Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Angelina Akilimali jana alistukia akiahidi kutoa kitimwendo kwa ajli ya mtoto yeyote mwenye ulemavu wa miguu katika Mtaa wa Kivule Majole, Gongolamboto, baada ya kuguswa na hatua ya Mama Kada wa CCM mwenye ulemavu kutoa msaada wa viti vya aina hiyo kwa watoto wawili wenye ulemavu katika mtaa huo.
Hayo yalijiri wakati Mama huyo Kada wa CCM Marshal Mbise, alipokuwa akimkabidhi MNEC Angelina viti hivyo ili kuvitoa kwa Watoto wenye ulemavu Amina Abdallah (9) anayesoma darasa la tatu Shule ya Msingi Mji Mpya Gongolamboto, na Amada Ramadhan (13) ambaye hasomi, katika hafla iliyofanyika katika mtaa huo wa Kivule Majohe, Dar es Salaam.
"Dada Marshal jambo hili ulilofanya ni kubwa na la kupigiwa mfano, maana japokuwa wewe pia unahitaji kusaidiwa kwa kuwa ni mwenye ulemavu, lakini umewiwa hadi ukaamua kuwasaidia watoto hawa wenye ulemavu kama wewe, hili jambo limenigusa. Kama alivyosema Mheshimiwa Diwani kwamba Kata hii moja tu kuna watoto zaidi ya 40 wenye ulemavu, kwa hiyo na mimi nitajaliwa nichangie kitimwendo kimoja kwa ajili ya mtoto yeyetote mwenye uhitaji", akasema MNEC Angelina.
MNEC Angelina aliwaomba watu kuendelea kujitokeza kusaidia watu wenye ulemavu hasa watoto popote walipo kwa kuwa kufanya hivyo wanalisaidia Taifa na kumtendea Mungu, kwa kuwa hata aliyemzima ni mlemavu mtarajiwa ambaye Mungu atakapoamua kumfanya mlemavu naye atahitaji msaada.
Kwa upande wa siasa MNEC Angelina aliwataka wenye ulemavu kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za Uongozi ndani ya CCM na kuwakumbusha pia wananchi wote wa Kata hiyo ya Majohe kujiandaa na kushiriki katika kuandikishwa wakati wa Sensa itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu hapa nchini.
Kwa upende wake, Mwenyekiti wa Mtaa huo wa Kivule-Majohe, Ali Mzava alisema, baada ya kuambiwa na Kada wa CCM Marshal Mbise kwamba anahitaji kutoa viti kwa kwatoto wenye ulemavu aliweza kuwataarifu wazazi wa Amina Abdallah (9) anayesoma darasa la tatu Shule ya Msingi Mji Mpya Gongolamboto, na Amada Ramadhan (13).
"Licha ya kwamba hapa kwenye mtaa wetu tunao watoto wengi wenye ulemavu, ilinibidi niwalete hawa kwanza lakini siyo kwa upendeleo, maana walemavu wote tulionao wanahitaji kusaidiwa lakini misaada inayopatikana ni michache kuliko mahitaji", alisema Mwenyekiti huyo wa mtaa.
Naye Marshal akikabidhi viti hivyo kwa MNEC Angelina alisema, amefanya hivyo kwa sababu anajua dhiki wanayopata wenye ulemavu hasa watoto, ndiyo sababu akaamua kuwasaidia licha ya kuwa na uwezo wa kutosha kufanya hivyo.
Marshal aliiomba jamii na Serikali kuongeza juhudi za kusaidia wenye ulemavu kwa kuwa wanaishi maisha magumu, kwa kuwa watu wazima wenye ulemavu wengi wanao wanazo familia lakini wanashindwa kuyamudu maisha kiasi cha kufikia wakati mwingine kuonekana ni kero kwa wengine na kwa upande wa walemavu ambao ni watoto inashindikana kupata haki zao za msingi kama kusoma.
Katika hafla hiyo MNEC Angelina aliambana na Diwani wa Viti Maalum kwa tiketi ya CCM Semeni Mtoka na kuhudhuriwa na baadhi ya wakazi wa mtaa huo.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Angelina (Angel) Akilimali akimkalisha vema kwenye kitimwendo Mtoto mwenye ulemavu wa miguu Amina Abdallah (9) anayesoma darasa la tatu Shule ya Msingi Mji Mpya Gongolamboto, baada ya kumkabidhi kiti hicho kilichotolewa msaada na Mama mwenye ulemavu Marshal Mbise (Wapili kushoto) katika hafla ya kukabidhi viti viwili vya aina hiyo vilivyotolewa na Mama huyo, iliyofanyika Mtaa wa Kivule Majohe, Gongolamboto, Wilayani Ilala, Dar es Salaam, jana. Kushoto ni Diwani wa Viti Maalum (CCM) Semeni Mtoka, na anayesimama akishuhudia tukio hilo (kulia) ni Mwenyekiti wa Mtaa huo Ali Mzava. Kwa mujibu wa maelezo, Mtoto Amina alipata ulemavu wakati akipatiwa matibabu ya matege akiwa bado mchnga, kwamba baada ya kufungwa P.O.P mzunguko wa damu ulikwama kufika chini ya magoti miguu ikapooza na kuoza kisha mmoja kukatika na mwingine kukatwa katika Hospitali ya Bugando Mkoani Mwanza.Mjumne wa NEC ya CCM Angelina Akilimali alipokuwa akiwasili eneo la tukio akifuatana na Diwani wa Viti Maalum (CCM) Semeni Mtoka.MNEC Angelina Akilimali akisalimiana na Mama Marshal Mbise baada ya kuwasili eneo la tukio.Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule Majohe Ali Mzava (aliyesimama), akimkaribisha Diwani Mtoka (kulia) kumkaribisha mgeni rasmi MNEC Angelina Akilimali kuzungumza.MNEC Angelina Akilimali akizungumza baada ya kukaribishwa na Diwani Mtoka.MNEC Angelina Akilimali akifafanua jambo wakati akizungumza kwenye hafla hiyo.Mjumbe wa NEC ya CCM Angelina Akilimali akimshukuru Mama Marshal Mbise wakati Mama huyo akimkabidhi Vitimwendo kwa ajili ya kuwagawia watoto wawili wenye ulemavu wa miguu katika hafla hiyo. Katikati ni Mwenyekiti Mzava na Diwani Mtoka wakishuhudia tukio hilo.MNEC Angelina Akilimali na Diwani Mtoka wakimkalisha vema kwenye Kiti mwendo mtoto mwenye ulemavu Amina wakati akipewa kiti hicho na MNEC Akilimali.Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Angelina (Angel) Akilimali akimfunga vema mkanda mtoto Amina baada ya kumkabidhi kiti hicho.Mama Mbise akikabidhi kitimwendo kwa MNEC Akilimali kwa ajili ya mtoto mwingine aitwaye Amada.Mwenyekiti Mzava akimchukua mtoto Amada ili akabidhiwe kiti chake.Mtoto Amada akionyesha kufurahi wakati akikabidhiwa kiti chake na MNEC Akilimali.Mwenyekiti Mzava akizungumza baada ya watoto kukabidhiwa viti.Mtoto wa Mama Mbise, Zulfa Shaibu Mmma akitoa neno la shukrani mwishoni mwa hafla hiyo.Mama Mbise akitoa neno la Shukurani mwishoni wa hafla hiyo. Kushoto ni MNEC wa CCM Akilimali akimsikiliza kwa makini.Mharami Juma Pemba ambaye amepata ulemavu wa mguu kutokana na ajali ya gari mwaka juzi, naye akizungumza maneno ya kumshukuru MNEC kwa aujio wake na haja ya Serikali na jamii kuwasaidia wenye ulemavu. Bidhaa za kazi za mikono za Mama Mbise👇
"Hizi ni miongoni mwa bidhaa ambazo Mama yangu Mama Mbise huwa anatengeneza", akasema Zulfa wakati akimuonyesha MNEC Akilimali moja ya bidhaa ambazo hutengenezwa na Mama Mbise (kulia)."Ahaa, hili ndiyo taji la CCM, nzuri sana", akasema MNEC Akilimali huku akijaribu taji hilo kulivaa."Sasa hiki nacho ni kidani cha aina yake chenye rangi za CCM, nacho pia nimetengeneza mimi", akasema Mama Mbise wakati akimuonyesha MNEC Akilimali kidani hicho ambapo baadaye alimuunga mkono kwa kununua baadhi ya bidhaa kikiwemo kidani hicho."Acha namimi nipate picha ya kumbukumbu na huyu Kiongozi wetu", akasema Binti huyu mlemavu wa afya ya akili, wakati akipigwa picha na MNEC Akilimali. Hata hivyo Binti huyu bado anao uwezo wa kujieleza vizuri na inaonekana bado anajitambua."Haya Dada Zulfa chukua hii utakunywa soda na Mama yako, kwa heri tutakuja kuwatembelea siku nyingine", MNEC Akilimali akamwambia Zulfa ambaye alimsindikiza hadi kwenye gari lake alipokuwa akiondoka baada ya hafla kukamilika.©June 2022 CCM Blog/Bashir Nkoromo
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇