LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 19, 2021

NAIBU KATIBU MKUU CCM BARA AAGIZA UCHUNGUZI WATUMISHI WA AFYA KUWATAKA WATU KUVUA VIATU WODINI

 


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christina Mndeme ameagiza uchunguzi dhidi ya watumishi wa afya wilayani Uvinza kuwataka wananchi kuvua viatu pindi wanapoingia wodini kuwatembelea wagonjwa.

Mndeme amesema mtumishi atakayebainika kutoa agizo hilo kinyume cha utaratibu, hatua kali za kinidhamu zichukuliwe kwa muhusika.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, aliyasema hayo juzi jioni wakati akizungumza na wananchi katika Shina Namba 1, Tawi la CCM Nyakatakala A, wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

“Hii ni kero ambayo wakina mama inawasumbua kuwambiwa kuvua viatu wanapoingia wodini. Wanachohofia wanasema tunavua viatu kuingia wodini inawezekana mule wodini sio salama unaweza ukaondoka na magonjwa mengine.

Aliongeza kuwa: “Nakuagiza kamisaa wetu (Mkuu wa Wilaya) serikali lichunguzeni hili suala la wanawake kulazimishwa kuvua viatu pindi wanapoingia wodini kutizama wagonjwa.”

Alisema uchunguzi ufanyike kubaini nani aliyetoa maagizo hayo na kwa sababu zipi na hatua kali za kinidhamu zichukuliwe kwa muhusika.

“Ni mtu mmoja ameamua watu wasiingine na viatu. Ni hospitali gani watu huwa tunaingia bila kuvaa viatu. Hakuna hospitali ambayo watu wakienda wanavua viatu.

“Kwanini hapa tunaambiwa tuvue viatu? hili limeleta ukakasi. Hawa wahudumu nani kawapa maelekezo ya kuwavua viatu ndugu wa mgonjwa?. Serikali lichunguzeni kama mtu ameamua kwa mapenzi yake kuwavua watu viatu hatua za kinidhamu zichukuliwe,” alisisitiza huku akishangiliwa na wananchi baada ya kutoa agizo hilo.

Awali, katika risala iliyosomwa na Katibu wa Shina hilo, Ali Kimilila, alisema miongoni mwa changamoto za wananchi wa Kata ya Basanza ni wahudumu wa afya kuwataka kuvua viatu pindi wanapoingia wodini kuwatembelea wagonjwa.

Akielezea kwa undani kuhusu vitendo hivyo, Mkazi wa Kijiji cha Basanza, Neema Julius, alisema imekuwa kawaida kwa wao kutakiwa kuvua viatu wanapoingia wodini kuwatembelea wagonjwa.

“Mule wodini wakati mwingine sio kusafi alafu tunaambiwa tuvue viatu. Hii unaweza kusababisha sisi kupata maambukizi,” alieleza.

Kutokana na malalamiko hayo, Mndeme alimtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uvinza kujibu malalamiko hayo mbele ya wananchi katika mkutano huo.

Akijibu malalamiko hayo, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya, Hussein Kateranya, alisema malalamiko hayo ndio kwa mara ya kwanza ameyasikia, hivyo aliahidi kuyafanyia kazi kubaini wahusika na sababu za kutoa agizo hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Anafi Msabaha, alisema serikali itachungua suala hilo na kuchukua hatua kwa wahusika.

“Ninachofahamu kuna maeneo hospitalini hupaswi kuingia na viatu kama chumba cha upasuaji ambako utatakiwa uvae viatu vingine ndipo uingie. Lakini hapa ni tofauti watu wanazuiwa kuingia na viatu hadi wodini. Tutachukua hatua,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages