WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 12 la Wanawake Waombolezao Kitaifa ambapo ameruhusu makongamano ya dini yanayoombea amani nchini.
Waziri Simbachawene akikabidhiwa zawadi ya vitabu na Askofu Malasa
Wakiomba na kuimba
Mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Tunu Pinda (kulia) akiwa miongoni mwa wageni waalikwa kwenye kongamano hilo.
Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia na Jamii wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Grace Mwangwa akihutubia wakati wa kongamano hilo.
Wakiendelea na maombi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ameruhusu makongamano ya dini yanaoombea amani na utulivu nchini.
Simbachawene ameruhusu makongamano hayo alipokuwa akihutubia katika Kongamano la 12 la Wanawake Waombolezao Kitaifa katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma alipoalikwa kuwa mgeni rasmi leo Agosti 12, 2021.
"Endeleeni na makongamano ya kuliombea Taifa, amani na utulivu ni ajenda yetu ya kudumu, si rahisi kama ulivyotokea msiba wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli na kuzikwa kwa heshima zote bila kufinyana,"amesema Waziri Simbachawene.
"Nitumie jukwaa hili kuwaomba waendelee kuliombea Taifa letu liwe na amani na utulivu, kupitia hayo maombi tunapata ndiyo maendeleo, kuna nchi kubwa zenye utajiri zinashindwa kupata maendeleo kwa vile muda wote wako kwenye mapigano," amesisitiza Waziri Simbachawene.
Amesema kuwa kuna wakati fulani mambo yakiwazidi serikalini huwaomba viongozi wa dini wawasaidie kuweka mambo sawa na inakuwa.
Licha ya wanawake hao waombolezaji kuiombea mihimili mitatu ya nchi yaani Serikali, Bunge na Mahakama, pia wamemuombea Rais Samia Suluhu Hassan aliongoze Taifa kwa hekima, busara na kwa mafanikio makubwa.
Naye Mwenyekiti wa Mkesha Mkuu Dua Maalumu kwa Taifa, Askofu Godfrey Malasa amesema kuwa wanashukuru ushirikiano uliopo kuanzia Awamu ya Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, John Magufuli na sasa Samia Suluhu Hassani wote walikuwa mstari wa mbele nchi kuiweka mbele ya Mungu.
Askofu Malasa ambaye ni miongoni mwa waasisi wa kongamano hilo la wanawake waombolezao, amesema kuwa Viongozi wa kiroho wana kazi ya kuwahubiria wananchi kwenda sawa na nchi yao. "Tunakuwa bega kwa bega, tunashirikiana. Wao kimwili sisi kiroho."
"Taifa letu limebarikiwa na Uongozi umebarikiwa jambo ambalo linawashangaza walimwengu. Wanawake msonge mbele msirudi nyuma. Hata sasa tuna imani kubwa sana kuhusu kilio chenu, hata janga la corona Mungu atasikia na atajibu. Naamini kwamba roho Mtakatifu yupo kati yetu, maombi yetu Mungu atakwenda kujibu. Naamini moto huu wa maombi utakwenda hadi mikoani." amesema Askofu Malasia.
Mwenyekiti wa Kongamano hilo kwa Mkoa wa Dodoma,Dkt. Juliani Manyerere ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi hiki cha janga la Corona kuruhuru shughuli za kiuchumi, siasa na kijamii ikiwemo kongamano hilo.
Amesema kuwa tangu waanzishe kongamano hilo, wamepata faida kwa kutoa huduma ya kuwatembelea wenye uhitaji ambapo hivi karibuni waliwatembelea wafungwa wanawake katika Gereza la Segerea Dar es Salaam kwa kuwapatia misaada mbalimbali pamoja na kuwahubiria neno la Mungu ili wakitoka wawe na maadili mema.
Kongamano hilo limehudhuriwa na wanawake wachungaji wa madhehebu mbalimbali pamoja na waumini kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Imeandaliwa na Richard Mwaikenda
Mhariri Blog ya Taifa ya CCM
0754264203
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇