NA
K-VIS BLOG, MOROGORO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista
Mhagama amezindua Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii,
(NSSF) kwenye hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa NSSF Mafao House mjini
Morogoro Januari 8, 2022.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo
ni Balozi Ali Idi Siwa ambaye aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo kwa kipindi kingine cha
miaka mitatu.
Akizungumza na Wajumbe
wa Bodi hiyo, Mhe. Waziri aliwapongeza kwa kuaminiwa na kuwataka wawe
wasimamizi wazuri wa Mfuko kwa kushirikiana na Uongozi.
“Nichukue
nafasi hii kuwapongeza Wajumbe walioteuliwa lakini nimpongeze sana mwenyekiti
wa bodi ambaye amerudi tena kuongoza bodi hii kwa kipindi kingine cha awamu ya
pili cha miaka mitatu.” Alipongeza na kuongeza………..:Wenzangu Mfuko huu si mdogo
hesabu za Disemba 2021 thamani imepanda hadi Trilioni
5.4 wakati huo bodi iliyokuwa ikiongoza
Mfuko ilikuwa chini ya Mhe. Balozi Siwa, hapa ndio tunaona ni kwa sababu gani
Mhe. Rais ameona amrudishe kuendelea Kuongoza tena Bodi ya NSSF
Alisema matazamio ya
Serikali ni kwamba yale yaliyofanyiwa kazi
vizuri kwenye Bodi iliyopita, chini ya
Bodi hii mpya wanapaswa kuongeza nguvu mara mbili na zaidi ili kwenda mbali
zaidi ya hapo Mfuko ulipo na hilo linawezekana.
Aliwakumbusha majukumu
ya Bodi kuwa ni kuangalia ustawi na uendelevu wa Mfuko, ambapo moja ya majukumu
hayo ambayo yapo kisheria ni pamoja na kuandikisha Wanachama ili kupanua wigo
wa uchangiaji ambao thamani ya Mfuko inaongezeka pia.” Alifafanua Waziri
Mhagama.
Aidha Mhe. Waziri
Mhagama alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba ambaye katika
kipindi kifupi tangu ateuliwe kuongoza Mfuko huo, amehakikisha kuwaweka
wafanyakazi wote kuwa kitu kimoja, timu moja.
“Mahali
popote ambapo wafanyakazi ni wamoja tija itapatikana, tumeshuhudia kasi ya
kukua kwa Mfuko, lakini utatuzi wa changamoto mbalimbali za Mfuko ambazo ni
shirikishi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wanaongea lugha moja na sasa Bodi
imeingia, wote tutakuwa kitu kimoja.” Alifafanua.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti huyo mpya wa Bodi, Balozi Ali Idi Siwa alimshukuru Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na
kumteua kwa kipindi kingine cha pili cha miaka mitatu.
“Uteuzi
huu na imani hii ni changamoto kubwa kwangu na chachu kubwa ya kunifanya niweze
kurudisha imani kwake kwa kufanya kazi kwa nguvu zaidi na ufanisi zaidi.”
Alisema.
Pia alimpongeza Mhe.
Waziri kwa uteuzi alioufanya wa wajumbe wa Bodi kwa kuzingatia mahitaji ya taaluma
na hana shaka kuwa Bodi imesheheni taaluma zinazohitajika.
Alisema kwa sasa kazi
ya Bodi ni moja tu, kutimiza yale ambayo wanapaswa kuyatimiza ikiwa ni
pamoja na usimamizi na kutoa mwelekeo.
“Sisi kazi hii tunayokwenda
kufanya inapimika, na tuache watu wa aina tatu watupime ambao ni wale
wanaotusimamia ambao ni Wizara, Menejimenti inapofanya tathmini zake za kazi na
Wanachama wa Mfuko.” Alibainisha.
Awali Mkurugenzi Mkuu
wa NSSF, Bw. Masha Mshomba alimshukuru Mhe. Waziri kwa kuzindua Bodi hiyo ambayo
alisema imesheheni uzoefu wa kutosha.
”Ninahakika
kwa sasa tutakwenda mbele tukijivunia kwa uhakika yale malengo tuliyojiwekea kwenye
mikakati yetu ya maendeleo ambayo inaishia 2025 tutayatimiza, sambamba na yale ambayo
sisi kama Taasisi tunayopaswa kuyatimiza ambayo yapo kwenye mpango wa taifa wa
miaka Mitano unaoishia 2025, ikiwa ni pamoja na maelekezo ambayo Mhe. Rais
aliyatoa Bungeni akielezea dira yake ya yale atakayoyafanya katika uongozi
wake.” Alisema.
“NSSF
inakwenda vizuri, na kama ambavyo unajua tuna wanachama kutoka sekta binafsi ambao
kisheria inatupasa kuwa cover wote, lakini pia sheria iliyofanyiwa marejeo 2018
ilitupa mamlaka ya kuwa cover pia Sekta isiyo rasmi na katika hii napenda
kukuhakikishia kwamba Mfuko unafanya kazi kubwa ili kuhakikisha kwamba
matarajio yaku cover Sekta yote isiyo rasmi tunayafikia.” Alitoa hakikisho Bw.
Mshomba.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa. Jamal Katundu, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martin Shigela na Menejimenti ya Mfuko wa NSSF.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇