LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 17, 2021

WAZIRI SIMBACHAWENE:TIMIZENI WAJIBU WENU KWA KUZINGATIA SHERIA KULINDA USALAMA WA WATU NA MALI ZAO+video

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akihutubia wakati wa ufunguzi wa Baraza Kuu la  Wafanyakazi wa wizara hiyo jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi na Katibu Mkuu - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ndugu, Christopher D. Kadio

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi - Mhe. Khamis H. Khamis – Chilo (Mb.)








 HOTUBA YA MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE (MB.) WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI KATIKA UFUNGUZI WA BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI, DODOMA TAREHE 17 DESEMBA, 2021

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi - Mhe. Khamis H. Khamis – Chilo (Mb.),Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi na Katibu Mkuu - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ndugu, Christopher D. Kadio,Katibu wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Ndugu, Dorothy Mayala, Wakuu wa Vyombo vya Usalama mliopo [IGP, CGI, CGP na CGF),Makamishna wa Vyombo mliopo,Wakuu wa Idara na Vitengo,Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE),Viongozi wa TUGHE Taifa na Mkoa, Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi la Wizara,Waandishi wa Habari,Mabibi na Mabwana,Wageni Waalikwa,Ninawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...!!Mshikamanooo…!!!!Mshikamanoo ….!!!!


Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutukutanisha mahali hapa kwa ajili ya Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


 Aidha, kwa dhati kabisa, ninakushukuru wewe binafsi, Mwenyekiti wa Baraza hili pamoja na timu yako kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuwa Mgeni Rasmi kwa mara nyingine kwenye mkutano huu muhimu kwa ustawi wa Wizara yetu.


Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Kipekee ninawashukuru Watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ushirikiano mnaonipa katika kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi.


 Vilevile, ninapenda kutumia fursa hii kuwapongeza watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kutekeleza majukumu mliyopewa pamoja na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi mkubwa.


 Wananchi wameongeza imani kwa Wizara kutokana na huduma mnazotoa na hii ni kwasababu usalama wa raia na mali zao umeendelee kuimarika nchini kote. 


Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Nimeelezwa kuwa, Baraza hili limehudhuriwa na Viongozi wa Wizara, wawakilishi wa wafanyakazi kutoka katika Idara, Vitengo na Vyombo vya Usalama chini ya Wizara pamoja na waalikwa kwa kuzingatia Mkataba wa Baraza Kuu.


 Pia, Baraza hili linafanyika baada ya Mabaraza Madogo ya Mafungu yaliyopo katika Wizara kufanyika.  Nimefurahi kuona mnatekeleza mkataba huo kama mlivyokubaliana.


Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi,Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu sana mahala pa kazi kwani ni kiunganishi kati ya Menejimenti na Wafanyakazi.


 Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kushirikiana ili kuleta ufanisi kwa Wizara na Taifa kwa ujumla. Mabaraza ya Wafanyakazi yameanzishwa Kisheria kwa lengo na madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi za idara, taasisi na Wizara kuhusu usimamizi wa kazi na rasilimaliwatu, utekelezaji wa majukumu, kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi, maslahi ya Wanyakazi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi.


 Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi,Wajibu wa mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao, pia wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo ya utendaji wa kazi wenye tija, ufanisi, weledi, umahiri, staha na upendo.


Hata kama kutakuwa na Sera, Sheria na Kanuni nzuri mahali pa kazi pasipokuwa na ushirikiano baina ya mwajiri na watumishi itakuwa vigumu kwa Taasisi kutimiza malengo yake.


 Hivyo, pamoja na mambo mengine, Baraza hili lina wajibu wa kuishauri Wizara kwa lengo la kuleta tija na mshikamano baina ya mtumishi na mwajiri. 


Ni vyema madai ya maslahi ya watumishi yaendane na kiwango cha utekelezaji wa wajibu wao, kwa maana hiyo hakuna haki bila ya wajibu. 


Nichukue fursa hii kuwakumbusha na kuwasisitiza watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuendelea kutekeleza majukumu yenu ya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kazi ili kutimiza DIra ya Wizara inayosema, Nanukuu; “ kuwa Wizara yenye ufanisi katika kusimamia na kuhakikisha Amani, Utii wa Sheria, Usalama wa Raia na Mali zao” Mwisho wa kunukuu.


Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Mkutano huu ni maalum kwa ajili ya kupitia na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti wa Wizara kwa kipindi cha Julai – Novemba, 2021 kwa mwaka 2021/2022. 


Hivyo, ninawaomba mtumie fursa hii kujadili taarifa hiyo pamoja na mada nyingine zitakazowasilishwa kwa uhuru na uwazi pamoja na kutoa ushauri, maoni na mapendekezo ambayo yataisaidia Wizara kutimiza malengo yake. 


Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, maoni, ushauri na mapendekezo hayo ni vema yazingatie vipaumbele vya Wizara na maeneo muhimu ya kazi za kila Idara, Kitengo pamoja na Vyombo vya Usalama chini ya Wizara.


 Kwa kufanya hivyo itatusaidia kubaini changamoto, upungufu na uwezo tulionao ili kubainisha mikakati kwa ajili ya kutatua changamoto na kutimiza malengo ya Wizara kwa manufaa ya Taifa letu.


 Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Ninawakumbusha kuwa, katika mkutano huu wajumbe wote mna haki na fursa sawa ya kutoa maoni na michango kwa lengo la kuboresha utendaji wa Wizara.


 Kwa kuzingatia hilo, nimuombe kila mjumbe kutumia fursa hii aliyoipata kupitia kikamilifu taarifa na mada zote zitakazowasilishwa ili kuwa na michango yenye tija itakayoisaidia Wizara kuendelee kutoa huduma bora kwa wananchi ambao tumepewa jukumu la kulinda usalama wao pamoja na mali zao. 


Ninatarajia katika mkutano huu, kutakuwa na mapendekezo ambayo kwa namna moja au nyingine yataisaidia Wizara kutekeleza mipango yake kwa ufanisi. 


Ninatoa rai kwenu kujikita katika majadaliano yenye tija na yakakayosaidia kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi. 


Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Matunda ya mkutano huu, yanategemea mambo yote mtakayoyajadili na kukubaliana kwa pamoja kuyatekeleza kwa ukamilifu.


 Ninatumaini kuwa majadiliano yenu yatatawaliwa na hekima, busara, uwazi pamoja na maelewano. Ninawaomba muwe wawakilishi wazuri wa watumishi wenzetu ambao wameonesha imani kubwa kwenu na kuwachagua kuwawakilisha.


 Aidha, mtakaporudi katika vituo vya kazi mkawajulishe watumishi wenzetu mambo yote tuliyokubaliana katika mkutano huu.


 Ninatumaini kuwa, kila mtumishi atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili kuendelea kutekeleza jukumu la msingi la Wizara la kulinda usalama wa watu na mali zao.


Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Kama tunavyofahamu nchi yetu na dunia kwa ujumla kuna janga la UVIKO-19, ambalo limekuwa likipoteza nguvu kazi.


 Ninawasihi watumishi wenzagu kuendelea kuchukua tahadhari kama inavyoelekezwa na Serikali pamoja na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kujikinga na ugonjwa huu. 


Pia, kwa sasa Serikali yetu imeendelea kutoa chanjo ya ugonjwa huu kwa wananchi wote. Hivyo, kwa wale ambao bado hawajapata chanjo hiyo na wapo tayari, ni vema kupata chanjo ili kuhakikisha tunaendelea kujikinga na ugonjwa huu hatari. 


Ujanja ni Kuchanja…!Imekuwa ni desturi kuwa, kipindi cha mwisho wa mwaka, wengi wetu huwa tunapenda kwenda likizo nyumbani kwa wazazi au ndugu, ni vema tukachukua tahadhari kubwa ya kujikinga na UVICO – 19 na vilevile kuwalinda wenzetu. 


Tuvae barakoa kwenye mikusanyiko, tunawe mikono mara kwa mara, tutumie vitakasa mikono na kwenda Hospitali pale tunapohisi mabadiliko ya hali ya miili yetu. 


Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Mwisho lakini siyo kwa umuhimu, nihitimishe kwa kuwatakia mkutano wenye tija. 


Ni matarajio yangu kuwa mtahitimisha mkutano huu kwa maazimio yatakayowawezesha kufanya kazi kwa nidhamu, bidii, uadilifu pamoja na kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi.


Baada ya maelezo haya ninatamka kuwa Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi umefunguliwa rasmi leo tarehe 17 Desemba, 2021.


  Asanteni kwa kunisikiliza…!!!Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!!!!!!

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages