LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 27, 2021

SIMULIZI: SAIDI MWAMWINDI, MKULIMA ALIYEMUUA MKUU WA MKOA SIKU YA KRISMASI

Mwaka 1971 siku ya Sikuku ya Noeli almaarufu Christmas, aliyekuwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Iringa, msomi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) wa Uchumi wa Kijamaa katika Kilimo ambaye alikuwa amehamishiwa mkoa huo akitokea Mtwara, Dk. Wilbert Kleruu,  aliuawa na Mkulima aitwaye Said Mwamwindi.

Kipindi hicho kulikuwa na kampeni ya kutaifisha mashamba ya wakulima wakubwa na kuyafanya mashamba ya kijiji. Na Dkt. Kleruu alipelekwa Iringa ili akatekeleze kazi hiyo kwani kipindi hicho Iringa ilikuwa na wafanyabiashara wakubwa waliomiliki mashamba makubwa ya Kilimo hasa maeneo ya Isimani.

Katika eneo hilo la Isimani kulikuwa na mkulima mmoja aliyekuwa anamiliki takribani hekari 400 za mashamba na mfanyabiashara aliyekuwa anamiliki majumba Iringa mjini - Said Mwamwindi-
Kwa wakati ule ilishauriwa angalau kila mtu awe na shamba lisilo zidi hekari 4. Jambo ambalo lilileta mvutano mkubwa kati ya wakulima wakubwa na Serikali.

Sasa siku hiyo ya Christmas, Dkt. Kleruu alikwenda Isimani akiwa katika utekelezaji wa sera ya kutaifisha mashamba. Moja kwa moja alikwenda hadi shambani kwa Mwamwindi, na kumkuta analima.

Mkuu huyo wa Mkoa akamuuliza mbona unalima shamba lako mwenyewe na si la kijiji? Mwamwindi akajibu, sioni tatizo hakuna mtu shambani, leo ni Jumapli tena ni sikukuu.

Maneno yale yalimuudhi Dkt. Kleruu, ambaye alikuwa akisifika kwa ukali, kutekeleza sera za serikali na maneno makali au kutukana watu hadharani pale wanapo fanya makosa.

Dkt. Kleruu baada ya kuudhika alimtukana Mwamwindi tusi lililomlenga mama yake ambaye tayari alikuwa marehemu. Mwamwindi alihoji inakuwaje anamtukania mama yake, huku akimuonyesha kaburi alimozikwa?

Mkuu wa Mkoa, aliendelea kuja juu, huku akisema kaburi ndio nini? Huku akilipiga mateke kaburi la Mama yake Mwamwindi. Kwa kabila la wahehe makaburi yana heshima yake, kwani ndipo nyakati nyingine hutumika katika sala, matambiko na mila kadha.

Kitendo kile kilimghadhabisha Mwamwind, na kuanza kukimbia kuelekea nyumbani. Mkuu wa Mkoa akadhani Mwamwindi anamkimbia, akaamua kumfuata.

Alipofika nyumbani, tayari Mwamwindi alisha ingia ndani na kuchukua bunduki yake, Dkt. Kleruu baada ya kuona hali ile mara moja alianza kumuomba msamaha, lakini hasira zilimuwaka Mwamwindi kama moto wa nyika; hakuwa na msamaha, alimfyetulia risasi kichwani Dkt. Kleruu na kumuua.

Baada ya kumuua, Mwamwindi aliuchukua mwili ya Mkuu wa Mkoa na kuuweka ndani ya gari (inadaiwa kwenye boneti) alilokuja nalo Mkuu huyo wa Mkoa.

Kisha alichukua kofia ya Dkt. Kleruu na kuivaa, akaingia ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea Iringa mjini tena akipita njia isiyo ruhusiwa kwani barabara ilikuwa 'one way'.

Alipo karibia mjini, askari walishangaa ni nani anaye pita njia isiyo ruhusiwa, ila mara waligundua ilikuwa gari ya RC wa Iringa, hivyo walidhani amepata dharura.

Gari lilipowasili kituoni, Polisi walijiandaa kupiga salute, mara alishuka Mwamwindi akiwa na bunduki yake na kuelekea ndani (counter). Askari walipigwa na butwaa.

Alipofika aliwaambia "Nendeni mkachukue Nguruwe wenu ndani ya gari," na Kisha akakabidhi bunduki yake.

Lilikuwa tukio la kustaajabisha, na kushangaza na lililofanyika kwa haraka sana.

Baada ya taarifa kuenea, msako wa polisi ulianza mara moja. Ila katika msako huo, Polisi waliwakamata baadhi ya watu walio kuwa wakinywa bia kwa furaha, shangwe na nderemo baada ya kusikia Dkt. Kleruu ameuawa. Kwani wanadai alikuwa na dharau.

Kesi ya Mwamwindi alipelekwa haraka sana na ndani ya miezi kadhaa, Juni 1972, Mwamwindi alihukumiwa kunyongwa hadi kufa, ikiwa ni moja ya hukumu chache za kunyongwa zilizo wahi kuidhinishwa.

Inadaiwa Mwalimu. Nyerere alihuzunishwa sana na kifo hicho, na hata kesi ya Said Mwamwindi ilipoisha na kupewa hukumu ya kifo, Inasemekana Nyerere hakusita kusaini, na ni mojawapo ya hukumu tatu tu za kifo zilizotekelezwa wakati wa utawala wa Nyerere

Said Mwamwindi

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages