LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 11, 2021

MKUU WA WILAYA YA IRAMBA SULEIMAN MWENDA APIGA MARUFUKU SHUGHULI ZA KIBINADAMU KANDO YA VYANZO VYA MAJI

Na Mwandishi Maalum, Iramba
Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda amepiga marufuku wananchi kufanya shughuli mbalimbali za kibinadamu kando ya vyanzo vya maji.

Mwemda ametoa marufuku hiyo jana, katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maji katika Kata ya Maluga Wilayani ya hapa ambapo katika ziara hiyo aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.

Amemtaka Mhandisi wa Maji, Ezra Mwacha kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na iwe na viwango vinavyofanana na fedha iliyotolewa.

Katika hatua nyingine DC Mwenda amezitaka Serikali za Vijiji kuhakikisha vinalinda vyanzo vya maji ambapo Serikali imewekeza fedha nyingi ili huduma hiyo itatuwe changamoto ya kupatikana maji kwa muda mrefu.

“Nawaagiza Wenyeviti wa Vijiji vyote ambavyo miradi ya maji inatekelezwa kulinda miradi ambayo Serikali inajenga kwa fedha nyingi na kutouza maeneo ya vyanzo vya maji. Hakikisheni mmepanda miti katika vyanzo vyote vya maji ili kulinda vyanzo hivyo kwa masilahi yetu wote.” alisema DC Mwenda.

Pia, alimtaka Mhandisi wa Maji, Mafundi Sanifu na Venyeviti wa Vijiji katika maeneo mbalimbali yanayotekeleza miradi hiyo kuijenga kwa kiwango bora ili kutimiza makusudio ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha maji yanapatikana kila eneo na muda wote ili kumtua mama ndoo ya maji.

Akizungumza na wananchi katika ziara hiyo mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Wananchi Wilayani hapo, SSP. Peter Lusesa amewataka wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wanatumia sheria ndogo kulinda vyanzo vya maji hali ambayo itawaepusha na migogoro ya hapa na pale.

Awali akitoa tarifa fupi ya utekelezaji wa miradi ya maji mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya, Meneja wa Maji Wilayani hapo, Mhandisi Ezra Mwacha alisema kuwa kazi zinazoendelea katika maeneo yote ambayo miradi inatekelezwa ni ujenzi wa matenki ya kuhifazia maji mita 12 na yenye ujazo wa lita 50,000, nyumba za  kuhifadhia mashine (vyanzo vya maji), uchimbaji wa mitaro na DP nane katika kila mradi.  

Aidha alifafanua kuwa miradi mitatu aliyoitembelea Mkuu wa Wilaya inatakribani 1.2 Bilioni na kumuhakikishia kuwa ifikapo Machi 2022 miradi itakuwa imekamilika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Zinziligi Tarafa ya Ndago Wilayani hapa, Anthony Kitalu amemshukuru Rais Samia kwa kuwaletea miradi ya maji ambayo inatatua changamoto ya kupata maji waliyokuwa nayo kwa kipindi kirefu.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Wananchi hawa wameipokea miradi hii kwa mikono miwili na kukuomba wewe uwafikishie salamu kwa Rais Samia kwa huruma yake ya kuwaletea maji.” Alisema Kitalu.

DC Suleimani Mwenda akizungumza katika ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages