Na.Mpiga picha wetu - GST
Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya amefungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Madini mkoani Dodoma.
Akizungumza wakati akitoa hotuba yake, Prof. Manya alisema kuwa kazi kubwa ya Baraza la Wafanyakazi katika Taasisi ni kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu, na sio mkutano wa kushughulikia migogoro ya watumishi inayojitokeza mahali pa kazi.
Aidha, Prof. Manya aliongeza kuwa Idara inayoshughulikia masuala ya watumishi ikifanya kazi zake vizuri na Menejimenti ikaendesha Taasisi kwa uwazi anaamini kikao cha baraza la wafanyakazi kitaendeshwa kwa ufanisi zaidi na utakuwa na matokeo chanya kwa watumishi na taasisi kwa ujumla.
Sambamba na ushauri huo Prof. Manya alitumia nafasi hiyo ya kikao cha baraza kuipongeza GST kwa namna inavyojitangaza na kufanya ifahamike zaidi kwa wadau wake. “Kwa sasa GST inafahamika zaidi kwa wadau wengi, wachimbaji wadogo wa madini wanaitaja GST zaidi ukilinganisha na kipindi kilichopita. Pia, tokea kuanzishwa kwake mwaka huu GST imesogeza huduma zake karibu na wadau wa sekta ya madini kwa kuanzisha ofisi zake katika mkoa wa Geita, hongereni sana. Prof. Manya alipongeza.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba aliushukuru uongozi wa Wizara ya madini kwa namna unavyoshirikiana na GST katika kutekeleza majukumu yake. “Uendeshaji wa Taasisi unahitaji pamoja na mambo mengine rasilimali watu na fedha, ninawashukuru sana viongozi wa wizara wakiongozwa na Mhe. Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwa ushirikiano mkubwa mnaonipatia katika kutekeleza majukumu yetu ikiwemo uwezeshaji wa bajeti kwa wakati” Alisema Dkt. Budeba.
Akizungumzia juu ya uwajibikaji na uwazi mahali pa kazi Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi Serikali Kuu na Afya Tanzania (TUGHE) taifa Rugemalira Rutatina alieleza kuwa njia rahisi ya kuondoa migogoro au sintofahamu zozote zinazojitokeza ni kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji kwa watumishi kupitia njia sahihi za mawasiliano zinazowezesha kupata majibu sahihi ya changamoto husika.“Mara nyingi mahali pa kazi kumekuwepo na migogoro lakini ukiangalia chanzo chake ni kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa njia sahihi za utoaji wa taarifa zinazowahusu watumishi juu ya jambo husika” alisema Rugemalira.
Msingi wa Baraza la Wafanyakazi umetokana na dhana ya ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya masuala mbalimbali mahala pa kazi.
Dhana ya ushirikishwaji wa wafanyakazi mahali pa kazi maana yake ni uhusishwaji wa mawazo au mapendekezo ya wafanyakazi katika maamuzi ya uongozi.
Kwa Tanzania dhana hii ilitiliwa mkazo na Agizo la Raisi wa awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Agizo Namba 1 la Mwaka 1970.
*Zifuatazo ni picha mbalimbali za kikao hicho*
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇