LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 19, 2022

KILELE CHA WIKI YA MAJI KURINDIMA JUMANNE IJAYO, MLIMANI CITY JIJINI DAR ES SALAAM CHINI YA RAIS SAMIA

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya Kilele cha Wiki ya Maji mwaka huu, itakayofanyika Jumanne ijayo, Machi 22, katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Bila Shaka Rais Samia atakuwa na mazuri na makubwa ya kuzngumza kwenye killele hicho, akivinjari mikakati iliyopo na iliyokwisha fanywa na Serikali ya awamu ya Sita, hasa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ambacho ametimiza leo Machi 19, 2022 tangu ashike hatamu ya Urais wa Tanzania.

Matarajio ni kwamba Rais Samia atalizungumzia kwa undani kwa kuwa mbali ya kwamba maji ni muhimu kwa matumizi ya binadamu kwa ajili ya kunywa, kupikia na kuoga, lakini Maji ni kichocheo muhimu cha maendeleo katika sekta mbalimbali za uchumi katika nchi yoyote ikiwemo Kilimo, Biashara, Utalii na Viwanda na pia ni muhimu kwa binadamu

Wakati Watanzania wanasubiri kwa hamu kumsikia Rais Samia, tuangazie japo kidogo Chimbuko la kuwepo Maadhimisho ya Wiki ya maji na imeamuliwa iwepo kwa manufaa gani katika sekta ya maji.

Kwa kutambua umuhimu na thamani ya maji katika maisha ya binadamu na uchumi wa Dunia kwa ujumla, Mwaka 1993 Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira na Maendeleo lilipitisha Azimio rasmi la kuadhimisha Siku ya Maji Duniani kila mwaka ifikapo tarehe 22 Machi.

Lengo la Umoja wa Mataifa kupitisha Azimio hilo, kubwa lilikuwa na bado ni kutumia Maadhimisho ya Wiki ya Maji kama fursa maalum ya Sekta za Maji katika Nchi mbali mbali kujitathimini kwa kujilinganisha na nchi nyingine Duniani katika kutazama hatua iliyofikiwa katika utoaji wa huduma hiyo muhimu ya maji na namna ya kukabiliana na changamoto zinazokuwa zinaikabili sekta ya maji.

Katika mwitikio wa Azimio hilo, Tanzania kupitia Wizara ya Maji imekua ikiratibu na kuadhimisha Wiki ya Maji au siku hiyo muhimu kuanzia mwaka 1988 kwa kuwashirikisha wananchi na wadau wa Maji katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na huduma ya maji ikiwemo kutoa maoni ya namna bora ya kuboresha huduma za maji na namna ya kuzikabili na kzitatua changamoto zinazokuwa zimejitokeza katika sekta hiyo.

Maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika hapa Nchini ikiwa ni mwitikio wa Azimio Na. 47/193 la Umoja huo wa Mataifa (UN) linalozitaka nchi wanachama kuadhimisha Siku ya Maji Duniani kila Machi 22 ya kila mwaka siku ambayo kwa Tanzania inakuwa ni kilele cha Wiki hiyo ya Maji.

Bila shaka lengo kuu la maadhimisho haya hapa nchini ni kuungana na Mataifa mengine Duniani
katika kutathmini utekelezaji, mafanikio, changamoto na kuainisha mikakati ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira na kusimamia utunzaji wa rasilimali za maji nchini.

Maadhimisho ya mwaka huu yamepewa kaulimbiu inayosema: Maji chini ya Ardhi; Hazina isiyoonekana kwa Maendeleo Maendeleo.

Bila shaka miongoni mwa madhumuni ya siku hii ni kama ifuatavyo; kuelimisha Jamii kuhusu Seraya Maji na Majukumu yao katika kuitekeleza, Kutathmini Maendeleo ya Utekelezaji wa Programu ya Maji, hali ya huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini na kuweka Mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Maeneo mengine yanayotiliwa mkazo ni; kuwaleta pamoja wataalam wa sekta ya maji katika majadiliano, kujifunza na kubadilishana uzoefu; Kuhamasisha ubunifu wa kisayansi katika utafiti na teknolojia katika utoaji wa huduma na utunzaji wa vyanzo vya maji, kutathimini mafanikio ya sekta maji kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP).

 

Aidha ni Kuwakutanisha wadau mbalimbali (taasisi binafsi, wadau wa maendeleo na Serikali) katika kubaini fursa za uwekezaji kupitia sekta ya maji, na kutathmini mchango wa sekta ya Maji katika tasnia nzima ya maendeleo ya Viwanda nchini.

Katika kuadhimisha wiki ya maji Wizara ya Maji inasema, inashirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya maji katika kutathmini utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira pamoja na uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji. Wiki hii inaenda sambamba na shughuli mbalimbali zinazohusiana na utoaji wa huduma ya maji na utunzaji wa vyanzo vya maji nchini.


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages