Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akiangalia madini ya Tanzanite kwenye kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary (T) LTD inayomilikiwa na Faisal Juma Shabhai (kulia) alipotembelea Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameagiza zawadi aliyopewa mke wake Mama Mary Majaliwa na Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary (T) LTD ya kidani cha Tanzanite iuzwe ili fedha zitumike kwa ajili ya kujenga bweni la wanafunzi wa Wilaya ya Simanjiro.
Waziri Mkuu Majaliwa akizungumza mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro alipohitimisha ziara yake ya siku ya siku nne kwenye Mkoa wa Manyara ameshukuru kwa zawadi hiyo ila akaagiza iuzwe kisha fedha zitakazopatikana zitumike kujenga bweni moja kwenye shule iliyopo Simanjiro.
Amesema anashukuru amepatiwa zawadi hizo kutoka kwenye mkoa huo na kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary LTD ila itumike kwa ajili ya kujengwa bweni la kulala wanafunzi.
“Nawashukuru kwa zawadi japokuwa mama Majaliwa hajaiona ila hatachukia hivyo iuzwe ili ijengwe bweni la kuwasaidia wanafunzi kwenye Wilaya ya Simanjiro,” amesema.
Hata hivyo, amezipongeza kampuni zilizoitikia wito wa Serikali wa kufungua ofisi na kuhamishia biashara ya madini ya Tanzanite kwenye mji mdogo wa Mirerani ikiwemo kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary LTD.
“Nimetembea ofisi ya Tanzanite Forever Lapidary na nikashuhudia wanaofanya usanifu wa madini ni wanawake na mwanaume mmoja na nikamuuliza mmiliki akasema wamama ndiyo wanaweza kutengeneza vizuri,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, alimshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kuhitimisha ziara yake kwenye mkoa huo na kueleza kuwa wameandaa zawadi.
Makongoro amesema wamempa zawadi Waziri Mkuu na zawadi nyingine ya kidani cha madini ya Tanzanite wameitoa kwa ajili ya mke wake Mama Mary Majaliwa ambayo imeagizwa iuzwe kwa ajili ya kujenga bweni.
Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary Ltd Faisal Juma Shabhai, akizungumza baada ya Waziri Mkuu Majaliwa kutembelea soko la madini ameishukuru Serikali kwa kuona na kutambua umuhimu wa biashara ya madini ifanyike Mirerani.
Faisal amesema zao la Tanzanite linawanufaisha watu tofauti baada ya Mungu kuyaweka madini hayo kwenye eneo hilo na kunufaisha watu wengi kwani Tanzanite ni zao la Taifa.
“Nawaomba wafanyabiashara wenzangu wa madini ya Tanzanite tufuate masharti yaliyowekwa na Serikali ili biashara hii iweze kunufaisha watu wote na Taifa kwa ujumla na siyo mtu mmoja mmoja,” amesema Faisal.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇