New York, Marekani
Wakati Rais Samia Suluhu Hassan, leo Septemba 23, 2021 atahutubia Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) unaoendelea hapa New York nchini Marekani, jana alishiriki mkutano wa pamoja kati ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Marekani.
Taarifa ya Ikulu imesema, katika Mkutano huo Rais Samia amehimiza kuimarishwa kwa biashara kati ya mataifa hayo mawili ili kuwa na faida kwa pande zote.
Rais Samia amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa kwa sasa biashara zinazofanyika kati ya Tanzania na Marekani ni ndogo ikilinganishwa na fursa zilizopo.
Amesema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2019, Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 241 na kuuza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 46.
Kwa upande mwingine Marekani imewekeza Tanzania Dola za Kimarekani bilioni 5.55 na kuajiri watu 44,118 wakati Tanzania imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni moja tu ambacho ni kiasi kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa uchumi wa Marekani duniani na fursa zilizopo Tanzania.
Rais Samia amewaeleza wafanyabishara hao kuwa angependa kuona biashara inaongezeka kwa kuwa Tanzania ni mwanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na pia Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo zinatoa fursa za wawekezaji na wafanyabishara wa Marekani kwa soko la watu milioni 450, hivyo kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji.
Aidha, Rais Samia pia amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa Tanzania imesaini mkataba wa Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA) ambao umelegeza masharti ya biashara na kuunganisha soko la watu bilioni 1.3.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwenye mkutano wa pamoja kati ya Wafanya Biashara wa Tanzania na Marekani, Septemba 22, 2021 Jijini New York
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇