Na Bashir Nkoromo, Mlimani Chity
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amewakingia kifua Walimu Wakuu, kwa kupiga marufuku tabia ya Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuwashusha vyeo walimu hao, shule zao zinapofanya vivaya katika matokeo ya mitihani.
Ummy alisema inashangaza kuona kuwa Wakurugenzi wamekuwa wakikimbilia kuwashusha vyeo Walimu Wakuu kila shule inapofanya vibaya, bila kutazama sababu zingine, kwa kuwa wakati mwingine shule inakuwa imefanya vibaya kwa kuwa huyo Mwalimu hakuwezeshwa vya kutosha kufanya shule ipate matokeo mazuri.
Hayo aliyasema na kupiga marufuku hiyo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 16 wa Wakuu wa Shule za Sekondari nchini jana katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, chini ya Umoja wa Walimu Wakuu Shule za Sekondari (TAHOSSA).
“Sasa Mkurugenzi kila ukiona shule katika Halmashauri yako imefanya vibaya unakimbilia kumshusha cheo Mkuu wa Shule, hata hushughuliki kutaza sababu zingine, inawezekana huyo mwalimu hujamuwezesha, sasa unadhani kama hakuwezeshwa atawezaje kuifanya shule ipate matokeo mazuri?
Walimu mmekuwa msaada mkubwa sana kwa maendeleo ya elimu katika nchi yetu, lakini hii tabia ya kuwaonea kwa kuwashusha vyeo imeshamiri sana na siikubali. Sasa kuanzia leo sitaki kusikia tabia hii, nitawalinda Walimu wangu dhidi ya unyanyaswaji na mtu yeyote,” alisema Waziri Ummy
Kuhusu kupewa kipaumbele ufundishaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Waziri Ummy alisema shule zote mpya zinazojengwa na Serikali ya Awamu ya Sita iliyopo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, zitakuwa na mabara na vifaa vyote vinavyohitajika kufundishia TEHAMA.
Alisema katika mpango wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2022-2025 Serikali inapanga kuanza na shule 1,500 kuwekwa maabara ya kompyuta zenye vifaa vyote muhimu vya TEHAMA ambapo katika mpango huo Serikali imepanga kuweka Kompyuta 50 kila shule zikiwa na vifaa vyote vya Tehama na kuwa mpango wa muda mrefu ni kuhakikisha shule zote za serikali zitakuwa na maabara za kompyuta.
Kuhusu Michango, Waziri Ummy alipiga marufuku michango holela shuleni ambayo alisema imekuwa kero kwa Wazazi na kuonya kuwa ambao hawatasikia agizo hilo watachukuliwa hatua kali ili kuwa mfano kwa wengine.
“Magufuli (aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano Dk. John Magufuli), alipiga marufuku michango kama hii na Rais Samia ameendeleza elimu bure na Serikali yake imekataza michango lakini haiishi, mzazi anadaiwa hadi sh. 200,000 kuingiza mtoto kidato cha kwanza, atazipata wapi, wengi hawana uwezo wa kulipa hizo.
Mwalimu unataka mtoto aanze shule na trucksuit pea mbili, viatu pea mbili, na sare pea mbili, halafu kama mzazi hana vitu hivyo unazuia mtoto asiingie shule, hapana. kama mtoto hana pea mbili anayo moja mpokee tu, nyingine itanunuliwa baadaye, nasema waacheni wanafunzi wajiunge na shule hata kama hawana sare kwani bila sare mtoto hafundishiki?,” alihoji Waziri Ummy.
“Katibu Mkuu tutoe mwongozo michango ya lazima ni ipi ili iwe wazi mtoto akianza kidato cha kwanza awe nanini maana bila hii miongozo wengine wataendeleza hii tabia tumesema sana lakini naona kuna watu hawasikii,” alisema Waziri Ummy.
Kuhusu unyanyasaji wanafunzi hasa wa kike, Waziri Ummy alisema walimu wanapaswa kuwa walezi na washauri bora wa wanafunzi hivyo wasiwe sehemu ya kundi ovu linaloharibu wanafunzi na Vile vile, na kuonya kuwa hatamvumilia Mwalimu yeyote atakeyebainika kumdhalilisha mwanafunzi na kwamba mwalimu huyo atafukuzwa kazi na hatarudishwa.
Akizungumzia kuhusu masomo ya ziada, Ummy alisema Serikali inachokataza ni masomo ya ziada ya lazima ambayo wanafunzi wamekuwa wakilazimishwa kulipia wakati wa likizo.
“Kama unataka kufanya masomo ya ziada wakati wa likizo fuata utaratibu kwa sababu kanuni na miongozo kuhusu hilo ipo ifuate kwa kuomba kibali sehemu husika badala ya kila mmoja kufanya holela holela na mwanafunzi apewe muda wa kutosha wa kupumzika,” alisema.
Mkutano huo Mkuu wa 16, ambao utamalizika kesho, umehudhuriwa na Walimu zaidi ya 500 na utatumika kujadili masuala mbalimbali ikiwemo changamoto zinazohusu sekta ya elimu na mafanikio katika sekta hiyo ikiwemo uboreshwaji wa miundombinu ya kufundishia kama ujenzi wa shule mpya na vyumba vya madarasa unaoendelea nchini kote.
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu akifungua Mkutano Mkuu wa 16 wa Wakuu wa Shule za Sekondari nchini jana katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, chini ya Umoja wa Walimu Wakuu Shule za Sekondari (TAHOSSA).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇