LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 9, 2022

DC NVGUVILA: TUSIPANDISHE BEI ZA BIDHAA KIHOLELA KWA KISINGIZIO CHA KUPANDA BEI YA MAFUTA

Muleba, Kagera
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila amewataka wafanyabiashara wilayani hapa mkoani Kagera kuacha kupandisha bei za bidhaa zinazopatikana ndani ya wilaya hiyo kwa kisingizio cha kupanda bei ya mafuta na hivyo kuumiza wananchi.

Katika mkutano aliofanya jana viongozi mbalimbali na wafanyabiashara, wilayani hapa, sanjari na hilo, DC Nguvila amewasihi wafanyabiashara kuwajali wateja wao ili waweze kupata faida ambayo ni halali bila kuwaumiza kwa kuwauzia bidhaa kwa bei ya juu.

"Tukizingatia hayo tutakuwa na wateja wengi, mtafanya mzunguko wa biashara kuwa mkubwa na mtapata faida kubwa. Hata upendo kwenye jamii utakuwa mzuri mkiuza bidhaa zenu kwa wananchi kwa bei ambayo ni nzuri," ameeleza Mhe. Nguvila.

Aidha, amewashauri wafanyabiashara kuwa kadri wanavyoagiza mzigo mara kwa mara na kuuza kwa bei nafuu watakuwa kwenye nafasi ya kupata faida zaidi kuliko kuuza kwa bei kubwa na kusababisha bidhaa kukaa dukani muda mrefu bila kununuliwa.

Lakini pia ameagiza kufanyika kwa mkutano wa  Baraza la wafanyabiashara mara mbili kwa mwaka ili kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wafanyabiashara pamoja na wanufaika wa biashara ikiwa ni kukuza afya ya biashara na kutatua changamoto mbalimbali za wafanyabiashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Ndg. Elias Kayandabila amewasihi wafanyabiashara kuacha ubinafsi kwa kuwaeleza kuwa sio jambo jema kupandisha bei ya vitu vilivyomo kwenye maduka yao baada ya bei elekezi kutangazwa na Serikali.

Naye Katibu Tawala wa wilaya ya Muleba Ndg. Greyson Mwengu amewaomba wafanyabiashara kuweka bei ambazo haziwaumizi wananchi hasa kwa bidhaa zinazopatikana ndani ya wilaya kwa kuwaeleza kuwa wakiendelea kupandisha bei hasa za bidhaa za vyakula wanaweza kupelekea wananchi kushindwa kumudu gharama za bidhaa hizo na hatima yake bidhaa zao kutonunuliwa kabisa.

Afisa Biashara wa wilaya ya Muleba Ndugu Dickson Mnyaga amewaomba wafanyabiashara kupunguza bei, hasa kwa bidhaa kama mafuta ya kupikia, sabuni za kufulia bidhaa za ofisini kama karatasi nyeupe na vyakula kama nyama. Bidhaa hizi zishushwe bei na kuuzwa kwa bei stahili ambazo wananchi wanazimudu.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila akizungumza katika mkutano wake na viongozi mbalimbali na Wafanyabiashara wilayani humo, jana.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages