Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumbaro, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 3,2022 jijini Dodoma kuhusu Mpango huo wa miaka 10 wa maadhimisho ya Mwalimu Nyerere unaokwenda kwa jina la ‘Mwalimu Nyerere @100’ .
……………………………………………….
Na.Alex Sonna,DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau imezindua mpango wa miaka 10 wa kuenzi na kusherehekea urithi wa maisha ya Baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere.
Mpango huo unalenga kuwashirikisha wadau ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere kitaifa na kimataifa.
Hayo yamesemwa leo Februari 3,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumbaro, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mpango huo wa miaka 10 wa maadhimisho ya Mwalimu Nyerere unaokwenda kwa jina la ‘Mwalimu Nyerere @100’ .
Amesema kuwa umuhimu wa kuandaa, kutangaza, kumuenzi, kukusanya,kuendeleza, kuhifadhi na kutangaza rasilimali za urithi wa Mwalimu Nyerere kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho ili kukuza na kuendeleza utalii.
“Maadhimisho ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere (Mwl.Nyerere @100) kama sehemu ya kutekeleza mpango wa miaka 10 wa kuenzi na kusherehekea urithi wa maisha ya mwalimu Nyerere yanatarajiwa kufika kilele tarehe 13 Aprili 2022, Butiama mkoani Mara tarehe ambayo ndiyo kama angekuwa hai angetimiza miaka 100”alisema Dk. Ndumbaro
Hata hivyo Dkt.Ndumbaro amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuenzi na kusherehekea mchango maridhwa wa Mwalimu Nyerere katika Nyanja mbalimbali kitaifa na kimataifa.
“Mwalimu Nyerere alikuwa maarufu sana nchi za nje kuliko hata hapa kwetu hivyo kupitia mambo aliyofanya tutakwenda hadi nje ya mipaka yetu kuyatangaza ili vizazi vya nje kuyajua mambo kama ukombozi wa mataifa ya Afrika”amesema Dk. Ndumbaro
Kwa upande wake Katibu mkuu Wizara hiyo Dk. Francis Michael, amesema kuwa Mpango huo umeanisha kazi ambazo zitatekelezwa na taasisi mbalimbali ambapo wizara yake ndiyo itaratibu shughuli zote.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇