Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati akifungua mkutano wa Wadau wa uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Nzega mkoani Tabora Juni 22 Juni 2022. Wa pili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Salha Burian
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa Wadau wa uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Nzega mkoani Tabora Juni 22 Juni 2022.
(PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
…………………………………………..
Na Munir Shemweta, WANMM NZEGA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka halmashauri zote nchini kutoa kipaumbele katika utengaji bajeti za ndani ili kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi inaandaliwa katika vijiji.
“Ni vyema halmashauri zote zikatoa kipaumbele katika utengaji bajeti za ndani kuhakikisha kuwa mipango ya matumizi ya ardhi inaandaliwa katika vijiji walau vijiji 5 kwa mwaka kwa kila halmashauri ya wilaya” alisema Dkt Mabula.
Akizungumza wakati akifungua mkutano wa Wadau wa uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Nzega mkoani Tabora tarehe 22 Juni 2022, Dkta Mabula alisema nchini Tanzania kuna jumla ya halmashauri za wilaya 139 ambapo kati ya hizo ni takriban 41 sawa na asilimia 29.5 ndizo zilizoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ya wilaya.
Alisema, kutokana na kasi ndogo ya uandaaji mipango hiyo amewataka wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na Tume na wadau mbalimbali ili kuwezesha uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya wilaya hasa vijjji ili kuleta manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, alihimiza wahisani na wadau mbalimbali kushirikiana na Tume ya Matumizi ya ardhi na mamlaka za upangaji nchini kuendelea kuwezesha uandaaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
“Mpango wa uendelezaji wa mfumo wa kuandaa mipango hii ni vyema ukaandaliwa, kuboreshwa na kusambazwa katika halmashauri zetu nchini ili kusaidia kuongeza kasi ya uandaaji mipango hii” alisema Waziri wa Ardhi Dkt Mabula.
Mkuu wa mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Salha Burian alisema mpago wa mtumizi ya ardhi unaondaliwa katika wilaya ya Nzega mkoani Tabora utatoa dira ya namna rasilimali za ardhi katika wilaya hiyo zitakavyotumika katika kuwaletea maendeleo wananchi na kukuza uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla.
‘’Sisi sote ni mashuhuda kuwa sasa Nzega inakwenda kufunguka upya kutokana na uwepo wa miradi ya kimkakati katika wilaya hii’’ alisema Dkt Batilda Burian.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Matumizi ya Ardhi Prof Wakuru Magigi alisema kazi ya uandaaji mpango wa matumizi ya ardhi katika wilaya ya Nzega ilianza Juni 1, 2022 kwa ushirikiano wa Tume yake na wataalamu wa halmashauri na viongozi wa wilaya.
Kwa mujibu wa Profesa Magigi, kazi iliyokwisha fanyika hadi sasa ni pamoja na kujenga uelewa na dhana nzima ya mpango wa matumizi ya ardhi, kuijengea uwezo timu ya upangaji matumizi ya ardhi ili kushiriki kikamilifu katika kazi hiyo, pia kufanya kazi ya ukusanyaji taarifa zote kutoka idara na taasisi zote sambamba na kuchakata taarifa zilizopatiakana.
Profesa Magigi alisema, baada ya kupata taarifa za msingi za matumizi ya sasa makadirio ya mahitaji mbalimbali ya kipindi cha miaka 20 yalifanyika
‘’Kwa kuzingatia makadirio ya matumizi mbalimbali Tume ya Matumizi ya Ardhi imewezesha kuandaa dhana ya muelekea wa ukuaji wa wilaya halmashauri kuwa kitovu cha kilimo na ufugaji sambama kuwa kitovu cha kilimo na uwekezaji na madini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇