alisisitiza Kanali mstaafu Lubinga.


Suala lingine ambalo alisema ni la kuepukwa ni fitina na majungu, na kwamba mgombea atakayeshindwa katika uchaguzi hana budi kutulia na kusubiri wakati mwingine.


Aliwapongeza wanachama mkoani Kilimanjaro walivyotumia demokrasia ndani ya CCM kuwapata viongozi wa mashina na matawi.


Aliwapongeza viongozi wapya katika ngazi hizo za uongozi wa chama, na kuwataka kuchapa kazi kwa moyo ya uzalendo.


Kanali Lubinga alisema uimara wa CCM unatokana na umadhubuti katika ngazi ya shina na tawi.

 

"Heshima ya CCM inatengenezwa na shina na matawi, na ili serikali iwe imara lazima chama kiwe madhubuti," alisema.


Kanali Lubinga, alisema kwamba heshima ya CCM ni ya kimataifa tangu kilipoongoza harakati za ukombozi wa nchi za kusini wa Afrika, na miaka ya hivi karibuni kimekuwa ni msuluhishi katika kuhakikisha mataifa yakuwa na amani, akitolea mfano wa nchi jirani za Kenya na Burundi, zilipokumbwa na machafuko kwa nyakati tofauti.


Kanali Lubinga tangu Julai 12, 2022, yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya kikazi ambapo Julai 13, 2022, alifungua semina iliyowashirikisha madiwani wote wa CCM kutoka halmashauri saba za mkoa wa Kilimanjaro.


Semina hiyo ilihusu kuwajengea uwezo wawakilishi hao wa wananchi katika kutekeleza kazi na majukumu yao.


Mwanasheria wa CCM, Wakili Anthony Kanyama, akiwasilisha mada katika semina hiyo, alisema miongoni mwa sifa za diwani ni kuwa na uwezo wa kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na utaratibu bila upendeleo.


Pia, kusimamia utoaji wa huduma kwa haki, usawa bila ubaguzi wa aina yoyote.


Mwaka huu wa 2022 ni wa uchaguzi wa viongozi ndani Chama Cha Mapinduzi, tayari umefanyika katika ngazi ya shina na tawi, mchakato unaendelea kwa ngazi za kata, wilaya, mkoa na taifa.

Kanali mstaafu Ngemela Lubinga akizungumza katika semina hiyo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages