Na Mwandishi Maalum, Katavi
Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Mageuzi ya Kijani Afrika(AGRA) Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, ameishauri Serikali kuimarisha Vyama vya Ushirika ili viwe suluhisho ya upatikanaji wa masoko ya mazao ya wakulima.
Kikwete ameyasema hayo kwa nyakati tofauti jana, Februari 17, 2022 Wilaya za Mpanda na Tanganyika mkoani Katavi akiwa na Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, katika ziara ya kikazi ya kutembelea wanufaika mbalimbali wa miradi inayotekelezwa chini ya ufadhili wa AGRA.
"Hapo nyuma wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, tuliamua kubeba madeni yote ya vyama vya ushirika ili kuweza kuviimarisha na kuviongeza nguvu ya kukopa na kuhudumia wakulima.
Miaka ya nyuma Serikali ilibaini kuwa viongozi wengi wa vyama vya ushirika walikuwa si waaminifu, hali iliyopelekea kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha za wakulima na mali za ushirika.
Kimsingi, Serikali iliamua kuimarisha ushirika ili utumike kama nyenzo kuu ya kutafuta masoko ya mazao ya wakulima na kuwasaidia kupata pembejeo sahihi kwa wakati na kwa bei nafuu, hivyo, Mavunde, kama Serikali jaribuni kuimarisha ushirika ili uweze kusaidia kutafuta masoko ya mazao ya wakulima" alisema Kikwete.
Naye Naibu Waziri Mavunde, alieleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha Ushirika ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa tujenge ushirika imara, wenye nguvu na utakaomnufaisha mkulima na serikali kupitia Mrajisi wa Ushirika.
Mavunde alisema na katika kuhakikisha Ushirika unakuwa imara na wenye manufaa Serikali itaendelea kuwachukualia hatua kwa mujibu wa sheria viongozi wote wa Ushirika watakaoshindwa kusimamia ushirika kwa mujibu wa sheria na kwa wale pia watakaobainika kufanya ubadhirifu.
Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Mageuzi ya Kijani Afrika(AGRA) Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete akishauriana jambo na Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mvunde.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇