.
Na Dotto Mwaibale, Singida
BARAZA Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida limewatahadharisha Waislam kuwa muislam yeyote atakayefanya ubadhirifu wa mali za Waislam kuanzia sasa litachukua hatua kali dhidi yake.
Pia baraza hilo limetoa angalizo kwa wanasiasa kuacha mara moja kujiingiza kwenye masuala yoyote yanayohusiana na uendeshaji wa dini hiyo mkoani hapa na kuwa kwa wakati huu hawatapewa nafasi ya kufanya hivyo kama walivyozoea.
Kauli hiyo imetolewa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro wakati akitangaza mawaidha ya swala ya Eid -El-Fitr yaliyofanyika Msikiti wa Taqwa na Viwanja vya Ukombozi mkoani hapa.
"Nipo tayari nife lakini sitakubali kuona ubadhirifu wa mali za kiilam ukifanyika nasema sitakubali sitakubali sitakubali.. na sitakubali kuona wnasiasa wanaingilia masuala ya dini sisi tunafanya kazi zetu kwa kufuata katiba na si kuingiliwa na viongozi wa kisiasa" alisema Sheikh Nassoro.
Aidha katika hatua nyingine Nassoro amewataka Waislam kutojihusisha na vitina, majungu ya aina yoyote ile na migogoro ambayo inaweza kuhatarisha ustawi wa taasisi hiyo badala yake wayakatae mambo hayo ili kuijenga na kuifanya kuwa na mshikamano thabiti.
Aidha katika mawaidha hayo amewahamasisha waislam kujifunza elimu dunia na elimu ya dini ili kupata maarifa stahiki ambayo ndiyo msingi wa kuchagiza maendeleo ya muislam mmoja mmoja na ustawi wa dini ya kiislam kwa ujumla.
Akizungumzia zoezi la Sensa ya Watu na Mkazi litakaloanza hivi karibuni aliwataka Waislam kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo muhimu ambalo pia ni maiaaagizo ya Mtume Muhammad (S.A.W) ambaye katika kuleta muktaza muzuri kwa mafanikio na ushindi wa maendeleo ndani ya dini ya kiislam.
"Sensa ilifanyika tangu enzi za Mtume Muhammad (S.A.W) na sisi ni lazima tuifanye zote mbili ya kitaifa na yetu ya kiislam kwani inaleta maendeleo katika Taifa na ndani ya dini yetu ya kiislam tukijua idadi yetu tutaweza kupanga vizuri mambo yetu" alisema Nassoro.
Nassoro aliwataka makatibu wa Bakwata katika maeneo yote walipo kupita kila nyumba kuwahesa watu na kuwaomba wahusika kutoa ushirikiano kwa kuandika taarifa zao kwa usahihi bila ya kudanganya.
Hata hivyo Sheikh Nassoro amewasihi Waislam kuhakikisha wanaendeleza mema ambayo wameyapa wakati wa kipindi chote cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa ustawi wa roho na mwili lakini pia kuwa mfano wa kuigwa kwa yeyote anaoutizama uislam na Mtume Muhammad (S.AW.).
Katika hatua nyingine Sheikh Nassoro amewataka Waislam kutunza chakula ili kujikinga na njaa kutokana na mwaka huu kukosekana kwa chakula kuliko sababishwa na mvua kuwa chache,
"Ndugu zangu Waislam tutunzeni chakula na ninyi wafanyabiashara msiuze chakula kwa bei ya juu katika kipindi hiki ambacho kunauhaba" alisema Nassoro.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇