Makamu wa Rais wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu, (TAPIE), Mahmodu Mringo akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa chama hicho ambao pamoja na mambo mengine ulimchagua yeye na kamati yake ya utendaji kuongoza tena kwa muda wa miaka mitano.
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu (TAPIE), kimemchagua Mkurugenzi wa shule za Paradigms Mahmoud Mringo kuongoza chama hicho kwa muda wa miaka mitano.
Mringo na Kamati ya Utendaji wote walipita bila kupingwa kwenye uchaguzi uliofanyika kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Wengine waliochaguliwa bila kupingwa ni Makamu wa Rais wa chama hicho, Chacha Wambura ambaye ni Mkurugenzi wa shule zaa WAJA, Katibu Mkuu Dk. Albert Katagira ambaye ni Mkurugenzi wa shule za Tusiime na Mweka Hazina ni Shani Khalfan Swai (CPA), Mkurugenzi wa shule ya Baobab Mapinga Bagamoyo.
Akizungumza mara baada ya kupitishwa, Mringo alisema atafanya mabadiliko makubwa kuiwezesha taasisi hiyo kuwa imara na kuwa mtetezi wa wamiliki wa shule ambao alisema wanabakiliwa na changamoto mbalimbali.
Akizungumza kwenye mkutano huo jana, Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Maulid aliwataka wamiliki wa hule binafsi zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali kuziwasilisha serikali ili zipatiwe ufumbuzi.
“Semeni nini mnataka serikali iwafanyie sisi tuko tayari kupokea changamoto zenu na kuzifanyia kazi na mengine makubwa tutayapeleka sehemu husika kwaajili ya kupatiwa ufumbuzi,” alisema
Aliwataka wamiliki wa shule hizo kuziendesha kwa kufuata sheria za nchi kwa kuhakikisha zimesajiliwa na kupata vibali vyote vinavyohitajika kwaajili ya usajili.
Alisema serikali inawajali na kuwathamini sana wamiliki wa shule binafsi kwani wamekuwa wakipata changamoto kama ambazo maofisa wa elimu wamekuwa wakizipata hivyo wanachotakiwa kufanya ni kushirikiana kwaajili ya kuzitatua.
“Nyinyi mnapata changamoto kama sisi tunavyopata changamoto sasa naomba niwaambie changamoto zangu kwenu nanyinyi mtaniambia za kwenu cha muhimu endesheni shule zenu kwa kufuata sheria,” alisema
Afisa Elimu alisema changamoto nyingine ni tabia ya baadhi ya shule ambazo zimekuwa zikitumia mbinu mbalimbali kuiba mitihani kwa lengo la kufaulisha wanafunzi wengi .
Alitaka wamiliki wa shule hizo kukomesha tabia hiyo na kusimamia vizuri walimu wao waweze kufundisha kwa viwango ili waweze kufaulu bila kutumia njia haramu za wizi wa mitihani ambayo itawasababishia matatizo.
Alisema mkoani Dar es Salaam kuna baadhi ya shule binafsi ambazo zimekuwa zikisua sua kutokana na uhaba wa fedha na kuwataka kwenda kukopa CRDB kama ambavyo wameahidiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo.
Aliwataka wamiliki hao kuzitangaza shule zao zinapopata matokeo mazuri au huduma bora zinazopatikana lakini wasitumie mbinu chafu ambazo zinasababisha maumivu kwa watu wengine.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇