LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 28, 2022

CHUO KIKUU MZUMBE: PROF. NGOWI ALIKUWA MHIMILI MUHIMU WA CHUO

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Chuo Kikuu cha Mzumbe kimesema Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Ndaki ya Dar es Salaam Prof. Prosper Ngowi ambaye amefariki dunia pamoja na dereva Innocent Mringo, kwa ajali ya gari alikuwa mhimili muhimu katika Menejimenti ya Chuo hicho.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chuo Kikuu Mzumbe Rose Joseph, imemkariri Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Lughano Kusiluka akisema Prof. Ngowi alikuwa muhimili wa Chuo hicho hususani katika usimamizi wa shughuli za kitaaluma Ndaki ya Dar es Salaam, mbunifu, na msimamizi mahiri wa miradi ya maendeleo, utafiti, machapisho na elimu kwa Umma.

"Baraza, Menejimenti, Wafanyakazi na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu Mzumbe, tunatoa pole kwa Familia ya Marehemu Prof. Prosper Honest Ngowi, na Innocent Gerson Mringi, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote waliogushwa na msiba huu mzito, Daima tutawakumbuka na kuuenzi mchango wao mkubwa kwa kipindi chote cha utumishi wao katika kuendeleza Chuo Kikuu Mzumbe", imesema taarifa hiyo.

Taaarifa imethibitisha kuwa Profesa Ngowi na Dereva Mringo wamepatwa na ajali hiyo katika eneo la Mlandizi katika mkoa wa Pwani, wakiwa njiani wakitokea dar es Salaam, kwenda Kampasi Kuu ya Chuo hicho, Morogoro kwa ajili ya shughuli za kikazi.

"Mipango ya mazishi inaendelea kwa kushirikiana na familia za marehemu, na mara taratibu zitakapokamilika, Umma utajulishwa", imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema, Prof. Ngowi aliajiriwa na Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 1994 kuwa Mkufunzi Msaidizi, baada ya kuhitimu Stashahada ya Juu ya Mipango ya
Uchumi.

Baadae alijiendeleza na kupata Shahada ya Kwanza, Shahada ya Umahiri katika Biashara na Uchumi, na baadae mwaka 2014 alihitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uchumi.

Mwaka 2015 alipandishwa cheo na kuwa Profesa Mshiriki, na kuongoza Idara mbalimbali za Chuo Kikuu Mzumbe kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Ndaki ya Dar es Salaam hadi umauti ulipomkuta, leo.

Mbali na kushika nafasi za uongozi Prof. Ngowi amekuwa Mjumbe wa Bodi mbalimbali za Taasisi za Umma na Binafsi, Bodi za Kitaaluma, Mshauri na mchambuzi wa masuala ya kiuchumi na biashara, Mtafiti, Mshauri na Mwandishi wa Makala mbalimbali za uchumi, na mtoa mada katika makongamano ya kitaifa
na kimataifa.

Kwa upande wa Dereva Innocent Gerson Mringo, taarifa imesema,  aliajiriwa na Chuo Kikuu Mzumbe kuwa Dereva Daraja la Pili mwaka 2017 hadi umauti ulipomkuta leo.

Alipata mafunzo yake ya udereva na kuhitimu Chuo cha Taifa cha Usaririshaji mwaka 2016, na VETA
mwaka 2017.

Mwandishi wa Blog ya Taifa ya CCM (CCMBlog) Mwamvua Mwinyi, ameripoti kutoka mkoa wa Pwani akimkaririri Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Pius Lutumo kwamba gari aina ya Scania lenye namba T608 AGV  likiwa na tela lenye namba T317 AQM likiendeshwa na Raymond Kimaro (36) mkazi wa Ubungo lililokuwa limetokea Congo DRC kwenda Dar es Salaam, lilihama upande wake wa barabara na kugonga gari aina ya Noah lenye namba T256 CMF lililokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Morogoro.

Alieleza, hali hiyo ilisababisha Kontena kuchomoka na kuangukia gari SU 38223 aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa ikitokea Dar es salaam kwenda Morogoro ikiendeshwa na Innocent Gerson Mringo (33) na kusababisha vifo na majeruhi hao ambapo Dereva Mringo na Profesa Prosper Ngowi (55) walifariki Dunia.

Kamanda huyo wa Polisi amesema waliojeruhiwa ni Raymond Kimaro (39) na Abdallah Mohammed (33) Dereva wa Noah mkazi wa Dar es Salaam.

Kamanda huyo alifafanua, chanzo Cha ajali bado kinachunguzwa hata hivyo uchunguzi wa awali unaonyesha Kuwa ni uzembe wa dereva wa gari aina ya scania kuhama upande wake wa barabara na kugonga gari aina ya Noah na kupelekea kontena kuchomoka na kuliangukia gari Toyota Cruiser.

Prof. Prosper Ngowi, enzi za uhai wake.
Innocent Gerson Mringo

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages