LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 20, 2021

KANISA HALISI LAWAALIKA BODABODA KUHUDHURIA IBADA YA KUFUTA AJALI, ITAFANYIKA JUMAPILI HII KWENYE KANISA HILO, TEGETA

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog

Katika jitihada za Serikali kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, usafiri na usafirishaji nchini ulifanya Serikali ikubali kuidhinisha pikipiki za matairi awili na matairi matatu maarufu (Bajaji) kutumika  katika  biashara  ya usafiri na usafirishaji wa abiria.  

Bila shaka pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo, uamuzi  huu ulichangiwa pia kwa  kiasi kikubwa na idadi  kubwa ya vyombo hivi katika  maeneo mbalimbali  nchini na kutumika bila kuruhusiwa na mamlaka zinazosimamia usafiri na usafirishaji wa abiria nchini.  
 
Na kwa hakika uamuzi huo wa Seikali umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwapatia vijana wengi nchini shughuli  ya  kuwapatia kipato halali na kuwaepusha na uwezekano wa kushawishika kujiingiza katika shughuli haramu ikiwemo uhalifu.


Pamoja na kutoa ajira kwa vijana wengi, uamuzi huu wa Serikali pia umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la usafiri katika maeneo mengi nchini hasa katika maeneo ambayo usafiri wa magari hauna uhakika. Maeneo mengi ambayo magari ya abiria hayawezi kufika sasa yanafikika kirahisi kwa pikipiki.  

Wananchi wa kipato cha chini wanaweza kutoka eneo moja kwenda jingine kwa gharama nafuu zaidi  tofauti  na  hali ilivyokuwa kabla ya uamuzi huo wa Serikali. 

Aidha, katika miji yenye  tatizo  la  msongamano  mkubwa  watu na magari barabarani husasani  Jiji la  Dar  es  salaam pikipiki  zinasaidia sana wananchi kuepuka msongamano na kuwahi katika shughuli zao za kujipatia kipato na kurejea majumbani kwa wakati.
 
Lakini kama  ambavyo mambo mema siku zote huwa hayakosi changamoto, matumizi ya pikipiki katika usafirishaji wa abiria yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambapo kubwa kuliko zote ni ajali nyingi za barabarani zinazohusisha pikipiki.

Matumizi ya pikipiki nchini yamesababisha ongezeko kubwa sana la ajali za barabarani ambazo zimesababisha vifo vya Watanzania wengi sana.


Pamoja na upotevu wa maisha, ajali hizi zimewasababishia watu ulemavu wa kudumu watu kwa kupoteza viungo vyao na kuwafanya kuwa tegemezi.
 
Kwa mujibu wa taarifa za Serkali ilizopo kwa jumla Matukio ya ajali za pikipiki (hususani Bodaboda)  ni mengi idadi ya vifo na majeruhi ni kubwa  kiasi cha kusababisha hospitali nyingi nchini kuanzisha wodi maalum za majeruhi wa pikipiki.  

Kutokana na Changamoto hiyo ya ajali za Pikipiki (bodaboda) serikali kwa upande wake imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana nayowatu wasiojiweza na kuwafanya wawe tegemezi.   
 
Bila shaka jukumu la kupambana na changamoto hii ni la Watanzana wote, ndiyo maana Serikali inasisitiza kuwa ni vema wadau wote washirikiane kwa pamoja kwa manufaa ya  wananchi badala ya wengine kukaa pembeni na  kutoa lawama kwa Serikali.

Kanisa Halisi la Mungu Baba lenye Makao yake Makuu Tegeta, jijini Dar es Salaam, limeoyesha kuguswa na changamoto hiyo ya ajali za Bodaboda, hivyo kwa kuwajibika kama sehemu ya kuisaidia jamii limeandaa Ibada Maalum ya 'Kufuta ajali'.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo anayetambuliwa kwa jina la Baba Halisi wa Uzao, amesema Ibada hiyo itafanyika Jumapili, Oktoba 24, 2021 Makao Makuu ya Kanisa hilo, Tegema na ametoa Mwaliko kwa Bodaboda wote kuhudhuria Ibada hiyo.

 

Mwaliko wa Kanisa Halisi ulioandikwa na Baba Halisi wa Uzao na sisi ukatufikia, 

huu hapo 

👇 

Lango la 5 Eluli, Vol.2 (17 Oktoba,2021) Kanisa Halisi la MUNGU BABA, lilifuta tamko la Ole kwa waandishi wa Habari, lililotolewa na Yesu zaidi ya miaka 2000 iliyopita.Ukifuatilia mwenendo wa waandishi wa habari, ni kweli tamko hilo la Ole kwao lilikuwa bado linasonga utendaji wa waandishi. Kuanzia tarehe tajwa hapo juu, Ufunuo 22:3, inayosema kuwa “hapatakuwa na laana yoyote tena”, ilitimia kwa waandishi wa habari na Janmii yote pia.

 

Kwa mujibu wa mfululizo wa Ibada za kijamii katika Kanisa Halisi la MUNGU BABA Mwezi huu, wanaofuata ni BODABODA Lango la 12 Eluli, Vol.2 (24 Oktoba, 2021); MAMA/BABA LISHE wao ni Lango la 19 Eluli, Vol.2 (31 Oktoba, 2021); wakati WAFANYA BIASHARA NDOGO NDOGO itakuwa Lango la 26 Eluli, Vol.2 (7 Novemba, 2021)

 

NINI DHUMUNI LA KANISA KUFANYA IBADA ZA KIJAMII?

Katika Ufunuo 11:1-2, inasomeka kuwa wakati wa Majira ya Mwana, mafundisho ya Kanisa yalikuwa ya kuhudumia Behewa la Ndani peke yake, ikiwa na maana ya Mchungaji kuhudumia washirika wake tu. Hali hiyo ya kuhudumia walioko ndani ya jengo peke yake, iliendelea kwa kuwa katika mistari hiyo miwili, imeandikwa kuwa Behewa la Nje (yaani Jamii), walipewa Mataifa. Hata katika Matendo 2:42-47, inathibitisha hivyo kwa kuwa baada ya Yesu kuwaeleza Wanafunzi kwamba watafundisha habari zake kuanzia walipo [Yerusalemu], kisha waende Yudea mpaka Samaria na mwisho wa nchi (Matendo 1:8), hawakufanya hivyo mpaka pale adha ilipotokea kwao ndipo wakakubali kutawanyika kwenda kuihudumia jamii (Matendo 8:1-).

 

Kulikuwepo pia na msingi mbaya kuanzia kwa Musa, Eliya Mtishbi na Yesu, ambao hawakuwa na mahusiano mazuri na Taifa (kwa wakati wao), uliosababisha mfumo huo kuendelea kwa wale tuishio leo. Baada ya CHANZO HALISI kuja juu ya Nchi ambaye ni Mungu Mmoja Baba wa Wote, aliyeko Juu ya Yote na ndani ya Yote, amevunja huo msingi mbaya. Yeye anataka Kanisa lishirikiane na Jamii.

 

Katika Efeso 3:10, kuna mstari ambao haujawahi kufanyiwa kazi na Kanisa. Mstari huo unasema kuwa “ili sasa kwa Barabara [njia] ya Kanisa, Hekima ya Mungu iliyoya Namna nyingi, ijulikane kwa Falme na Mamlaka katika Ulimwengu wa Roho”.

 

Kilichosababisha mstari huo usifanyiwe kazi, ni kwa kuwa katika Majira zilizopita, ilikuwa sio rahisi kupata Kanisa ambalo halishindwi na malango ya kuzimu (Mathayo 16:18). Ila kwa kuwa Kanisa lisiloshindwa na malango ya kuzimu lipo, basi ushirikiano wa Kanisa na Jamii ni wakati wake.

 

FALME NA MAMLAKA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO NI KITU GANI?

Ukitaka kujua falme na Mamlaka katika Ulimwengu wa roho ni nini, tafakari milipuko kama vile: Kipindupindu; Ukimwi; Mafua ya Ndege; Volcano; Sunami; Kimbunga Jobu; Milipuko ya Moto kwenye Magorofa na majengo mbalimbali; ajali za Treni, Meli, Ndege, Magari, pikipiki; vita, mafuriko ya mvua; na kadhalika.

 

Haya yote (pamoja na idara ya majanga kuwepo), ni kazi ya Kanisa kuyazuia yasitokee. Tukiwalaumu viongozi wa kisiasa ni Kosa. Maana ukiona kiongozi wa kisiasa amekosea, ujue kwa mujibu wa Efeso3:10, wewe mwananchi ndiye hujamwinua kwenye Shukrani (Maombi) sawa sawa. Maana katika 2Nyakati 7:14-16, inasomeka kuwa ‘‘ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinynyekesha na kuacha mambo yao mabaya na kuomba nitasikia na kuponya nchi yao”. Hivyo, ina maana kuwa jamii ikimwinua kiongozi yeyote lazima huyo kiongozi afanye vizuri. Katika Yeremia 5:1, imeandikwa kuwa CHANZO CHA MEMA NA MAZURI anatafuta mmoja tu katika mji anayetenda kwa haki, akimpata huyo anaponya mji au nchi yote.

 

Katika I Timotheo 2:1-4, kitabu kinasema kwamba kabla ya kufanya chochote: Shukrani; Maombi; Dua; Sala na maombezi vifanyike kwa ajili ya walioko madarakani ili Jamii tuishi kwa Amani na Utulivu. Kitabu kinasema hilo ni zuri nalo lapendeza kwa Mungu Mwokozi wetu. 

 

Tatizo lililokuwa bado lipo kwa wote, ni kutokuwa na Upendo usiobagua. Wengi wanapenda kuombea vitu ambavyo vinawapa maslahi binafsi. Hata hivyo, wajibu wa Kanisa sio huo wa kutafuta Maslahi binafsi, bali wajibu wa Kanisa ni kufuta shida mbali mbali ambazo husababishwa na falme na mamlaka katika ulimwengu roho ndani ya jamii.

 

Kilichokuwa kinasababisha Jamii katika Mataifa mengi wapatwe na shida na majanga, ni kukosekana kwa Kanisa la Kweli ambalo linauwezo wa kushinda malango ya kuzimu, kama ilivyoandikwa katika Mathayo 16:18. Jamii yoyote ambayo ina Kanisa la Kweli haipatwi na vurugu kama hizo (Isaya 65:16).

 

MWALIKO WA BODA BODA; MAMA/BABA LISHE; NA MACHINGA NI WA NINI?

Wengine wanauliza. Je! Na Baba Halisi ameshaanza kutafuta umaarufu kama wengine? Jibu ni Hapana. Makundi haya matatu ni sehemu ya Jamii na wao wanahitaji upendo usiobagua kutoka kwa Aliyewaumba (Efeso 4:6).

 

Kwa kuwa Kanisa Halisi linaongozwa na Sauti kutoka kwa MUUMBA WA VYOTE, tumepata Sauti ya kuwahudumia BODABODA, MAMA/BABA LISHE na MACHINGA kama tulivyofanya kwa Waandishi wa Habari Lango 5 Eluli, Vol.2 (17 Oktoba, 2021).

 

Mwezi utakaofuata, tutafanya hivyo kwa Mitume, Manabii, Wachungaji, Wainjilisti na Waalimu ili nao wapate upendeleo kutoka kwa MUUMBA WA VYOTE kama tulio nao wa kufahamu SURA HALISI YA KANISA NI IPI. Maana Efeso 4:6 inasema Mungu ni Mmoja, ni Baba wa Wote, Aliye juu ya yote na ndani ya yote. Amekuja ili ageuze uteka wa kila mmoja (Ayubu 42:10).

 

HITIMISHO

Tulianza na Waandishi wa Habari kwa kuwa, walitamkiwa magumu na Yesu katika Mathayo 23:1-. Wanaofuata ni Bodaboda kwa kuwa ajali zinazotokea kwao ni nyingi mno. Tunatakiwa kuzifuta hizo ajali kwa Damu Safi Nyeupe (Mathayo 26:29/Ufunuo 11:6), hakuna kizuizi, kwa kuwa majira yake kufanya hivyo imefika. Tuna shuhuda nyingi kwa kuwa hakuna tuliyemuombea asijibiwe. Hivyo, tunapenda kusema kwa Jamii na hasa bodaboda wote karibuni tufute suala la kupatwa na ajali za mara kwa mara. 

HERI MLIOBARIKIWA KULIKO WOTE.


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages