LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 26, 2022

DC MWENDA AAGIZA IDARA YA AFYA IRAMBA KUFIKISHA CHANJOYA POLIO KATIKA TAASISI MBALIMBALI IKIWEO MAGEREZA

Na Hemedi Munga, Iramba

Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda ameiagiza Idara ya Afya kufikisha chanjo ya polio katika taasisi mbalimbali ikiwemo Magereza.

Mwenda ametoa agizo hilo leo Jumatatu Arili 25, 2022 wakati wa mafunzo ya chanjo ya polio kwa Kamati ya Msingi ngazi ya jamii yaliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo mjini hapa.

“Sasa nitoe maelekezo rasmi kuwa zoezi la chanjo lifike katika maeneo muhimu hasa katika kila tukio litakalokusanya watu, watu wa Idara ya afya mfike kutoa elimu ili watu wapate chanjo.” aliagiza na kuongeza kuwa

 “Ninatoa maagizo maalumu kwa Idara ya afya kutembelea Magereza kukagua kama kuna watoto na kuhakikisha watoto hao wanapata huduma muhimu za afya ikiwemo chanjo ya polio.”

Halikadhalika, Mkuu huyo wa wilaya aliitaka kamati hiyo kuifikia jamii ili kuipa elimu na kuisisitiza kuendelea kuchukua tahadhari ya maambukizi dhidi ya virusi vya UKWIMI hasa katika maeneo ya barabara kuu itokayo Singida kuelekea jijini Mwanza, Migodini na Ziwa Kitangiri.

“Ndugu zangu ni wajibu wetu sisi tuchukue tahadhari, pia tutoe elimu kwa jamii inayotuzunguka.” Alisistiza

Aidha, aliongeza kuwa upo ugonjwa wa Homa ya Inni ambao unaonekana kuwa hatari sana katika afya ya mwanadamu, hivyo ni vyema wananchi na watumishi wakachukua tahadhari na kuchanja.

“Nitoe wito kwa watumishi wote na kuwahamasisha wananchi kuchoma chanjo ya Homa ya Inni ambayo hushambulia zaidi Inni, habari njema nikwamba chanjo hiyo ipo.”

Akiongelea kuhusu ugonjwa wa malaria, Mkuu huyo wa wilaya aliendelea kuitaka kamati hiyo kuchukua tahadhari na kuielimisha jamii kujikinga na ugonjwa wa malaria.

“Tunatamani na ndio lengo letu ifike wakati wilaya ya Iramba na nchi kwa ujumla tunakuwa na zero malaria, hivyo tuendelee kuwahamasisha wananchi wafukie madimbwi, kutumia neti na kusafisha kila penye mazalia ya mbu.”

Pia, aliitaka kamati hiyo kuendelea kuhamasisha watu kujitolea katika zoezi la kuchangia damu ili kukidhi haja ya hitajio la damu pale inapotokea wagonjwa wanahitaji damu.

Katika kuhakikisha elimu ya chanjo inawafikia watu wengi katika jamii, Mkuu huyo wa wilaya aliitaka kamati kuongeza wigo wa kushirikisha viongozi kuanzia ngazi ya kijiji.

Hatua hiyo itasaidia jamii kupata elimu sahihi ya chanjo na kuepukana na upotoshaji na tamaduni za kuwafunga watoto mvuje na hirizi wakidaiwa kuamini kuwa ni kinga kuliko chanjo hizi za kitaalamu.

“Ndugu zangu tukifanikiwa kushirikisha viongozi kuanzia ngazi ya kijiji elimu itafika kwa jamii na tutafanikiwa kupunguza vifo vya watoto.”

Akiongea katika kikao hicho Mkuu wa Idara ya Afya, Dkt Hussein Sepoko alisema kuwa kampeni ya chanjo ya polio itaanza Aprili 28, 2022, hivyo aliwaomba wanakamti hao kuwa mabalozi wa kufikisha elimu sahihi ya chanjo.

“Ndugu viongozi! Niwaombe tufahamu kuwa chanjo hii ya polio lengo lake ni kuwaongezea kinga watoto na si vinginevyo.”

Kwa upande wake mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo Mkuu wa Gereza la Kiomboi Iramba, Denis Njegite aliiomba Idara ya Afya kutoa nakala ya mafunzo hayo ili kuwawezesha wao kufikisha ujumbe huo katika tasisi wanazoziongoza.

Naye katibu tawala wa wilaya hiyo, Pius Songoma alishauri timu hiyo kuelekeza nguvu katika maeneo ya machimboni, wafugaji na ziwani ili kufikisha chanjo hiyo kwa lengo lakutimiza zoezi la kitaifa.

Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda akizungumza wakati wa mafunzo ya chanjo ya polio kwa Kamati ya Msingi ngazi ya jamii, yaliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo mjini Ikungi, leo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages