CCM Blog, Dodoma
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa maelekezo kwa Serikali kuhusu namna njia bora ya ununuzi wa mahindi ya wakulima ikiwemo kuweka vutuo maalum vya kuyanunulia huku ikitoa bei sawa kwa wakulima kutoka maeneo yote.
Pia CCM imeziagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kilimo kukaa na kujadili kwa pamoja ili kutafuta unafuu wa bei ya ununuzi wa mbolea kwa wakulima.
Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo katika mkutano wake na waandishi wa Habari, uliofanyika leo, Ofisini kwake, Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma.
Katibu Mkuu amesema CCM imefikia hatua aya kutoa maelekezo hayo, baada ya kusikia malalamiko ya wakulima kuhusu uhaba wa masoko ya mahindi, ambapo Chama kimeilekeza Serikali kutafuta fedha kwa ajili ya kununua mahindi katika mikoa yenye uzalishaji mkubwa.
"Baada ya maagizo ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika ziara ya mwezi Julai mwaka huu kwenye mikoa ya Rukwa, Songwe na Mbeya, kuhusu utafutaji wa masoko ya mahindi, NFRA na Bodi ya Mazao Mchanganyiko ilitenga fedha kununua mahindi.
Na taarifa zilizopo ununuzi unasuasua kutokakana na fedha kuisha, sasa hatuwezi kukaa namna hii wakulima wetu hawana pa kuuza mahindi yao, hivyo maagizo ya Chama kwa serikali, watafute fedha popote wanapojua na suala la kununua mahindi liendelee kwenye maeneo yote ya uzalishaji." Ameelekeza Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo.
Aidha, katika Hatua nyingine, baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wakulima kuhusu uchache wa vituo vya ununuzi wa mahindi, Chama kimeilekeza serikali kupitia Wizara ya Kilimo, kuongeza vituo vya ununuzi na gharama za usafiri wasibebeshwe wakulima kama inavyofanyika sasa kwa wakulima waliopo pembezoni mwa vituo vya ununuzi badala yake bei iwe sawa kwa wakulima wote..
Kuhusu changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea, Katibu Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango kukutana haraka kwa ajili ya kuangalia namna ya kupunguza mzigo kwa wakulima baada ya ongezeka kubwa la bei ya mbolea kutoka shilingi 50,000 kwa mfuko wa kilo 50 na sasa kupanda hadi kufikia sh.85,000 sababu kubwa ikiwa ni katokana na athari za janga la Uviko 19 lililoikumba Dunia nzima.
Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo akizungumza na Waandishi wa Habari, leo jijini Dodoma
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇