LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 27, 2021

NMB YATANGAZA FAIDA YA KIHISTORIA YA SH.BILIONI 211 BAADA YA KODI

 

…………………………………………………………………..

Katika robo ya tatu ya mwaka iliyoishia Septemba 2021, Benki ya NMB imeonesha ufanisi mkubwa na mafanikio katika maeneo mbalimbali ya kimkakati.

Kasi ya ongezeko la mapato iliendelea huku uwekezaji katika maeneo mapya na utekelezaji mipango endelevu ya kidijitali nayo ikiimarishwa pia.

Nidhamu ya kukabiliana na hatari za kiuendeshaji na ya maswala yote ya utawala bora yalizingatiwa kikamilifu kipindi chote cha robo hii ya mwaka.

Matokeo ya kuimarika kiutendaji yameiwezesha NMB kupata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 302 na faida baada ya kodi ya shilingi Bilioni 211, hili ni ongezeko la asilimia 43 ya faida iliyopatikana kipindi kama hicho mwaka jana na zaidi ya faida ya kihistoria ya mwaka wote wa 2020 ambayo ilikuwa ni kiasi cha Shilingi bilioni 206.

Nidhamu ya hali ya juu ya NMB katika kutekeleza mipango yake ya kimkakati imeendelea kuiongezea imani kwa wateja na hivyo  na kuifanya iimarike zaidi kwenye nafasi yake ya benki inayoongoza nchini.

Katika kipindi cha miezi 9 kufikia mwezi Septemba 2021, jumla ya mapato ya NMB yalikuwa ni Shilingi bilioni 721, kiasi ambacho ni asilimia 20 zaidi ya TZS bilioni 601 zilizopatikana kipindi kama hicho Mwaka 2020 ikichangiwa zaidi na  kuongezeka kwa mikopo na miamala.

Mikakati ya benki ya kudhibiti gharama za uendeshaji imeendelea kuzaa matunda na kusababisha kuboreka kwa uwiano wa matumizi na mapato halisi kufikia asilimia 47 kutoka asilimia 52, kiwango kilicho ndani ya matakwa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) cha asilimia 55. Benki inaendelea kuboresha utendajikazi na uwekezaji hasa kwenye maeneo ya kimkakati.

Ubora wa mikopo umeendelea kuimarika ambapo uwiano wa mikopo chechefu umeshuka hadi asilimia 3.8 kwenye robo ya tatu, kutoka asilimia 6.6 kipindi kama hiki mwaka jana ikionyesha hatua nzuri iliyopigwa kudhibiti ukopeshaji usiokuwa na tija.

NMB imeendelea kuwa na mizania madhubuti ambayo ukuaji wake unaonyesha kuimarika kwa mahusiano na wateja wetu. Mwishoni mwa robo ya tatu ya mwaka, mikopo iliongezeka kwa asilimia 13 hadi kufikia shilingi trilioni 4.5 kutokana na kukua kwa mikopo kwenye maeneo muhimu  hasa kilimo, biashara ndogo na za kati pamoja na mikopo binafsi.

Amana za wateja nazo ziliongezeka kwa asilimia 18 mpaka shilingi trilioni 6.1 kufikia tarehe 30 Septemba 2021 ukilinganisha na shilingi trilioni 5.3 mwezi Septemba 2020 kutokana na NMB kuendelea  kutoa suluhisho stahiki katika kuimarisha urahisi na upatikanaji wa huduma za kibenki kwa wateja. 

Mali zote za benki zilikuwa na thamani ya shilingi trilioni 8.2 mwishoni mwa Septemba 2021, ongezeko la asimilia 17 (YoY) kutoka TZS trilioni 7 kipindi kama hicho mwaka jana.

Akitoa maoni yake juu ya utendaji huo na nafasi ya NMB sokoni, Afisa Mtendaji Mkuu, Bi Ruth Zaipuna, alisema: “Timu ya wafanyakazi wetu imekuwa na kipindi kingine chenye mafanikio kwa kuongeza faida ya miezi 9 kwa asilimia 43, hali inayoonyesha kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi na hatua madhubuti za sera za fedha zilizopitishwa na Benki Kuu ya Tanzania.”

“Mkakati wetu wa uendeshaji umeendelea kuwa sahihi huku mafanikio ya kuendeleza umiliki wa soko ukipelekea kupatikana kwa faida kubwa.Tunaendelea bila kuchoka kuzingitia matakwa ya wateja na tumeshuhudia kukua kwa kasi ya ukopeshaji na amana za wateja kwa mwaka huu mzima,” Bi Zaipuna aliongeza.

“Tukiwa kinara wa Ajenda ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa nchi yetu, katika kipindi cha miezi 9 cha mwaka 2021 tumekuwa na  mafaniko makubwa yafuatayo:

  • Tulitekeleza mipango kadhaa kwenye uwekezaji katika shughuli za kijamii sanjari na nguzo kuu za mikakati yetu. Upande wa afya tuliwafikia watu zaidi ya elfu 48 (48,000) kupitia misaada ya vifaa tiba. Wanafunzi zaidi ya elfu kumi (10,000) walinufaika na madawati  tuliyoyatoa. Pia tuliwawezesha vijana na watu wazima 3,500 kupata elimu hitajika katika maswala ya fedha kupitia program yetu ya elimu ya kifedha kwa jamii
  • Tulifanikisha mbio za NMB Marathon maarufu kama ‘‘Mwendo wa Upendo’’ zilizotuwezesha kukusanya shilingi milioni 400 kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa Fistula kwa akina mama.
  • Pia hivi karibuni tumezindia mfumo wa ‘’sandbox environment’’unaozipa kampuni chipukizi fursa ya kubuni suluhishi  za kidijitali na kuzifanyia majaribio kwenye mifumo yetu kwa minajili ya kujenga jamii ya Kitanzania iliyojumuishwa kwa teknolojia za kisasa. .

Aidha, Bi Zaipuna aliongeza kusema: “Tuna furaha na fahari kwamba mafanikio yetu katika maeneo muhimu ya utendaji, ubunifu na huduma kwa wateja, zietufanya tuweze kupata tuzo saba za kimataifa, zote zikiitaja NMB kuwa benki bora Tanzania. Tuzo hizi zinaipa benki msukumo wa kuendelea kutoa huduma bora zaidi sokoni.

“Tunawashukuru wateja wetu wenye thamani kubwa kwetu, wanahisa, wadau wote na wafanyazi kwa ujumla kwa kuendelea kutuunga mkono. Tunapoelekea kumaliza mwaka wa 2021 tuna matumaini makubwa na safari iliyo mbele yetu na tutaendelea kujitolea kusizadia jamii zote tunazozihudumia.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages