Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Eliezer Feleshi ( AG) amesema akiwa ni Wakili wa Serikali namba moja yupo tayari kwenda mahakamani kuendesha mashtaka ya jinai ikiwa itamlazimu kufanya hivyo.
AG Feleshi amebainisha hayo mwisho mwa wiki katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dodoma. Mgeni Rasmi katika Baraza hilo alikuwa ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dk. Damas Ndumbaro (Mb).
Utayari wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda mahakamani unatokana na matangazo ya Serikali (GN) namba 55, namba 56 na namba 97 yaliyotolewa kwa nyakati tofauti na Mkuruganzi wa Mashtaka Bw. Sylvestar Mwakitalu ambaye kupitia matangazo hayo amewateua na kuwatangaza mawakili wa serikali 168 akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa waendesha mashtaka ya jinai na watatekeleza jukumu hilo kwa maelekezo ya DPP.
”Mhe Waziri, mwanzoni mwa mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashtaka aliteua na kuwatangaza mawakili 168 na kuwapatia ’intrustment’ ya kuwa waendesha mashtaka ya jinai, na mimi kama wakili namba moja jina langu lipo, kwa hiyo nitakuwa tayari kwenda mahakamani kama mwendesha mashtaka kama nitahitajika na kwa maelekezo ya DPP.
Lakini pia nitumie nafasi hii kuwakumbusha mawakili wote wateule kwamba, instrument waliyopewa siyo kitambaa cha mfukoni, wanatakiwa kuifanyia kazi na nitataka kuona matokeo yake mwishoni mwa mwaka,” akasisitiza AG Feleshi.
Aidha AG Feleshi ambaye katika nafazi zake za uongozi amewahi pia kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo za Mkurugenzi wa Mashtaka na Jaji, amewasisitiza maafisa Masuuli wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria kuweka mipango mikakati ya kuwezesha mawakili wateule kuendesha mashauri hayo kwa maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
AG Feleshi amesema uamuzi huo wa kuwateua na kuwatangaza Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi hizo kuwa waendesha mashtaka, ni hatua ambazo zimechukuliwa pamoja na mambo mengine, zinalenga katika kuharakisha uendeshaji wa mashauri mahakamani, kuongeza tija Serikalini na pia kuongeza ujuzi, uwezo na uzoefu wa Mawakili waliopo katika Ofisi utumishi wa umma.
Aidha kufuatia uteuzi huo wa Mawakili wa Serikali 168 kuwa waendesha mashtaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema hatarajii kuona kuna mlundikano wa mashauri mahakamani au ucheleweshaji kwa kile alichosema, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeongezewa nguvu kazi.
AG Feleleshi ameongeza kwamba, kupitia maboresho yanayoendelea hivi sasa yakiwamo ya kuwasajili wanasheria na mawakili wa serikali walipo katika utumishi wa umma kupitia mfumo wa OAG-MIS, muda si mrefu utaratibu utawekwa kuhusu namna ya kuwatumia kikamilifu wanasheria wote walio katika ofisi za umma.
Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameelezea matarajio yake kwamba, Wakili Mkuu wa Serikali naye atatoa Hati kwa Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali itakayowezesha kuendesha Mashauri ya Madai Mahakamani.
Akifungua Baraza hilo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dk. Damas Ndumbaro ( Mb) pamoja na kuipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa na Baraza la Wafanyakazi lililo hai na linalofanya vikao vyake kwa mujibu wa sheria amewataka Watumishi wa Ofisi hiyo kutambua kwamba wao ni taswira ya Taifa kwenye masuala ya Utawala na Sheria na akatoa rai ya kuwataka kuendelea kutekeleza majukumu hayo kwa weledi na uadilifu wa kiwango cha juu na kwa mashalhi mapama ya Taifa.
Aidha Waziri Ndumbalo amesisitiza masuala kadhaa ambayo watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanapaswa kuyazingatia katika utekelezaji wa majukumu yao, Masuala hayo ni pamoja na kufahamu vipaumbele ya serikali na namna ya kuoanisha vipaumbele hivyo na mipango ya Ofisi , watumishi kuzingatia Sheria, Kanuni na miongozo ya Utumishi wa Umma ili kuongeza tija na ubora wa kazi na kuwa waadilifu.
Ajenda kuu iliyojadiliwa katika Baraza hilo ilikuwa ni kupokea na kujadili taarifa ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi, akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni Rasmi Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dk. Damas Ndumbalo (Mb) kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililofanyika mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇