LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 21, 2021

CCM Blog: RAIS WA BURUNDI KUTUA JIJINI DODOMA KESHO, KUZURU ZANZIBAR KESHOKUTWA

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Burundi Evariste Ndayishimiye, anatarajiwa kuwasili nchini kesho kuanza ziara ya Kitaifa ya siku tatu kuanzia hiyo kesho Ijumaa, tarehe 22 hadi 24 Oktoba, mwaka huu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amesema Rais Ndayishimiye atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma na kwenda Ikulu ya Chamwino ambako atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema baada ya kuwasili Ikulu ya Chamwino, Rais Ndayishimiye atakagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21 kwa heshima yake na baadae viongozi hao watakuwa na mazungumzo ya faragha na kufuatiwa na mazungumzo rasmi.

Balozi Mulamula amesema akiwa jijini Dodoma siku hiyo (kesho) mchana) Rais Ndayishimiye atatembelea na kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kuzalisha mbolea ya asili yenye mchanganyiko wa madini ya phosphate na samadi kinachojengwa katika eneo la viwanda la Nala, kiwanda ambacho kinajengwa na Wawekezaji wa kampuni ya Itracom Fertilizers Limited (ITRACOM) ya Burundi na baadaye jioni atahudhuria dhifa ya kitaifa itakayofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Oktoba 23, 2021 Rais Ndayishimiye ataenda Zanzibar ambako atapokelewa na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi na kuwa na mazungumzo na mwenyeji wake huyo na baadaye ataelelekea Mkoani Dar es Salaam ambapo ataungana na mwenyeji wake Mhe. Rais Samia .

Amesema akiwa jijini Dar es Salaam Rais Ndayishimiye anatarajiwa kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na kukagua ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaoendelea nchini kutokea stesheni ya Dar es salaam hadi stesheni ya Kwala – Ruvu pamoja na kutembelea bandari kavu ya Kwala inayojengwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania katika eneo hilo la Kwala mkoani Pwani ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa bandari kavu hiyo.

Akizungumzia ziara hiyo ya Rais Ndayishimiye nchini, Balozi Mulamula amesema ni mwendelezo wa hatua zinazochukuliwa na Serikali za Tanzania na Burundi za kuimarisha uhusiano na ushirikiano kwa maslahi ya pande zote na itaendeleza na kukuza ushirikiano uliopo na kufungua fursa ya kuanzisha maeneo mingine ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuwawezesha Waheshimiwa Marais hao (wa Tanzania na Burundi) kufahamu hatua zilizofikiwa katika kutekeleza maagizo yao waliyoyatoa wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Burundi tarehe 16 na 17 Julai, 2021.

Balozi Mulamula amesema Mhe. Rais Ndayishimiye na ujumbe wake wanatarajiwa kuondoka nchini kurejea Burundi tarehe 24 Oktoba 2021 baada ya kumaliza ziara yake.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages