LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 28, 2021

KEKO FC BINGWA JIMBO KILAVE CUP 2021, MBUNGE KILAVE AMWAGA ZAWADI ZA MAMILIONI KWA TIMU HIYO NA WASHINDI WENGINE

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Timu ya Keko FC imeibuka kidedea katika Mchuano wa Kilave Jimbo Cup 2021, baada ya kuichapa Timu ya Tandika Combine bao 1-0 katika mechi ya fainali Iliopigwa baina ya timu hizo katika Uwanja wa Bandari, Temeke jijini Dar es Salaam, jana, Jumamosi. Novemba 27, 2021.

Kufuatia ushindi huo Keko FC imetwaa Kombe la gharama ya Sh. Million 2.5, fedha taslimu Sh. milioni moja, Seti 3 za jezi na Mipira mitatu, huku mshindi wa Pili, Tandika Combine ikitwaa Fedha taslim Sh. 500,00, Seti mbili za Jezi na Mipira miwili.

Katika zawadi hizo za mamilioni zilizotolewa mapema na Mbunge wa Jimbo la Temeke Dorothy Kilave, wakati wa hotuba yake,Timu za Temeke 14 na Azimio Combine zilizawadiwa kila timu Seti moja ya jezi na Mpira mmoja kwa kufanikiwa kuingia nusu fainali huku timu ya Chuo cha Diplomasia (Diplomasia FC) nayo ikiingiza kibondoni Sh. 100,000 kwa kuongoza kuwa timu yenye Nidhamu katika muchuano hiyo.

Pia zawadi ziliendelea ambapo golikipa bora katika michuano hiyo alipata pea moja ya gloves na fedha taslim sh. 50,000 huku Kikundi Bora cha ushangiliaji nacho kikiondoka na zawadi ya fedha taslim Sh. 100,000.

Katika mechi hiyo ya fainali za Jimbo Kilave Cup 2021 Mbunge Kilave aliambatana na Viongozi mbali mbali wakiwemo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanzia ngazi ya Matawi hadi Wilaya, Viongozi wa Dini, Wabunge wa Viti Maalum (CCM) Mariamu Kisangi na Stella.

Wengine waliohudhuria fainali hiyo ni Viongozi wa Serikali, Kutoka katika Mitaa ya Jimbo la Temeke, Madiwani wa Manispaa ya Temeke, Watendaji wa Kata na Viongozi wa Taasisi Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kutoka Jimbo hilo la Temeke.

Mapema Mbunge katika hotuba yake alizipongeza timu zote 16, zilizoshiriki Michuano hiyo ya Kilave Jimbo Cup 2021,  na pia alikumbusha kuwa kauli mbiu ya Mashindano hayo ni 'Michezo ni Afya, Kazi na Ajira'  huku akiwataka wananchi jimboni humo kushiriki michezo kwa pamoja bila kubaguana kiitikadi za siasa na pia kila mmoja kupata Chanjo ya UVIKO 19 na kufanya kazi kwa bidii.

Vilevile, Mbunge Kilave alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Wananchi wa Temeke kushiriki zoezi la Sensa ya watu na Makazi litakalofanyika Oktoba  mwakani, Kisha kuwaomba Wananchi kuendelea kutii utaratibu wa ufanyaji wa Usafi katika Mazingira wanayoishi, kama inavyoagizwa na Mkuu wa Mkoa Amosi Makalla na Mkuu  wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo.

Aidha Mbunge Kilave, aliwahakikishia Wananchi Juu ya Mipango ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani, katika kuwaletea Maendeleo Watanzania na amewataka kushiriki kikamilifu katika kulipa Kodi kwa Maendeleo ya Taifa.

Akizungumza kwenye hafla hiyo ya mechi ya fainali Meya wa Manispaa ya Temeke Abdalla Mtinika ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi alimpongeza Mbunge Kilave kwa Kuthamini, kuandaa, kusimamia na kuratibu Jambo la Michezo akisema ni jambo jema ambalo mbali na kujenga Umoja pia Michezo ni Afya, Kazi na Ajira.






No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages