LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 15, 2021

KANISA HALISI LANENA, MATENDO MAZURI TUNAYOFANYA WAKATI WA UZALISHAJI NDIYO IBADA YENYEWE

Kiongzi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, Baba Halisi wa Uzao akisisitiza jambo wakati akiendesha Ibada ya Mauzo na Uzalishaji' iliyoambatana na Maonyesho ya Huduma na bidhaa mbalimbali za Wazalishaji, iliyofanyika Jumapili iliyopita, Oktoba 10/ 201 Makao Makuu ya Kanisa hilo, Tegeta Dar es Salaam.

 

Na CCM Blog. Tegeta
Kanisa Halisi la Mungu Baba lililopo Tegeta Namanga jijini Dar es Salaam, limekuwa likiendesha Ibada zake mara kwa mara hususan siku za Jumapili, na ibada hizo zote huonyesha  kuwa zimeacha alama bora na imarata kwa waaumini wake ambao kulingana na Kanisa hilo wanafamika kwa jina la Uzao Halisi.

Ibada zilizo kubwa huendeshwa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo anayetambulika kwa jina la Baba Halisi wa Uzao.

Katika Ibada ambazo zimewahi kushuhudiwa na Mwandishi wa habari hii, japo zote zimekuwa na mada motomoto kutoka kwa Baba Halisi wa Uzao, Ibada iliyofaanyika Jumapili ya Oktoba 10, 2021 (26 Abu Vol.2) naweza kuandika kuwa ilikuwa ya kipekee mno.

Ibada hiyo ambayo ilihudhuriwa na Uzao pomoni, ilikuwa ya aina yake kwa kuwa, mada yake ilikuwa inahusu zaidi jamii kwa kuwa ililenga kuwafunda Waumini wa Kanisa hilo na wananchi kwa jumla kwamba, wanapaswa kujua kuwa Ibada iliyo njema na sahihi mbele za Mungu ni kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi afanye kazi kwa Bidii, juhudi, maarifa na uadilifu.
 
Katika ibada hiyo ambayo ilitwa ' Ibada ya Mauzo na Uzalishaji' iliambatana na maonyesho ya huduma na bidhaa mbalimbali za Wazalishaji.

Akizindua rasmi Ibada hiyo, Baba Halisi alifafanua kwa kina akirejea katika Biblia kwamba mtu akifanya kazi yoyote halali na akaitenda kwa uaminifu basi hiyo ndiyo ibada yenyewe.

"Ukiendesha Bodaboda, ukawatendea haki abiria wako, au Mama lishe akawatendea haki wateja wake hiyo ndiyo ibada. hata ukiwa mtoa huduma kwenye ofisi ukiwatendea haki wateja bila kuomba rushwa au kuonyesha dharau kwa kuangalia umhuduie kwanza nani umbague hiyo ndiyo Ibada.

Hata Mwandishi wa habari, akiandika habari zake kwa uadilifu ni ibada, hata mwanafunzi akisoma masomo kwa bidii, juhudi na maarifa na akawa mwadilifu katika usomaji wake hiyo pia ni ibada, hata viongozi wa duni, akiongoza vizuri nayo ni kazi hiyo wakiitenda kwa uadilifu ndiyo ibada yenyewe", alisisitiza Baba Halisi wa Uzao na kuendelea kutoka mifano mbalimbali kudhuhirisha kuwa Kazi yoyote halali ikifanywa kwa uadilifu ndiyo ibada yenyewe.

Baba Halisi amesema, kutokana na umuhimu, Kanisa hilo litakuwa linaifanya ibada hiyo ya Uzalishaji mali hadi pale jamii itakapoelewa kuwa ibada ni uzalishaji na sio kulia na kuomboleza tu kwenye nyumba za ibada.

"Tulipoanza ibada katika 'level' ya unabii maswali yalikuwa mengi, mbona Yesu alipindua meza za wafanyabishara hekaluni. Nisikilizeni kwa makini, Yesu alipopindua meza hizo hakumaanisha kukataa uzalishaji bali wapangaji wabaya ikiwemo uzinzi, uasherati, wivu, chuki na kiburi vitoke mioyoni." Amesema.

Aidha ameitaka jamii kufanya kila kitu kwa utii na haki wakiwemo wanafunzi kwa kusoma kwa bidii na utii, madaktari kutoa huduma kwa haki na madereva kuendesha vizuri na kwa halali na kwa kufanya hivyo ni ibada.

Kanisa Halisi la Baba Mungu ambalo limeanzishwa mwaka 2018, lina vituo nchi nzima na mataifa 136 na limejijenga katika misingi ya imani, amani, upendo, matendo mema na ibada hiyo ya uzalishaji mali.

Katika Ibada hiyo Kanisa liliwakutanisha watoa huduma, wazalishaji na wafanyabishara mbalimbali kwa ajili ya kuuza na kutangaza bidhaa zao ambapo miongoni waliohudhuria ni Kina mama wajasiriamali watano kutoka Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Kunduchi.

Kina mama hao ambao baadhi yao walipata mikopo isiyo na riba ambayo hutolewa na Serikali kupitia Halmashauri zote nchini waliweza kupewa na Kanisa hilo nafsi za kuonyesha bidhaa zao bila kutoa gharama yoyote.

Yafuatayo ni Maneno ya Baba Halisi aliyoyasoma wakati wa Ibada hiyo



Kuanzia lango (siku) Kanisa Halisi la MUNGU BABA lilipoanza kufundisha kuwa Ibada ni Uzalishaji,kulitokea maswali ndani na nje ya Kanisa! Walioko ndani ya Kanisa walikutana na kile alichofanya Yesu alipoingia ndani ya Hekalu akakuta Meza za wafanyabiashara na kuzipiga mateke huku akisema nyumba ya Baba yake ni ya sala(Mathayo 21:12-13).Hawakujua kuwa Yesu alikuwa na maana ya kufukuza wapangaji wabaya ndani ya Moyo, ambao wanatakiwa kufutika ili Mzalishaji azalishe utajiri kwa amani, wapangaji hao ni wale walioandikwa katika Marko7:21-23.

 

Walioko nje ya Kanisa wao waliona ni mafundisho yasiyoeleweka kwa kuwa walifundishwa kuwa Kanisani ni mahali pa kwenda kumlilia MUNGU wakati wa shida na taabu peke yake.Hawakukumbuka kuwa, wakati wa kuumba kwa mara ya kwanza, MUNGU BABA yaani CHANZO CHA MEMA NA MAZURI, alianza kwa kuweka HESHIMA na UTAJIRI ndani ya ule Moyo wa Mwanzo aliouengua kushoto kwake (Mithali 3:16).

 

Aidha, hawakukumbuka kuwa Adamu akiwa bado kwenye kitanga cha Mkono wa CHANZO CHA MEMA NA MAZURI, aliambiwa azalishe, atiishe, aongezeke na amiliki kila kilichoumbwa (Mwanzo 1:28). Katika yote aliyoambiwa hapo juu la kwanzaaliloambiwa Adamu ni kuzalisha. Baada ya Adamu kutoka kwenye kitanga cha Mkono wa MUUMBA WA VYOTE, WOTE NA YOTE na kuonekana wazi, aliambiwa pia azalishe kwa maana ya kulima na kutunza Bustani ya Edeni (Mwanzo 2:7-15).

 

Kulima na kutunza Bustani ina maana kazi yoyote ya halali unayoifanya ni kulima na kutunza.Hiyo ndiyo ibada ambayo CHANZO HALISI aliitaka tangu anaanza kuumba hadi sasa. Waliobadilisha kusudi hilo la CHANZO CHA MEMA NA MAZURI, ni Watumishi ambao walipewa kusimamia shamba lake (Mathayo 21:33-40).

 

KUSUDI LA ALIYEUMBA VYOTE, WOTE NA YOTE NI LIPI?

Hekima ya yeyote ni jinsi anavyoanza na anavyomaliza kila anachokifanya.Tumeona katika ufunguo kuwa mahali CHANZO CHA MEMA NA MAZURI alipoanzia wakati wa kumuumba Mtu ni kuzalisha (Mwanzo 1:28). Mahali alipomalizia wakati wa kumuumba Adamu ni kwenye uzalishaji (Mwanzo2:15). Ukiuliza Wanatheolojia wote, wanakubali kuwa anachotaka MUUMBA WA VYOTE, WOTE NA YOTE ni kuabudiwa na kila alichoumba. Hata wakati anaengua Moyo wake wa Mwanzo upande wa kushoto ili aumbe Mbingu na Nchi (Mwanzo 1:1),alitaka kile alichokisikia katika Moyo wake(Zaburi 98), kitokeze ili kumuabudu kwa uhalisia na kweli (Yohana 4:23).Hivyo,alichoanza nacho kwa Adamu akiwa bado kwenye Kitanga cha Mkono wake na kukisisitiza baada ya kumuumba Adamu, hiyo ndiyo ibada anayoitaka kwa kila aliyeumbwa, yaani Uzalishaji.  Ndiyo maana kwenye Moyo wa Mwanzo baada ya kuuengua kushoto kwake, aliweka heshima na utajiri(Mithali 3:16).

 

Kuna mifano mbalimbali ya Ibada ni uzalishaji katika kitabu: Nuhukatika Mwanzo 7:1, tunasoma kuwaalikuwa mwenye haki. Ili ujue kuwa Ibada ni Uzalishaji, Nuhu alitoa ibada kwa CHANZO CHA MEMA NA MAZURI akiwa akiwa anatengeneza Meli au Safina. Ibrahimiambaye alipewa kibali cha kuwa Baba wa Mataifa yote kwa vizazi vinne (Mwanzo 15:16), nayealitoa ibada kupitia Uzalishaji wa mifugo, madini na dhahabu (Mwanzo 13:2).

 

KatikaMwanzo 26:12-25, tunasoma habari za Isaka kuwa naye pia alitoa Ibada kwa CHANZO HALISI kupitia Uzalishaji Shambani.Yakobo ambaye naye alikuwa mwenye haki, alitoa Ibada kwa Barabara ya Uzalishaji kwa mujibu wa Mwanzo 30:37-43. Kana kwamba hiyo haitoshi, Yusufuambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Misri,naye alitoa ibada kwa CHANZO HALISI kupitia uzalishaji kwa mujibu wa Mwanzo 41:41-45.

 

Baada ya kitabu cha Mwanzo kuisha, wakati waWana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri kwenda Kaanani, ndipo Musa alipolazimika kuwa na Hema ya Kukutania ili ajue wale anaowaongoza njiani wameshindaje? Kwa kuwa walikuwa wanakuja na Matunda (Sadaka) kwa Musa, Mitume na Manabii waliofuata baada ya Musa walipenda hiyo barabara ya kutoa Ibada kwa kukusanyikia Hemani.Pamoja na hayo Kusudi la CHANZO CHA MEMA NA MAZURI halikubadilika, maanahadi sasa bado Ibada ni Uzalishaji.

 

Katika Kipindi hiki, kitu cha kurekebisha ni hiki;waumini na wafuasi wa Dini na Madhehebu mbali mbali wakijenga shule, vituo vya kuwekea nishati, na ofisi za makampuni yao huwa wanajenga na hema ya kukutania hapo ofisini! Kwa kufanya hivyo wanaamini kuwa kutoa Ibada ni lazima uingie kwenye hema ya kukutania ndipo CHANZO HALISI akusikie na kupokea ibada. Kumbe ibada inayotakiwa ni wewe kufanya kazi ambayo ni halali.

 

Kama Mwalimuanafundisha kwa upendo watoto wakafaulu, hiyo niIbada.Daktari au Muuguzianayefanya kazi yake kwa upendo, hiyo ni Ibada. Mwanafunzi anayesoma kwa Upendo na utii, hiyo ni ibada. Dereva anayeendesha boda boda, daladala, basi laabiria kwenda mkoani au lori la bidhaa kwa haki, hiyo ni ibada anayoitaka CHANZO HALISI.Mfanyabiashara asiyelegeza mizani wakati wakupima sukari na unga wa ngano dukani, hiyo ni ibada ikiwa na maana ya harufu ya manukatokwa CHANZO HALISI. 

 

Kuhani anayehifadhi maarifa kinywani mwake (Malaki 2:7), nakuhudumia Uzao halisi kwa haki, hiyo ndiyo Ibada. Wewe unayesoma ujumbe huu ukiwa ofisini, na ofisi hiyo uliipata kwa Haki na kila anayekuja unamhudumia kwa haki, hiyo ndiyo Ibada, nakadhalika.

 

Katika kuhitimisha, tuelewe kuwa sijasema Mitume, na Manabii wabomoe nyumba zao za Ibada; bali nimesema kuwa twende kwenye Nyumba za Ibada kwa ajili ya kumrudishia CHANZO HALISI sifa, heshima, shukrani na utukufu(Isaya 42:8)kwa kutuwezesha kuzalishaji na kupata utajiri udumuo; huku tukijua kuwa ibada hasa ni ile tunayoifanya wakati wa uzalishaji.Karibuni wote.

 

Uzao wakiwa wamejaa Kanisani wakati Kiongzi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, Baba Halisi wa Uzao akikamilisha  kuendesha Ibada ya Mauzo na Uzalishaji' iliyoambatana na Maonyesho ya Huduma na bidhaa mbalimbali za Wazalishaji, iliyofanyika Jumapili iliyopita, Oktoba 10/ 201 Makao Makuu ya Kanisa hilo, Tegeta Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages