Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi , Profesa Adolf Mkenda(Mb) ameipongeza Benki ya NMB kwa kuwa mstari wa mbele kuinua Sekta ya Elimu nchini kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu wanaotoka kwenye familia zenye uhitaji.
Profesa Mkenda aliishukuru NMB wakati akiwakilisha Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa mwaka wa fedha 2022/2023. Aidha, alibainisha kuwa, Serikali inaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya kugharamia Elimu ya Juu nchini kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Juu, ili kuendana na mahitaji yanayotokana na ongezeko kubwa la uhitaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Benki ya NMB imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 200 kwa kuanzia katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kuanza kutoa mikopo ya elimu. Fedha hizo zitatolewa kwa utaratibu maalum wa kibenki na kwa mujibu wa makubaliano rasmi kati ya Wizara na NMB.
Mikopo hiyo itaongozwa na masharti yafuatayo:
· Itatolewa kwa riba nafuu.
· Itatolewa kuanzia ngazi ya stashahada (Diploma) na masomo ya Umahiri (Postgraduate).
· Itatolewa kwa waajiriwa wanaotaka kujiendeleza kielimu.
Katika hili, NMB itasaidia kupunguza idadi ya waajiriwa wanaowaombea watoto wao mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na hivyo kutoa fursa zaidi kwa waombaji wenye uhitaji.
Hivi karibuni, benki ya NMB ilizindua ‘Nuru Yangu Scholarship and Mentorship Program’ kwa ajili ya kusaidia elimu nchini, kwa lengo la kukata mnyororo wa umasikini na kuendeleza kizazi kijacho cha viongozi, kwa kutumia njia ya kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na sekondari (A-Level) na Elimu ya Juu.
Kupitia program hiyo, wanafunzi watalipiwa kila kitu ikiwemo ada, fedha za kujikimu, fedha za mafunzo kwa vitendo, bima ya Afya na Kompyuta mpakato. `
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Adolf Mkenda (Mb) akizungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna katika viwanja vya bunge jijini Dodoma, baada ya uwasilishaji wa Bajeti wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Adolf Mkenda (Mb) akizungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna katika viwanja vya bunge jijini Dodoma, baada ya uwasilishaji wa Bajeti wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇