LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 7, 2022

MKUU WA MAJESHI YA ULINZI TANZANIA JENERALI MABEYO KUSTAAFU MWEZI HUU WA JUNI 2022, AMUAGA RASMI RAIS DK. MWINYI

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo anatarajiwa kustaafu mwishoni mwa mwezi huu wa Juni 2022, kufuatia kumaliza muda wa Utumishi wake ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa mujibu wa sheria.

Jana Jenerali Mabeyo alienda Ikulu ya Zanzibar ambako alikutana na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi na kufanya naye mazungumzo na kumuaga kufuatia muda wake huo wa kumaliza Utumishi wake ndani ya JWTZ kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Taarifa iliyotolewa, imesema, katika mazungumzo hayo, Dk. Mwinyi amempongeza Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Mabeyo kwa kutekeleza vema majukumu yake katika kipindi chake chote cha utumishi ndani ya Jeshi hilo.

Taarifa imesema, Rais Dk. Mwinyi amemtakia kila la heri Jenerali Mabeyo katika maisha yake ya kustaafu hasa ikikumbukwa kwamba amelitumikia kwa muda mrefu Jeshi hilo na kufanya mambo mengi yatakayoacha alama.

Kwa upande wake Jenerali Mabeyo amesema Jeshi la Ulinzi Tanzania litaendelea kumkumbuka Rais Dk. Mwinyi kwa busara na hekima zake katika kuzishughulikia changamoto mbalimbali ndani ya Jeshi hilo ambalo hatimae limepata mafanikio makubwa.

Jenerali Mabeyo ni Mkuu wa Majeshi wa nane kuliongoza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu alipoteuliwa Februari 6, 2017 na Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli (ambaye sasa ni ameshafariki Dunia).

Alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania January 1, 1979 na kuhudhuria kozi ya Afisa Mwanafunzi na kupata Kamisheni mwaka 1980 kuwa Luteni Usu na baadaye alihudhuria kozi mbalimbali ndani na nje ya nchi zikiwemo Kenya, India, Canada na Marekani.

Katika kulitumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Jenerali Mabeyo, alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mwambata wa Jeshi nchini Rwanda, Msaidizi wa Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa Tawi la Usalama na Utambuzi na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ.

Jenerali Venance Mabeyo ametunukiwa medali mbalimbali zikiwemo za Miaka 20 ya JWTZ, Medali ya Utumishi mrefu, Medali ya miaka 40 ya JWTZ, Medali ya Utumishi uliotukuka, Medali ya Comoro na Anjouan,  Medali ya miaka 50 ya uhuru, Medali ya miaka 50 ya Muungano na ya Miaka 50 ya JWTZ.

Kuanzia Mwaka 1964 hadi 1974 Mkuu wa Majeshi alikuwa Jenerali Mirisho Sarakikya na kufuatiwa na Wakuu wengine sita nyuma ya Jenerali Mabeyo, kama ifuatavyo; 

Mwaka 1974 hadi 1980-Jenerali Abdalah Twalipo,
Mwaka 1980 hadi 1988-Jenerali David Musuguri, Mwaka 1988 hadi 1994-Jenerali Mwita Kiaro, Mwaka 1994 hadi 2001- Jenerali Robert Mboma, Mwaka 2001 hadi 2007- Jenerali George Waitara na Mwaka 2007 hadi 2017 - Jenerali Davis Mwamunyange.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akiagana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu, Zanzibar alipofika kwa ajili ya kumuaga, jana. (Picha na Ikulu)
 

© June 2022 CCM Blog/Bashir Nkoromo

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages