LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 24, 2021

NAIBU WAZIRI PINDA: OFISI YA MWANASHERIA MKUU NI NYETI NA YENYE DHAMANA KUBWA KWA SERIKALI

Na  Mwandishi Maalum, Mwanza
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geophrey Mizengo Pinda, amewataka Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  kutambua uzito na dhamana ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika uendeshaji wa  Serikali.

Ameyasema hayo leo, Wakati akifungua Mkutano wa siku mbili  wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambalo linafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo  la TMDA  Mkoani hapa.

Naibu Waziri Pinda amesema,  kwa mujibu wa  majukumu  ambayo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepewa Kikatiba, Ofisi hiyo ni nguzo na  mhimili wa uendeshaji wa Serikali na kwamba ufanisi wa serikali kwenye masuala ya  kisheria unawategemea sana watumishi wa hiyo Ofisi.

“Kwa muktadha huu ni  vyema mtambue kuwa mmpewa majukumu nyeti, na mmebeba dhamana kubwa ya kuiwezesha Serikali  kutekeleza majukumu yake, na ninyi ndiyo taswira ya taifa letu kwenye masuala ya Utawala na Sheria” amesisitiza Naibu Waziri Pinda.
 
Aidha  ametoa rai kwa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kwamba wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu wa kiwango cha juu na kwa maslahi mapana ya nchi na kwamba kufanya watumishi hao wataiwezesha Serikali kupata ushindi kwenye kesi nyingi na kupunguza migogoro ya kisheria baina ya Serikali na Wabia.

Katika  Baraza hilo la Wafanyakazi ambalo Mwenyekiti wake ni  Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Eliezer Feleshi, Naibu  Waziri  Pinda pia ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuendeleza juhudi za Serikali za kuondokana na Sheria zenye mianya ya rushwa kwa kuandaa Mikataba yenye tija na inayozingatia maslahi ya Taifa.

Vile vile Naibu Waziri Pinda amesisitiza  watumishi wa Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuvitambua vipaumbele vya Serikali ya awamu ya Sita na jinsi gani vipaumbele hivyo vinatekelezwa kwa kuzingatia majukumu ya  Ofisi.

Pamoja na  kusisitiza matumizi  ya  lugha ya Kiswahili katika  utoaji haki, pia amesisitiza umuhimu kwa watumishi kuzingatia Sheria, Kanuni na miongozo ya kiutumishi na kiutendaji, ikiwa ni pamoja na  kuweka mfumo wa kufutailia utendaji wa wanasheria wote wa Serikali  na mpango wa Mawakili wote kupata uzoefu wa kazi mahakamani.

Awali  akimkaribisha  Naibu Waziri wa Katiba na Sheria  kufungua mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Feleshi, alisema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  haitamvumilia mtumishi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa.

“Katika eneo hili la uadilifu, nawasihi watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Muu wa Serikali mnatakiwa kutekeleza majukumu yenu ya kazi kwa kuzingatia Maadili ya Utumishi wa Umma,  Sheria na Kanuni. Mla rushwa  hata vumiliwa hata kidogo” ameonya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kuhusu idadi ya watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Feleshi amesema  kwa mujibu wa Muundo wa Ofisi, Ofisi inahitaji kuwa na watumishi 477 ili kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika mikoa yote 26.

“Mheshimiwa Naibu Waziri  watumishi waliopo sasa ni  121, kati yao hao Mawakili wa Serikali ni 54  na watumishi wa kada nyingine ni 67, idadi hii ya watumishi hasa Mawakili wa serikali ni ndogo sana ikilinganishwa na mahitaji ya mawakili wa Serikali 241 wanaohitajika kutokana na kuongezeka kwa majukumu ya Ofisi katika maeneo ya upekuzi wa mikataba, Uratibu wa Huduma za Ushauri wa Kisheria na Uandishi wa Sheria.

Dk. Feleshi alisema  Ofisi imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za  kuongeza watumishi kwa kutenga nafasi za uhamisho na ajira mpya kwenye Ikama kila mwaka na kuwasilisha Ofisi ya Rais,  Utumishi  na Utawala Bora kwa Hatua zaidi.

Amebainisha kwamba suala  la uhaba wa watumishi haupo tu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bali pia ni tatizo ambalo pia linazikabili Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na kwamba zoezi la kukamilisha uchambuzi wa mahitaji ya watumishi kufuatia mahitaji halisi ya huduma za kisheria zintolewazo na ofisi hizo kwa mujibu wa Katiba na Sheria  ili kwenda na mgawanyo wa maeneo ya kiutawala  Serikalini.

Mkutano huo wa Baraza la  Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unahudhuriwa na  Wanachama 45 wa Chama cha Wafanyakazi cha TUGHE na Wajumbe waalikwa wakiwamo Mawakili wa Serikali  wanaosimamia Ofisi  za Tabora, Dar es Salaam,  Tanga, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Mtwara na Kagera.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Dk. Eliezer Feleshi alipokuwa akimkaribisha Mgeni Rasmi Naibu Waziri  Geophrey Pinda  Baraza la Wafanyakazi  la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo  la TMDA  Jijini Mwanza.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geophrey Mizengo Pinda akifungua Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Wafanyakazi  la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo  la TMDA Jijini Mwanza. (Picha zote na Mpigapicha Maalum)

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages