WaziriI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameipongeza Benki ya NMB kwa kuwa mshirika mkubwa wa serikali katika kuleta maendeleo kwenye sekta mbalimbali hasa elimu na afya.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mbio za NMB Marathon 2021, zilizoandaliwa na Benki ya NMB kwa kushirikiana na Hospitali ya CCBRT kwa lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kuchangia matibabu ya akina mama wenye tatizo la Fistula.Mbio hizo zenye kauli mbiu ya Mwendo wa Upendo zilikusanya shilingi milioni 400 zitakazosaidia matibabu ya akina mama 100 wanaosumbuliwa na tatizo la Fistula katika hospitali ya CCBRT.
Awali, NMB ilikusudia kukusanya sh. Bilioni moja ndani ya miaka minne-inamana kila mwaka sh. Milioni 250, hivyo wamevuka lengo lao la mwaka huu.
Mheshimiwa Majaliwa alibainisha kuwa tatizo la Fistula linawatesa sana akina mama, hivyo NMB kufikiria kuchangisha fedha kupitia Marathon ya Mwendo wa Upendo ni jambo la kipekee ambalo haliwezi kusahauliwa kirahisi kwa kila atakayeguswa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alisema wameamua kuja na mpango huo baada ya kuona namna akina mama wanavyoteswa na tatizo la Fistula, gharama ni kubwa na wengi wanashindwa kukidhi. Lakini sasa benki yake ina uhakika kuwa akina mama 100 watapata matibabu.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Doroth Gwajima aliipongeza NMB kwa mchango huu mkubwa kusaidia kutokomeza matatizo yanayorudisha nyuma maendeleo na kushusha utu wa mwanamke katika jamii.
Fistula ni hali inayosababishwa na uzazi pingamizi ambapo kwa mujibu wa takwimu za UNFPA, Tanzania hivi sasa kuna akina mama zaidi ya 10,000 wenye Fistula na takribani wagonjwa wapya 3,000 huongezeka kila mwaka lakini wagonjwa 1,300 pekee ndio wanaopata matibabu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇