LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 19, 2022

RAIS SAMIA AZITAKA WIZARA ZINAZOHUSIKA NA ELIMU TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUSHIRIKIANA ILI KUHAKIKISHA WATOTO WA JINSIA ZOTE WANATIMIZA NDOTO ZAO

CCM Blog Zanzibar
Rais Samia Suluhu Hassan, amezielekeza Wizara zinazohusika na elimu Tanzania Bara na Zanzibar  kuhakikisha zinashirikiana ili kuhakikisha watoto wakiume na wakike wote wanatimiza ndoto zao kwa faida ya Taifa zima.

Rais ametoa maelekezo hayo wakati akizindua Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) iliyopo Zanzibar inayojishughulisha na kumkwamua mtoto wa kike katika elimu ili kutimiza ndoto zake yenye kauli  mbiu inayosema “lea mwana tung’are”.

Kabla ya kuzindua taasisi hiyo katika Ukumbi wa wa Golden Tulip, Rais Samia ameupongeza uongozi wa MIF kwa mkakati kabambe wa taasisi hiyo wa kuleta chachu ya kuunganisha Serikali na MIF na taasisi nyingine katika kumkomboa mtoto wa kike kielimu huku akielekeza serikali inavyofanya maboresho izingatie masuala ya mitaala,ukaguzi wa elimu,utungaji wa mitihani na sifa za walimu.   

Ametoa mwito kwa wadau mbalimbali nchini kuunga mkono jitihada zinazofanywa na MIF huku akisisitiza kuwa suala la kuwakomboa Watoto wa kike ni suala la kila mtu. “Hilo ni jukumu letu sote, tunatakiwa wote tushirikiane.” akasema Rais Samia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Mfuko huo, Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar amemshukuru Rais kwa kuja kuzindua taasisi  hiyo  huku akielezea kuwa  kwa kuja kuzindua  amewapa heshima  kubwa wadau wote wa elimu nchini.

Amesema MIF inatambua kuwa kumekuwa na  changamoto katika jamii inayowazunguka  lakini wao wameamua kujikita katika elimu hususan  kubadili  mtazamo na fikra ya kuwa mtoto wa kike hana uwezo na badala yake ni kumkomboa ili hatimaye ayaishi malengo na ndoto za maisha yake huku akiiomba jamii iwaunge mkono.

Mwenyekiti huyo wa MIF amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza ambapo amewaomba kuendelea  kuchangia ili kuwasaidia watoto wa kike  waweze kutimiza ndoto zao.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa MIF, Fatma Mwasa ameyaelezea malengo makubwa ya taasisi hiyo  kuwa ni pamoja na kusaidia jamii huru iliyo na maendeleo isiyosumbuliwa na  ujinga, umasikini na maradhi kwa kumwinua mtoto wa kike kielimu, kuwawezesha vijana kiuchumi, kuongeza uelewa katika afya ya akili na kushughulika  na afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto.

Ameitaja baadhi ya mipango inayofanywa na MIF kuwa ni pamoja na kujenga kituo cha  cha kisasa cha mafunzo maalum kama vile ushonaji, umeme kinatakachogharimu takriban  bilioni 15 kwa ufadhili wa nchi za Falme za Kiarabu.

Pia kuendelea kuongeza mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na kuwachukua wanafunzi ambao hawajafanikiwa kwenye masomo na kuwa vhyuo  vya ufundi ambapo amesisitiza kuwa wamekuwa wakifanya vizuri.

Ameongeza kuwa MIF inafundisha kilimo cha mbogamboga  lengo ni kutaka kurudisha fedha  mapema, pia inajenga vyoo katika shule, kutoa ufadhili wa kusomesha  nje ya nchi wanafunzi wanaofaulu vizuri na kuwatafutia, masoko na mitaji.

Katika uzinduzi huo mawaziri anayesimamia elimu, Profesa Adolf Mkenda, anayesimamia Michezo Mohamed Mchengerwa na anayesimamia Utumishi, Jenista Mhagama wameungana na mawaziri kutoka  SMZ kushiriki uzinduzi huo.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) kwenye Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar, leo Juni 19, 2022. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa MIF, Fatma Mwasa na katikati ni Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Mfuko huo, Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages