Madaktari wazawa mabingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (aorta) uliokuwa umetanuka pamoja na valvu yake (Aortic valve insufficiency) bila ya usimamizi wa madaktari kutoka nje baada ya miaka kadhaa ya kujifunza upasuaji huo kutoka kwa wataalam wenzao wanaofika JKCI kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.
*********************************
Kwa mara ya kwanza madaktari wazawa mabingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (Aorta) uliokuwa umetanuka pamoja na valvu yake (Aortic valve insufficiency) bila ya usimamizi wa madaktari kutoka nje baada ya miaka kadhaa ya kujifunza upasuaji huo kutoka kwa wataalam wenzao wanaofika JKCI kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.
Upasuaji huo unaojulikana kwa jina la kitaalamu la Bentall Surgery uliochukua masaa matano kukamilika ulifanyika hivi karibuni ambapo mgonjwa anaendelea vizuri na anatarajia kuruhusiwa wakati wowote kuanzia sasa.
Mgonjwa huyo alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya kifua na baada ya uchunguzi aligundulika kuwa mshipa mkubwa wa damu (aorta) unaotoa damu kutoka kwenye moyo na kusambaza damu mwili mzima umepanuka sana na valvu yake ya moyo inavuja damu.
Akizungumzia upasuaji huo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Godwin Sharau alisema tatizo hilo mara nyingi huwapata watu wengi wenye umri wa kuanzia miaka ya 50 kwenda juu lakini pia uwapata watu wanaosumbuliwa na shinikizo la damu la muda mrefu hivyo mshipa huo kupoteza umahiri wake wa kuweza kustahimili presha.
Dkt. Sharau ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto alisema kwa mgonjwa ambaye hatapata matibabu husika kwa wakati mshipa huo huendelea kutanuka na hivyo kupelekea kufa ghafla.
“Kwa miaka mingi upasuaji wa Bental operation kwa hapa JKCI umekuwa ukifanyika lakini chini ya usimamizi wa madaktari wenzetu kutoka nje ya nchi, sasa wataalam wetu wameonesha umahiri mkubwa wa kufanya upasuaji huu. Hii ni hatua nzuri sana katika Taasisi yetu”, alisema Dkt. Sharau.
“Upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (Aorta) uliotanuka pamoja na valvu yake huchukua muda mrefu kutokana na ubadilishaji wa mishipa lakini pia baada ya upasuaji huu mgongwa anaweza akavuja damu kwa wingi na wakati mwingine kupoteza maisha”, alisema Dkt. Sharau
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya upasuaji watu wazima wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Evarist Nyawawa alisema mgonjwa huyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina ilionesha yakuwa mshipa mkubwa wa damu (Aorta) ulikuwa umetanuka kiasi cha kwamba muda wowote ungeweza kupasuka.
“Mgonjwa tuliyemfanyia upasuaji wa mshipa wake mkubwa wa damu (Aorta) pamoja na valvu yake (Aortic valve) iliyokuwa inarudisha damu kwenye chemba ya kushoto ya moyo ilikua inamfanya mgonjwa akose nguvu na kushindwa kupumua vizuri”, alisema Dkt. Nyawawa.
“Sasa tuna uzoefu mkubwa naamini tutaendelea kuokoa maisha ya watanzania wengi ambao wanahitaji upasuaji kama huu, na hii itapunguza wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta huduma za kibingwa za matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Nyawawa
Naye Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (aorta) uliotanuka pamoja na valvu yake (Bental operation) Benny Mongi aliwashukuru wataalamu hao wa JKCI na kuwapongeza kwa kutumia utaalam wa hali ya juu waliokuwa nao kwa kuokoa maisha yake.
“Nimeambiwa huduma kama hii niliyofanyiwa na madaktari wa JKCI haikuwahi kufanyika kupitia madaktari wazawa lakini kwangu wameweza, nikirejea nyumbani baada ya matibabu haya naenda kutoa ushuhuda wa huduma hii niliyoipata hapa hapa Tanzania ili watanzania wenzangu wafahamu na kutumia vizuri rasilimali zetu ambazo serikali yetu imetuwekea”,.
“Nimekuwa nikitafuta hewa kwa mikono kutokana na matatizo ya moyo niliyokuwa nayo, sikuwa naweza kupumua kabisa mikono yangu muda wote ndio ilikua ikinisaidia kujipulizia ili nipate hewa, sitaacha kumshukuru Mwenyezi Mungu na wataalam hawa kwa kuokoa maisha yangu”, alisema Mongi.
Kwa kipindi cha mwezi mmoja wa Oktoba hadi Novemba 2021 madaktari wazawa mabingwa waupasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (aorta) uliokuwa umetanuka pamoja na valvu yake (Aortic valve insufficiency) bila ya usimamizi wa madaktari kutoka nje ya nchi kwa mgonjwa mmoja na upandikizaji wa mishipa ya damu ya moyo bila ya kusimamisha moyo kwa wagonjwa watatu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇